YANGA KUANZA MAZOEZI NOVEMBA 24 BAADA YA MAPUMZIKO YA WIKI MBILI.

November 21, 2014
TIMU ya Dar es Salaam Young Africans inatarajia kuanza mazoezi Novemba 24 mwaka huu baada ya kuwa na mapumziko ya wiki mbili.
Maandalizi hayo yatakuwa ni kujiandaa na  mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC katikati ya mwezi Disemba mwaka huu.

Kocha mkuu wa Young Africans mbrazil Marcio Maximo alitoa mapumziko hayo kwa wachezaji wake, kufuatia baadhi ya wachezaji kuitwa na timu zao za Taifa kwa ajili ya mechi za kalenda ya FIFA na wengine kujiandaa na michuano ya Challenge Afrika Mashariki na Kati.

Wachezaji wa Young Africans walioitwa timu za Taifa ni (Tanzania), Deo Munish "Dida", Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub "Cannavaro", Saimon Msuva na Mrisho Ngasa (Rwanda) Haruna Niyonzima, (Uganda) Hamis Kizza.

Aidha kocha Maximo pamoja na wachezaji kutoka nchini Brazil kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Geilson Santos "Jaja" wako nchini Brazil kwa ajili ya mapumziko mafupi kabla ya kurejea kuendelea na maandalizi ya mechi za mzunguko wa nane.

Kocha msaidizi Leonardo Neiva amebakia nchini Tanzania, ambapo kwa sasa anaandaa programu ambayo itatumika kuanzia Novemba 24, 2014 pindi kikosi kitakapoanza tena maandalizi ya kujiandaa na michezo itakayofuata.

Wachezaj wote wanatarjiwa kuripoti Novemba 24, mwaka huu kwa ajili ya mazoezi ya kujiandaa kumalizia mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC. 
 chanzo:blog ya http://www.youngafricans.co.tz

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »