WATU
wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti mkoani Tanga ambapo tukio
la kwanza lilitokea kijiji cha Katurupesa kata ya Kwemkwazu wilayani Lushoto
mkoani hapa kwa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 ambaye
hakufahamika jina wala mahala anapoishi amegundulika amefariki dunia na mwili
wake ukiwa umesogezwa kwenye kalvati la Daraja ikiwa baadhi ya viungo vyake
sehemu ya kichwani sehemu za siri vikiwa vimeondolewa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fresser Kashai alithibitisha kutokea tukio hilo ambapo
alisema limetokea Septemba 26 mwaka huu saa nane mchana eneo ha Katurupesa
Kwemkwazu wilayani Lushoto mkoani Tanga ambapo mwili huo uligunduliwa na baadhi
wa wasamaria wema.
Alisema
baada ya polisi kupata taarifa hizo walifanikiwa kufika eneo la tukio ambapo
waliuchukua mwili na kwenda kuuzikwa na wananchi baada ya uchunguzi wa daktari
kufanyika.
Kamanda
Kashai alisema kuwa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na watuhumiwa
kuhusiana na tukio hilo bado hawajakamatwa wakati juhudi za upelelezi ukiwa
unaendelea ili kuweza kuwabaini wahusika.
Tukio
la pili lilitokea Kijiji cha Kwangahu Kata ya Mkata Tarafa ya Mazingira
wilayani Handeni lilihusisha mwendesha pikipiki Kiduo Rajabu (35) Mzigua akiwa
anaendesha pikipiki yenye namba T.813 CAM aina ya Fekon akiwa amempakia Amiri
Bakari (65) Mzigua mkulima wote wakiwa ni wakazi wa Mkonga wakielekea porini
kuwinda wanyama na kila mmoja akiwa amebeba silaha yake aina ya Gobole.
Alisema
kuwa walipofika kilima cha Lugala pikipiki ilishindwa kupanda mlima huo na
kuanza kurudi nyuma na kuanguka chini ambapo katika tukio hilo silaha aliyokuwa
ameibeba dereva alifyatua na kwa kuwa ilikuwa na baruti gololi na ilimjeruhi
abiria Amiri Bakari ubavu wake wa kushoto na kusababisha kifo chake.
Kamanda
Kashai alisema kuwa mtuhumiwa katika tukio hilo amekamatwa na upelelezi wa
kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea.
EmoticonEmoticon