Na Khamis Haji , OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka Mamlaka zinazosimamia majengo
katika enelo la Mji Mkongwe Zanzibar kuwa na utaratibu mzuri wa
kuyakagua ili kuhakikisha uimara wake na kuepusha maafa kwa watumiaji na
jamii nzima.
Maalim Seif amesema hayo wakati
alipofanya ziara ya kukagua shughuli za uondoaji kifusi katika jengo
lililoanguka jana katika eneo la Shangani mjini Zanzibar, zoezi
linalofanywa na askari wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa pamoja na
wananchi wa Mji Mkongwe.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema nyumba
zilizopo katika Mji Mkongwe zinasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya
Mji Mkongwe au Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, hivyo taasisi hizo
ni jukumu lao kuzigagua uimara wake na kuhakikisha ni madhuti.
Amesema pale ambapo taasisi hizo
zitabaini kuna nyumba ambazo zimechakaa zinazoweza kuanguka na
kuhatarisha maisha ya watu na mali zao ni vyema kuwataka watumiaji wake
wahame, ili kuepusha kuangukiwa na nyumba hizo na kuhatarisha maisha
yao.
Katika ziara hiyo, ambapo alifuatana na
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis na Mwakilishi wa
Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe. Ismail Jusa Ladhu alivipongeza vikosi
vinavyoendesha shughuli za Uokoaji na wananchi wa Mji Mkongwe kwa kazi
kubwa ya uokozi wanayoifanya.
Naye Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na
Uokozi Makao Makuu, Ame Ali ambaye anaongoza shughuli za uokozi na
usafishaji wa eneo hilo amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na
walitarajia kuikamilisha leo.
Amesema jengo hilo lililoanguka jana asubuhi lilikuwa halikaliwi na watu kutokana nakukabiliwa na uchakavu na hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa kufuatia tukio hilo
crdtblog ya wananchi.
EmoticonEmoticon