SAMATTA, KAZIMOTO ULIMWEMGU WATUA DAR KUJIUNGA NA STARS, KIKOSI KUONDOKA DAR IJUMAA, MECHI JUMAPILI BUJUMBURA

September 02, 2014
Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
NYOTA wa Tanzania wanaocheza nje, Mbwana Ally Samatta, Thomas Emmanuel Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto Mwitula wote wamewasili kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi Jumapili wiki hii.
Taifa Stars itacheza na Int’hamba Murugamba mjini Bujumbura Septemba 7 katika mchezo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kikosi cha Stars kinaanza mazoezi leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 
Mbwana Samatta kushoto na Thomas Ulimwengu kulia wakiwa na Mtendaji Mkuu wa BIN ZUBEIRY Blog, Mahmoud Zubeiry. Vijana wamekuja kulitumikia taifa

Mwesigwa amesema kwamba kikosi kitaondoka Ijumaa Dar es Salaam na kurejea Jumatatu baada ya mchezo huo. “Timu itaondoka hapa Septemba 5, Saa 11:10 alfajiri kwa ndege ya Kenya na kurejea  Septemba 8 saa Saa 1:00 usiku,”amesema.
Wakati Samatta na Ulimwengu, wote wanatokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kazimoto anatokea Al Markhiya ya Qatar.
Kikosi kinaanza mazoezi leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kikosi kamili alichoteua kocha Mholanzi, Mart Nooij kwa ajili ya mchezo huo ni makipa; Deogratias Munishi (Yanga) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni Said Morad (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Shomari Kapombe (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam), Joram Mgeveke (Simba) na Charles Edward (Yanga).
Viungo; Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Amri Kiemba (Simba), Himid Mao (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba), Said Juma (Yanga) na Haruna Chanongo (Simba).
Washambuliaji; John Bocco (Azam), Khamis Mcha (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Yanga), Mwegane Yeya (Mbeya City) na Juma Luizio (ZESCO, Zambia).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »