*Ataka Watanzania wajitokeze kwa wingi Oktoba 12
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kushangilia mechi ya viongozi
wa dini wa mkoa wa Dar es Salaam itakayochezwa Jumapili, Oktoba 12,
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi
(Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza na wachezaji wa timu za
AMANI na MSHIKAMANO zinazoundwa na Masheikh, Maaskofu, Maimamu na
Wachungaji kutoka madhehebu mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam ambao
wamepiga kambi mjini Morogoro.
“Hii haijapata kutokea… katika
hali ya kawaida mkusanyiko kama huu siyo rahisi na katika nchi nyingine
kupata mjumuiko kama huu haiwezekani,” alisema wakati akiongea nao
kwenye viwanja vya michezo vya taasisi ya Highlands Baptist Mission
iliyoko Kigurunyembe, Morogoro.
Alisema uamuzi wa viongozi wa
dini kukaa pamoja na kucheza mechi hiyo ni kutaka kuonyesha dhamira ya
kweli ya kufanya mshikamano na amani kuwa ajenda ya kudumu kwa Taifa
hili.
“Mimi ninaamini
kinachotuunganisha siyo dini bali ni kutambua kwamba sisi sote tumeumbwa
na Mungu… sisi sote ni bin-adam. Dini ni milango tu ya kutusaidia
tufike kule ambako Mwenyezi Mungu anataka tuende,” alisema.
“Ukichukulia mfano wa wakristo,
kuna madhehebu mengi. Kwa hiyo hawa wakigombana tayari ni tatizo. Hivyo
uamuzi wa kuwachanganya katika timu ni jambo zuri, ni kudumisha umoja,
amani na mshikamano,” aliongeza.
“Hii ni hatua ya kwanza kinachofuata sasa ni kuwa na One Destiny, One People, One Nation,”
akimaanisha kuwa na Lengo Moja, Watu Wamoja na Taifa Moja. Alisema hiyo
ni kama sura ya kwanza imefunguliwa hivyo, hawana budi kuendelea mbele.
Mapema, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Saleem alimweleza Waziri Mkuu kwamba
timu hizo ziko kambini hapo tangu Jumatano, Mei 8, 2014.
Alisema leo baada ya mazoezi
watakwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kurejea kambini
Morogoro. Wanatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho (Jumamosi)
tayari kwa pambano lao la Jumapili, Oktoba 12, 2014.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili
Morogoro jana mchana akitokea Dodoma, alifanya ziara ya siku kwa
kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine na leo atatembelea Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na Chuo Kikuu Huria kukagua miradi kama hiyo.
EmoticonEmoticon