Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akihutubia Mkutano wa pili wa Kimataifa kuhusu Lishe na Virutubisho
(ICN2) uliofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Shirika la Kilimo na
Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome, Italia juzi Novemba 19,
2014.
Papa Francis, akihutubia wakati wa mkutano huo....
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akijadiliana jambo na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania wakati wa
mkutano huo wa ICN2 (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Italia, James
Nsekela na Msaidizi wa Rais katika Masuala ya Lishe Dkt. Wilbald Lorri.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akijadiliana jambo na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania wakati wa
mkutano huo wa ICN2 (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Italia, James
Nsekela na Balozi Wilfred Ngirwa (kulia).
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango Maalum wa
Chakula Duniani (WFP) Ethria Cousin (kulia) na Balozi Wilfred Ngirwa
wakati wa mkutano huo wa ICN2, uliofanyika juzi Novemba 19, 2014, Jijini
Rome Italy.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akifuatilia hotuba mbalimbali za viongozi walioshiriki katika
Mkutano huo wa ICN2. Kulia ni Mfalme Letsie III wa Lesotho.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa FAO
Jose Graziano da Silva, wakati alipomtembea ofisini kwake na kufanya
naye mazungmzo, juzi Novemba 19, 2014. Kushoto ni Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid.
*********************************************************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAKAMU
WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA
PILI WA KIMATAIFA KUHUSU LISHE NA VIRUTUBISHO JIJINI ROME, ITALIA
NOVEMBA 21, 2014
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
Novemba 19, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Pili wa
Kimataifa kuhusu Lishe na Virutubisho uliofanyika katika Makao Makuu ya
Shirika la Kilimo na Chakula la
Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome Italia.
Mkutano
huu umefanyika ikiwa ni miaka 22 baada ya mkutano wa kwanza maarufu kwa
jina la ICN1 kufanyika katika jiji la Rome na kuazimia kuwa, upo
umuhimu wa kuhakikisha binadamu wanapata Lishe bora yenye virutubisho
ili kusadia kujenga afya ya binadamu duniani. Mkutano huu wa pili pia
umeandaliwa kwa pamoja na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)
pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mkutano
huo ulifunguliwa na Balozi wa Kudumu wa Italia katika Umoja wa Mataifa
Gianni Ghisi aliyesoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Italia Giorgio
Napolitano ambapo alifafanua kuwa Rome inawakaribisha wawakilishi wan
chi mbalimbali na kwamba inatamani kuona mkutano huu unatoka na majibu
ya tatizo la lishe duni kwa watu wa mataifa mbalimbali.
Katika
siku ya ufunguzi pia hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon iliwasilishwa pamoja na uzoefu wa masuala ya Lishe kutoka Italia
ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia
Paolo Gentiloni aliwasilisha hotuba yake huku akiwakaribisha washiriki
wa mkutano huu wa ICN2 katika jiji la Rome na kufafanua kuhusu matarajio
ya Italia katika mkutano wa sasa ukilinganisha na ule uliofanyika miaka
22 iliyopita.
Akiwasilisha
taarifa ya Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib
Bilal alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa Maendeleo ambao wamekuwa
wakichangia katika sekta za Afya na Kilimo na akafafanua kuwa Tanzania
imepiga hatua tangu ICN1 na sasa inahitaji kuona mkutano huu unatoka na
maamuzi yanayotekelezeka ili kuwasaidia wananchi wa mataifa mbalimbali
hasa watoto na akina mama wajawazito kuwa na uhakika wa lishe bora yenye
virutubisho.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza
vifo vya akina mama na watoto ambavyo vingi vilitokana na lishe duni na
kwamba serikali ya Tanzania inaendelea kulipatia msukumo suala la lishe
na virutubisho kwa wananchi wenye uhitaji ili kujenga taifa lenye afya
na lenye watu wenye uwezo wa kusaidia nguvu zao katika kuleta maendeleo.
Akizungumza
siku ya pili ya Mkutano huo Baba Mtakatifu Fransis alisema haki ya
chakula bora si tu kuwa imetolewa na Mwenyezi Mungu kwa binadamu bali
pia ni haki inayoashiria utu na ambayo haipaswi kutolewa kama zawadi kwa
wanadamu.
Papa
Fransis aliendelea kusema kuwa, katika dunia ya sasa masuala ya
chakula, lishe na mazingira yametokea kuwaunganisha binadamu wa mataifa
yote sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma na akazitaka serikali za dunia
kuhakikisha zinapunguza utupaji wa vyakula sambamba na kuongeza mikakati
ya kuhakikisha kila mwanadamu anapata lishe bora.
ICN2
inatazama pia kuhakikisha kuwa nchi zinakuwa na mikakati ya kupunguza
utapiamlo na kwamba chakula kinachopatikana kiwe kile kilichoboreshwa
ama kuongezewa virutubisho ili kusaidia jamii zinazokabiliwa na matatizo
kama utapiamlo kuepukana nayo
na
hivyo kuwa na kizazi chenye afya bora na chenye uwezo wa kutumika
katika uzalishaji ama katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Dkt.
Margareth Chan, Mkurugenzi wa WHO aliueleza mkutano huo kuwa suala la
lishe ni mhimili katika kufanya jamii inayoweza kukabiliana na magonjwa
huku pia Mkurugenzi wa FAO Jose Graziano da Silva akifafanua kuwa,
shirika lake linautumia mkutano huu unaoshirikisha nchi 172 kutoa
mwongozo kwa dunia kuhusu jambo hili muhimu katika maisha na hasa sasa
ambapo tunaelekea kukamilika kwa Malengo ya Milenia na kuanza malengo
mapya.
Katika
mkutano huo, licha ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Tanzania pia
iliwakilishwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid
pamoja na Waziri wa Mifugo Dkt. Titus Kamani sambamba na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dkt. Mahadhi Juma Maalim.
Sambamba
na kuhudhuria mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata fursa ya
kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaishi Italia na kufanya nao
mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa sambamba na
kukutana na Mkurugenzi wa FAO ambaye alionesha furaha yake kuhusu hatua
mbalimbali ambazo Tanzania imepitia na kuahidi ushirikiano zaidi katika
masuala ya Kilimo.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais na ujumbe wake umeondoka kurejea nyumbani Tanzania
tayari kuendelea na shughuli nyingine za Kitaifa leo Ijumaa Novemba 21,
2014.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Rome, Italia
Novemba 21, 2014
EmoticonEmoticon