Timu ya Panone FC ya Mkoa Kilimanjaro inayoshiriki ligi
daraja la Kwanza taifa, imeteuliwa kuwa mwenyeji wa timu ya nyota wa zamani wa Real Madrid
inayotarajiwa kuwasili nchini Agost 22 mwaka huu.
Panone FC watakuwa mwenyeji wa timu hiyo kutoka Hispania,
itakapowasili mkoani Kilimanjaro Jumapili ya Agost 24, mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama anatarajiwa
kuwaongoza maelfu ya wadau wa soka mkoani humo, kuwapokea magwiji hao waliowahi
kuichezea Real Madrid miaka ya nyuma wakiongozwa na Zinedine Zidane.
Nyota hao wanatarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro
(KIA) saa 5 asbuhi na kuelekea moja kwa moja katika geti la kupandia mlima Kilimanjaro
(Marangu Gate) kwa ajili ya kutalii na kupata maelezo mafupi kuhusu mlima huo
mrefu kuliko yote Afrika.
Chama Cha soka Mkoa Kilimanjaro (KRFA) kiko katika mchakato
wa kuandaa mechi moja kati ya Bingwa wa mkoa wa Kilimanjaro msimu huu, Panone
Fc na bingwa wa msimu uliopita Machava, ili ishuhudiwe na magwiji hao.
Msemaji wa KRFA, Yusuph Mazimu alisema mchezo huo wa
kirafiki unalenga kuwapa nafasi nyota wao wa Madridi kushuhudia vipaji vya soka
mkoani humo.
“ tunajua wana ratiba ngumu sana, wanapaswa kwenda kulala
Arusha siku hiyo hiyo, kwa hiyo hata ikikubalika, hawatashuhudia mchezo mzima,
labda dakika 10 au 15 ila uwepo wao utaleta hamasa kwa vijana wetu na ligi yetu
ya mkoa”.
Nyota hao wa Madrid kabla ya kuja Kilimanjaro, Agost 24 watakipiga
na nyota wa TSN Tanzania Eleven katika
uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, watakaokuwa chini ya makocha Charles
Boniface Mkwassa, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ na Fred Felix Minziro.
Mratibu wa ziara ya nyota hao wa Real Madrid, Denis Ssebo,
alisema, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo.
EmoticonEmoticon