SHIRIKISHO LA MUZIKI TANZANIA LATOA PONGEZI KWA BUNGE MAALUM LA KATIBA KWA KAZI NZURI.

October 09, 2014
Na Anitha Jonas –Maelezo.
 
SHIRIKISHO la Muziki Tanzania limetoa pongezi za dhati kwa Bunge Maalum  la Katiba lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Mhe. Samuel Sitta kwa kuingiza Ibara tatu katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa huko mjini Dodoma.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Addo November alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari hapo jana huku akisema kuwa Rasimu Inayopendekezwa imezingatia haki za Wasanii kwa kuingiza Ibara tatu zikiwemo Ibara ya 15, ya 38 (II)  na Ibara ya 56, 3 (e) ambazo Ibara hizo zinalinda kazi za muziki na sanaa zote kwa ujumla.
Bw. November alieleza kuwa Shirikisho limefurahi kuona kuwa Sheria ya inayohusu masuala ya kazi za sanaa katika nchini imeanza kutekelezwa Kikatiba kama ilivyo katika nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, Rwanda na Uingereza.
“Kwa kubainisha ibara hizi katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, zinaonyesha ulindaji wa Hati Miliki(Intellectual property) za Wasanii na kazi zao na hii itasaidia kuboresha maisha ya wasanii  kimapato kwa kupitia  kazi zao kwani Katiba hii itawalinda wasanii Kisheria”, alisema November.
Aliongeza kuwa Shirikisho limeingia Mkataba na Kampuni ya JB Belmont kwa kuweza kuwapatia wasanii na waandishi wa habari punguzo la bei katika huduma  mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.
Aidha, November aliwashauri waandishi wa habari kuunda Shirikisho la Waandishi wa habari la muziki kwani hii itasaidia kupata na kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii zinazohusu masuala ya muziki kwa kuaangalia walikotoka na wanakoelekea kimaendeleo.
 
Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya JB Belmont, Bi. Gillian Macheche alisema kuwa kutakuwa na punguzo la asilimia 40 kwa huduma mbalimbali ikiwemo kukodi Ukumbi wa Mkutano, Vyumba vya kulala wageni, vyakula na Vinywaji kwa wasanii na waandishi wa habari.
Kwa upande mwingine Mjumbe wa Shirikisho hilo ambaye pia ni Mwanamuziki mkongwe nchini Bw. Kassim Mapili alitoa shukrani zake za dhati kwa waandishi  wa habari kwa kutoa taarifa kwa umma  juu ya afya yake pamoja na jamii kwa ujumla kwa kumsaidia katika kipindi chote alichokuwa akitibiwa ugonjwa wa Moyo katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »