Dar/Dodoma. Kauli ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad kuhusu haja ya kupokezana nafasi ya urais kati ya Bara na
Visiwani imekuwa ‘ngumu kumeza’ kwa wanasiasa walio wengi.
Baadhi ya wanasiasa wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na
wasomi wengine waliozungumza na waandishi wetu wamepinga kauli hiyo
wakieleza kuwa suala hilo halitawezekana kwa sababu linaweza kusababisha
mgawanyiko mkubwa katika jamii.
Mwanasiasa pekee aliyeonyesha kuiunga mkono kauli hiyo ni Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliyesema jambo hilo linazungumzika kwa sababu
huwezi kuwa na nchi mbili zilizoungana lakini nchi moja pekee ndiyo
inayotoa rais mara zote.
“Miaka ya nyuma utaratibu huu ulikuwapo lakini baada ya Mwalimu Nyerere
kuondoka, CCM wakauondoa. Kitendo cha rais kutoka Tanzania Bara kila
baada ya miaka 10, ndicho chanzo cha Zanzibar kubadili Katiba yao na
kuifanya nchi hiyo kuwa na mamlaka kamili yasiyoweza kuingiliwa na rais
wa Muungano,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema
mfumo wa kubadilishana urais, utaleta mgawanyiko kwa makundi na maeneo
mengine ya nchi kudai kuwa na zamu ya urais.
“Hatuwezi kwenda katika mfumo huo. Utasababisha kugawanyika kwa sababu
ukishasema hivyo watatokea Waunguja nao watadai, Wakaskazini, Waislamu
na Wakristo nao watadai,” alisema.
Alitolea mfano katika uchaguzi uliopita ambao Dk Slaa alipata mgombea mwenza ambaye hatoshi upande wa Zanzibar.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Profesa Abdul Sheriff alisema utaratibu huo
utaleta maana iwapo kuna muundo wa serikali tatu na si wa serikali
mbili.
“Kwa sasa rais anachaguliwa na upande wenye watu wengi ambao ni Bara
kwani wazi atashughulika na mambo ya Serikali ya Tanzania Bara na si ya
Muungano,” alisema.
Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti alisema suala hilo ni zuri na analiunga
mkono iwapo nchi inakwenda katika muundo wa serikali moja. “Kama
tunataka kutekeleza chini ya mundo wa serikali mbili ni lazima
tubadilishe mambo mengi kwanza,” alisema.
Kimiti alisema zamani iliwezekana kwa sababu nchi ilikuwa katika mfumo wa chama kimoja cha siasa.
Mbunge wa Dole (CCM), Sylvester Mabumba alisema rais anatakiwa atokane
na uwezo, sifa, uadilifu, hekima na jinsi alivyo na upendo kwa
wapigakura wake, badala ya eneo anakotoka.
“Kama ni zamu ya upande Tanzania Bara na tumekosa mtu ambaye ana sifa na
uwezo tunafanyaje na tumeshajiwekea utaratibu huo?” alihoji Mabumba.
“Maalim Seif ni mwanasiasa mzoefu na aliyebobea na pia ni msomi katika
eneo la siasa angefanya uchambuzi, vinginevyo atasababisha mgongano
katika jamii,” alisema.
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM –Bara, Pius Msekwa alisema, “Sioni
tatizo lolote kwa sababu uongozi huwa haubadilishwi kama mtu
anavyobadilisha shati. Unajua mkiamua kupeana zamu ni dalili za
kutoaminiana.”
Huku akimtolea mfano Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Msekwa
alisema rais huyo alitokea Zanzibar na alipatikana kwa sababu kwa wakati
huo alionekana anafaa na si kwa sababu alikuwa akitokea upande huo wa
Muungano.
“Jiulizeni kama mnapotaka kubadilisha ili kila upande utoe rais kila
baada ya miaka 10 mnataka kurekebisha jambo gani? Mbona kwa sasa hakuna
tatizo lolote, binafsi naunga mkono utaratibu wa sasa.”
“Ndani ya CCM majina ya wagombea urais hupendekezwa na hatimaye kubaki
jina moja na huo utaratibu hutumika katika vyama vingine, sasa
ukifanyika uchaguzi anayeamua nani awe rais ni Watanzania wenyewe bila
kujali huyu wa huku na huyu wa kule,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustine Mrema alisema:
“Tukipitisha kisheria ya suala hili tutajiletea matatizo makubwa.
Anatakiwa kutizamwa mtu mwenye vigezo kwa wakati huo kama ilivyokuwa kwa
Mwinyi. Jambo hili lisiwe lazima, bali yatazamwe mahitaji ya wakati
husika.”
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura
alisema: “Hakuna sheria inayosema nchi mbili zikiungana lazima rais
atoke kila upande wa muungano kila baada ya miaka fulani. Binafsi sioni
kama jambo hili ni tatizo kwa sababu nchi hizi zinaweza kukubaliana tu
tena kwa mazungumzo ya kawaida kabisa.”
Rwechungura alisema ingawa Zanzibar wanaweza kuhoji kuwa udogo wa nchi
yao ndiyo sababu ya kutokutoa rais wa muungano, lakini hata kama
wakipewa fursa hiyo haiwezi kuwa dawa ya kuondoa kero za muungano
zilizopo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema tatizo
lililopo ni muundo wa muungano na si mzozo wa nani atoe rais na nani
asitoe.
“Lazima mkubaliane muundo wa muungano na mgawanyo wa mamlaka ya serikali
baina ya pande mbili za muungano. Rasimu ya Katiba ya sasa haisemi
lolote juu ya jambo hili na lingeweza kujadiliwa ila kama unavyoona
mchakato wa Katiba nao umeingia dosari,” alisema.
Mwananchi
EmoticonEmoticon