Eneo la bwawa la asili la Mdenga lililofukiwa
kinyume cha sheria na kampuni ya SBS inayojishughulisha na urejelezaji wa taka
mkoani Mtwara na kusababisha uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.
Na Mwandishi Wetu, Dar
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira,
Ummy Mwalimu, ameutaka uongozi wa kiwanda cha OK Plastic kilicho jijini Dar es
Salaam, kuwasilisha mara moja ripoti ya mwaka ya ukaguzi wa mazingira kwa
baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Alisema hayo Jumatano wiki hii alipofanya
ziara katika kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara zake katika viwanda
mbalimbali nchini kuangalia hali ya utunzwaji wa mazingira hasa baada ya
wananchi kulalamika kuwepo kwa uchafu wa mazingira katika maeneo ya viwanda
katika mikoa mbalimbali.
Aidha, Ummy alitoa agizo kwa kiwanda hicho
kusimamisha mara moja kutupa taka ngumu katika dampo la Kinyamwezi, kwa sababu
ni hatari kwa afya za wakazi wa eneo hilo.
“Kwanini mnafanya hivi, naagiza msitishe mara
moja kutupa taka ngumu katika dampo wala msichome mabaki ya taka katika eneo la
kiwanda na mkiendelea nitahakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa juu yenu
kwa sababu mambo haya si ya kuyaacha yapite ivihivi,” alisema Ummy.
Aliongeza kuwa agizo hilo si kwa kiwanda cha
OK Plastic peke yake bali ni viwanda vyote vya ndani na nje ya jiji hili
kuhakikisha vinatunza mazingira na kuacha kuchoma taka za viwandani kwani moshi
unaofuka husambaza hewa ya semu kwa wakazi wa jirani na viwanda hivyo hali
inayohatarisha afya za binadamu.
Jumatatu wiki hii Ummy, alikuwa katika ziara kwenye
mikoa ya Kusini hasa Mkoani Mtwara katika eneo la Mdenga, Manispaa ya Mtwara
kwa lengo la kuitikia wito wa wananchi waliotoa malalamiko kwa Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alipofanya ziara katika mikoa
hiyo na kulalamika kuhusu uchafuzi wa mazingira.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alitembelea
viwanda vidogo vya ubanguaji korosho na maeneo mengine kama bwawa la asili la Mdenga
mablo kwa sasa limefukiwa kutokana na shughuli zinazoendeshwa na kiwanda cha
SBS kinachoshugulika na kuzirudisha taka katika matumizi (Recycling).
Ziara hizo ni muendelezo wa ziara nyingi zinazoendelea
kufanywa na viongizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, zikiwa na lengo la kuhakikisha
mazingira yanahifadhiwa na kutunzwa. |
EmoticonEmoticon