KAULI YA WAZIRI MEMBE BUNGENI KUHUSU BIASHARA HARAMU YA PEMBE ZA NDOVU.

November 07, 2014
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe
Mheshimiwa Spika,
Siku ya Jana Vyombo vya Habari mbalimbali vya Ndani na Nje ya Nchi vilitoa habari kwamba ujumbe wa Rais wa China uliokuja nchini Miezi 18 iliyopita ulijihusisha na ununuzi wa pembe za ndovu nchini. Chanzo cha habari hizo ni taarifa ya taasisi isiyo ya kiserikali ya nchini Marekani ijulikanayo kama Environmental Investigation Agency (EIA). Habari hiyo imekwenda mbali zaidi kuituhumu nchi yetu na viongozi wake kutojali, wala kushughulikia tatizo la biashara haramu ya pembe za ndovu.

Mheshimiwa Spika,
Ninapenda kupitia Bunge lako tukufu kuutaarifu umma wa watanzania na dunia kwa ujumla kwamba madai yaliyotolewa na NGO hiyo ya Marekani ya kuihusisha ziara ya kihistoria ya Rais wa China kutembelea Tanzania kama nchi ya kwanza toka aingie madarakani na biashara ya pembe za ndovu hayana ukweli wowote. Vilevile, madai ya kwamba Serikali ya Tanzania haijali na wala haichukui hatua dhidi ya wanaojishughulisha na biashara haramu ya pembe za ndovu sio kweli.

Taarifa za EIA ni za kupikwa na kuungwa kuungwa ili kuchafua heshima ya nchi yetu, pamoja na kuchafua heshima ya rafiki zetu Taifa la China. Ni taarifa iliyoandaliwa na kutolewa wakati huu ili kukidhi ajenda mahususi ambayo tunaifahamu fika.
Mheshimiwa Spika,
Kabla sijaelezea kwanini ninasema taarifa hii sio ya kweli ningependa kwanza kulielezea Bunge lako tukufu mambo sita yafuatayo ambayo hayana ubishi:
1) Moja, ni kweli soko kubwa la pembe za ndovu lipo China. Wanaofanya biashara haramu ya pembe za ndovu hutafuta soko China;
2) Ni ukweli usiopingika kwamba pembe za ndovu nyingi zinazouzwa kwenye masoko haramu zinatokea Afrika, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zinapotoka pembe hizo;
3) Biashara hiyo haramu inahusisha wahalifu/ na mitandao ya waalifu ambao wana uraia wa nchi mbalimbali zikiwemo China na Tanzania;
4) Serikali ya Tanzania na Serikali ya China hazifanyi biashara haramu ya pembe za ndovu na wala hazihusiki na mitandao haramu.
5) Kwa kutambua ukubwa wa Tatizo la biashara hiyo haramu, Serikali zetu mbili zimekuwa na ushirikiano wa karibu kabisa katika kukabiliana na mitandao inayofanya biashara hiyo haramu. Vyombo vya dola vya nchi zetu mbili vimeshirikiana kwa karibu na kupashana habari kila wakati zilizowezesha kuwakamata wahusika wa biashara hiyo. Isitoshe wakati wa ziara iliyomalizika hivi majuzi Serikali zetu mbili zilisaini mkataba wa kutupatia vifaa vya kusaidia operesheni ya kupambana na ujangili wa wanyamapori – (China Aided Equipment for Forest Resources and Wildlife Conservation). Vilevile kwenye ziara hiyo tulisaini Mkataba wa kutupatia mitambo ya kisasa ya kufanya ukaguzi wa mizigo bandarini- ambayo itasaidia kubaini mizigo inayosafirishwa.
6) Tanzania na China zilishiriki kikamilifu kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara Haramu ya Pembe za ndovu (London Confrrence on Illegal Wildlife Trade) uliofanyika mwezi Februari 2014. Moja ya mafanikio makubwa ya mkutano huo ni kwa nchi za China, Botswana na Tanzania kusaini mkataba wa kupambana na biashara hiyo haramu. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa China kusaini Mkataba wa aina hiyo, jambo linalodhihirisha umakini wa Serikali ya Rais Xi Jinping kushughulikia tatizo la biashara haramu. Vilevile kabla ya mkutano huo wa London, Serikali ya China ilichoma moto hadharani shehena ya meno ya tembo haramu yaliyokuwa yakishikiliwa nchini humo.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe sababu kwanini ninasema habari za NGO ya EIA ni za uongo;
Mheshimiwa Spika,
Taarifa kama hii iliyotoka kwenye New York times sio mara ya kwanza kutolewa. Taarifa ya aina hii iliwahi kutolewa mwaka jana. Mtoa taarifa ambaye ametajwa kuwa chanzo cha habari ni mtu mmoja ambaye walimkuta barabarani na kuanza kumuuliza maswali. Mtu huyo sio mtumishi wa bandari wala uwanja wa ndege. Ni mpita njia tu wa mtaani. Hata video ya mahojiano inaonyesha hivyo. Ukiachilia mbali uwongo uliotolewa na bwana huyo, taasisi ya EIA imeongelea tukio la kontena lililokamatwa Bandarini likiwa na pembe za ndovu.
Ni kweli kabisa kwamba kontena la pembe lilikamatwa bandarini na vyombo vya dola. Jambo moja ambalo watu wengi hawalijui ni kwamba mafanikio ya operesheni ile yalitokana na ushirikiano wa vyombo vya usalama vya Tanzania na China. Taarifa za kiinteligensia juu ya operation hiyo zilitoka China na kuwasilishwa Tanzania ndio operesheni ikafanikiwa. Lakini habari zilizotoka kwenye mitandao zilisema kwamba Kontena limekamatwa likipelekwa kwenye meli ya kijeshi ya China...jambo ambalo sio kweli.
Mbali na hayo, ziara ha Rais Xi nchini ilikuwa ya masaa 24, na programu yake ilianza mara tu alipowasili nchini kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 4 usiku kwenye dhifa ya taifa. Siku ya pili ratiba ilianza asubuhi kwa uzunduzi wa Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Baada ya hapo Rais Xi na Ujumbe wake walikuwa na mikutano na Rais wa Zanzibar Mhe Dk.Ali Mohamed Shein na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe Benjamin William Mkapa. Baada ya hapo Rais Xi na ujumbe wake walienda kwenye makaburi ya Wachina kule Majohe na kisha wakaondoka kwenda uwanja wa ndege. Sasa hizo shopping zinazoelezewa kufanywa na ujumbe wa rais Xi zilifanyika saa ngapi?
Jambommuhimu kujiuliza, je hiyo taarifa ya Rais Xi na ujumbe wake kubeba pembe za ndovu iweje itoke leo? Kwanini wakati huu baada ya ziara ya Rais wetu nchini China? Kwanini itoke baada ya Mhe Rais kuhutubia mafanikio ya ziara yake nchini China?
Mheshimiwa Spika,
Jibu kila mmoja anaweza kujua. Wasambazaji wa taarifa hizi hawaitakii mema nchi yetu. Hawawatakii mema marafiki zetu wa China. Wamejawa na wivu na husuda kwa mafanikio ya China. Inashangaza kuona, wanawachukia huku wanawategemea. Wao wangependa wao peke yao wafanye biashara na China, wakachukue mikopo China, wavutie uwekezaji kutoka China, lakini tukifanya sisi waafrika inakuwa nongwa. Tusikubali upuuzi wa aina hii. Sisi ni taifa huru, hatutachaguliwa marafiki wala hatutarisishwa maadui. Tutaendeleza ushirikiano wetu wa kidugu na China na wala hatutorudi nyuma kamwe kutoka na maneno ya uwongo na uzushi.
Aidha, ninapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu Mheshimiwa Spika kwamba Serikali yetu haitorudi nyuma. Tutaendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya pembe za ndovu. Wale wote wanaoshughulika na biashara hizo, siku zao zimefikia mwisho.
Ahsanteni kwa kunisikili
crdt blog ya wannachi

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »