Waziri wa Ujenzi Dkt. John
Magufuli(kulia),akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam kuhusu ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 7.5 litakaloanzia
eneo la Aghakani na kuishia Coco beach, ujenzi huo unaotarajiwa kuanza
mapema mwakani na unafadhiliwa na Serikali ya watu wa Korea Kusini
,lengo ni kupunguza msongamano wa magari katika daraja la
Serender,kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Juma Iyombe.
(Picha Lorietha Laurence –Maelezo)
………………………………………………………………………………………..
Na Beatrice Lyimo -Maelezo
Zaidi ya Bilioni 110 zinatarajia
kutumika katika ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 7.5 ili
kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli
alisema daraja hilo litaanzia eneo la Aghakani na kuishia Coco beach.
Waziri Dkt. Magufuli alisema
daraja hilo litakalojengwa kwa msaada wa Serikali ya Korea Kusini
litakuwa na njia nne na barabara mbili za huduma kwa kila upande lenye
uwezo wa kupitisha magari elfu 61 kwa siku .
“Serikali ya Korea Kusini
imemaliza mradi wa ujenzi wa daraja la Kikwete pamoja na barabara ya
Malagalasi Mkoani Kigoma na sasa tumewaomba waendelee kutoa msaada kwa
ajili ya ujenzi wa barabara mkoani Dar es Salaama ili kupunguza
msongamano wa magari”, alisema Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
kutoka TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale amebainisha kuwa wataalamu
kutoka Korea Kusini wameshafanya Upembuzi yakinifu uliomalizika hivi
karibuni, hivyo ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa
mwaka ujao.
Aliongeza kuwa daraja hilo
litakalofahamika kwa jina la New Salender Bridge litaunganishwa na
barabara ya Ally Hassan Mwinyi kutokea Aghakani na kwa upande mwingine
litaunganishwa na barabara ya Chole iliyopo Masaki.
Serikali imeweka mikakati mingi
ya kupunguza msongamano wa foleni za magari kwa kuanzisha ujenzi mbadala
wa barabara za juu unaotarajiwa kujengwa maeneo ya TAZARA,Mbagala rangi
tatu hadi gerezani, kuanzishwa kwa kivuko cha Dar es Salaam hadi
Bagamoyo.
Pia utafanyika utanuzi wa
barabara nyingine za Dar es salaam kwenda Morogoro kupitia Chalinze na
ile ya Morocco hadi Mwenge na Bagamoyo hadi Msata.
EmoticonEmoticon