WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amewasili jijini Doha, Qatar jana usiku (Jumamosi, Desemba 20, 2014) kwa
ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa
kuanza leo.
Lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni
kukuza mahusiano baina ya nchi hizi mbili, kuangalia fursa za kiuchumi
na miradi mikubwa inayoweza kuzinufaisha nchi hizo na nje ya mipaka yake
kwenye Ghuba ya Arabuni (Arabian Gulf) na bara la Afrika.
Vile vile Waziri Mkuu anatarajiwa
kutangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania, fursa za biashara, za
utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta za uchimbaji gesi na
mafuta, usindikaji mazao, uvuvi na mifugo, ajira na uendelezaji
miundombinu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa
na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu
atakuwa na mazungumzo ya kiserikali na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh
Abdulla Nasser Al Thani. Vilevile atakutana na Mawaziri wa Kazi na
Ustawi wa Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na Uwekezaji wa nchi hii. Naibu
Mawaziri atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa Nishati.
Vilevile Waziri Mkuu amepangiwa
kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar
Business Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar
(Chamber of Commerce of the State of Qatar) na pia atakutana na
Watanzania waishio Qatar. Atatembelea pia Mamlaka ya Bandari ya Qatar na
makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya Qatar.
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na
Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa
Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge
wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali na wakuu wa taasisi za
TPSF na TPDC.
EmoticonEmoticon