LIGI DARAJA LA TATU KILIMANJARO KUANZA AGOSTI 23

August 20, 2014
Ligi Daraja la tatu ngazi ya mkoa kwa mkoa wa Kilimanjaro, inatarajiwa kuanza agost 23, mwaka huu.

Ligi hiyo itakayoshirikisha timu 19, itaendeshwa kwa hatua mbili, hatua ya makundi na hatua ya fainali itakayokuwa na timu tano, nne ni zile zilizoongoza kundi na moja ni ile itakayokuwa na matokeo mazuri (best looser). 

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), timu hizo zimegawanywa katika makundi manne, makundi matatu yakiwa na timu tano tano na kundi moja likiwa na timu nne.

Kundi A litakuwa na timu za Afro Boys, Reli, KIA, Soweto na Kilototoni wakati kundi B linaundwa na timu za New generation, Sango, Kilimanjaro Fc, Hai City na Lang’ata.

Timu za Polisi Kilimanjaro , Kilimanjaro Rangers, Kagongo, Magadini na Boda zinaunda kundi C na kundi D litakuwa na timu nne za Forest, Polisi Mwanga, Kitayosce na Machava ambaye ni bingwa wa misimu miwili iliyopita kabla ya kupokwa ubingwa na Panone FC katika msimu uliopita.

Pazia la ligi hiyo linatarajiwa kufunguliwa kwa mechi tatu ambapo timu za Afro boys itakipiga na Reli katika uwanja wa Magereza mjini Moshi, New Generation itakutana na Sango FC katika uwanja wa Memorial uliopo Soweto na Polisi Kilimanjaro itakuwa mwenyeji wa Kilimanjaro Rangers katika dimba la Mandela uliopo Pasua Moshi.

Akizungumzia maandalizi ya ligi hiyo, msemaji wa KRFA, Yusuph Mazimu alisema kila kitu kimekamilika ikiwa ni pamoja na maandalizi ya viwanja na waamuzi.

“tunataka ligi ya msimu huu iwe bora zaidi ya misimu mingine, ndio maana tumejitahidi kuandaa kila kitu mapema ili kutoa nafasi ya watu wa soka kufurahia michuano hii itakayokuwa na hatua mbili, ya awali na baadae hatua ya fainali itkayoshirikisha timu tano, nne zilizoongoaza makundi na moja itakayokuwa na matokea mazuri yaani besti looser”.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »