April 09, 2014


NA FATNA MFALINGUNDI,KOROGWE.
 Halmashauri ya wilaya ya Korogwe imetoa kilo 500 za mbegu ya mtama kwa Wananchi wake walioathiriwa na mafuriko na ukame katika msimu huu wa kilimo ili kukabiliana na njaa  kwa kuwa zao hilo linahimili ukame na hivyo kuwahakikishia usalama wa  chakula kwa mwaka huu.
Akikabidhi mbegu hizo juzi katika kijiji cha Mapangoni
kata ya Kerenge kilichoathiriwa na mafuriko, Afisa Kilimo wa wilaya Kakulu Lugembe aliwaambia viongozi na wakulima wa kijiji hicho kuwa halmashauri imetoa mbegu hiyo ili kuwakinga na upungufu wa chakula unaoweza kutokea kutokana  na mahindi yao kusombwa na maji yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa wiki.
Lugembe aliwasihi  wakulima hao kupanda mtama huo kwa kuwa wapo katika msimu wa mvua za masika zinazoelekea kwisha hivyo  hata zikikatika mapema wataweza kuvuna na kupata chakula kwa sababu mtama unastahamili ukame na kuwataka kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuepukana na athari za mvua nyingi hasa kwa wanaolima katika maeneo yenye miinuko ambako ndiyo hasa mahindi mengi yalisombwa na mawe na maji yaliyoporomoka kutoka milimani kutokana na mvua kubwa.
Awali akitoa taarifa ya athari za mvua hiyo, afisa kilimo wa kata ya Kerenge Frank Mbaga alisema kuwa uharibifu wa mahindi uliotokana na mvua hizo unakadiriwa kuwa  tani 15.75 za ekari  25 na wao walitegemea kuvuna tani 492 na hivyo hali hiyo inaweza kusababisha upungufu wa chakula kwa asilimia 3.25 ya kaya 328 za kijiji hicho.
Nao wakulima wa kijiji hicho walieleza jinsi mvua hizo zilivyosababisha athari kubwa kwa baadhi ya familia na kusema kuwa mtama huo unaweza kuwa tegemeo kwao.”Mimi nimelima ekari 3 kati ya hizo 2.5 zimesombwa na maji,nimebakiwa na nusu ekari tu na nina familia”, alisema Yohana Pius Mkulima wa kijiji cha Mapangoni.
Naye afisa pembejeo wa wilaya  Andrew Kambengwa alisema kuwa mbegu hizo zitaganywa pia katika kata za Mashewa,Mkomazi, Mazinde na Magamba kwa Lukonge kwa bei ya ruzuku ya Serikali ya shilingi 3750 kwa mfuko wa mbegu ya kilo 2.5 inayotesheleza ekari moja kwa kuwa kata hizo zimekuwa zikikabiliwa na ukame.


Mwenyekiti wa kijiji cha Mapangoni akiwaonesha Wataalam wa kilimo jinsi mvua ilivyoporosha rundo hilo la mawe kutoka katika mlima unaoonekana pichani hadi mashambani mwao.

Sehemu ya mbegu ya Mtama iliyogawanywa kwa Wanavijiji walioathiriwa na mvua.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »