Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Shirika la Nyumba Mkoa wa Katavi Ndugu Nehemia Msigwa juu ya miradi ya ujenzi wa nyumba itakayofanyika ndani ya mkoa wa Katavi.Pichani ni Michoro ya Nyumba zitakazojengwa mkoani Katavi na Shirika la
Nyumba ya Taifa,ambapo wilaya ya Mlele ,Shirika la Nyumba linajenga
nyumba 60 na zitachukua miezi nane kukamilika.
…………………………………………………………………………….
Shirika
la Nyumba Mkoa wa Katavi/Rukwa umejizatiti katika kutekeleza mpango
Mkakati wa Shirika wa miaka mitano yaani 2010/2011 hadi 2014/2015 kama
ilivyokwa mikoa mingine katika Shirika la Nyumba la
Taifa. Mpango huu umekuja wakati mwafaka kushughulikia tatizo la uhaba
wa nyumba za makazi na biashara kwa Mkoa huu wa Katavi/Rukwa. Katika
Mpango Mkakati huu, Shirika limejiwekea Dira, Dhima, Maadili ya Msingi,
Malengo na Matarajio ya Shirika.
Wakati
Utekelezaji wa Mpango huu unaendelea kwa sasa, unasaidia sana katika
kukuza uchumi kwa katika mkoa wetu kwa njia ya kuongeza Ajira mbalimbali
pamoja na kodi, na hili linatokana na uwezo mkubwa wa sekta ya Nyumba
katika kukuza uchumi katika eneo husika. Zaidi sana ni Msisitizo wetu
NHC-Katavi/Rukwa kuwa, Maendeleo ya Mikoa hii, lazima yaendane na
Ujenzi wa Nyumba Bora za Makazi na za Biashara. Na kwa hili NHC
tunaelekea kukamilisha malengo yetu mawili ya kuwa Kiongozi Mahiri
katika Kuendeleza Milki na Pia kuwa Msimamizi Mahiri wa Miliki si hapa
Katavi tu bali Tanzania Nzima.
Kwa
sasa kuna miradi Mitano ambayo ipo katika hatua mbalimbali ambayo
inatekelezwa na Shirika katikakufikia malengo shirika tuliyojiwekea.
Kuna
Mradi wa Ilembo ambao unatarajiwa kukamilika 30/Mei/2014. Mradi huu una
jumla ya nyumba 90. Ni mradi mkubwa kwa eneo kama la Mpanda ambao
utakuwa name gharama ya said I ya Tsh. 3.1 Bil. kuwepo na umesaidia sana
kutia hamasa kwa wananchi wa Mpanda kuongeza kasi katika sekta ya
ujenzi wa Nyumba, pia umesaidia kuleta mandhari bora ya makazi. Ni
matarajio yetu, kwa kuwa tumeshaanza kuuza nyumba hizo, Taasisi za
Serikali, Mashirika ya Umma, Mashirika Binafsi, Halmashauri za Miji
ambazo katika mkoa wa katavi watumishi wake wengi wanakosa Nyumba bora
za kuishi watazichangamkia Nyumba hizi kwa kuzinunua na kuwapangiza
watumishi wake. Vilevile ni matarajio yetu kuwa Wananchi nao kila mmoja
binasfi watajitokeza kwa wingi kununua Nyumba hizi ambazo ni Bora kwa
makazi.
Katika
Wilaya Mpya ya Mlele, Mradi wa nyumba za Gharama nafuu upo katika hatua
za awali, ni mmatarajio yetu mara baada kukamilika kwa Mradi huo tatizo
la uhaba wa nyumba Bora za Kuishi pale Inyonga, ambapo ndipo makao
makuu ya Wilaya, litakuwa limedhibitiwa kwa kiasi kikubwa, rai yetu ni
ileile kwa taasisi za serikali, Mashirika ya Umma, pamoja na Mashirika
Binasfi zichangamkie fursa hiyo ya kupata nyumba kwa ajili ya Watumishi
wake.
Miradi
kama hii ya Ilembo-Mpanda pamoja na Inyonga tunatarajia pia kuipeleka
katika Wilaya za Kalambo pamoja na Nkasi mkoa wa Rukwa na Halmashauri ya
Nsimbo mkoani Katavi. Miradi katika wilaya hizi itaanza mara tu
taratibu husika zitakapo kamilika. Ninatoa Ari kuwa halmashauri ambazo
zitatoa ushirikiano chanya kwa NHC katika kutatua tatizo hili la uhaba
wa nyumba bora za makazi kwa wafanyakazi wake na wananchi kwa ujumla
ndio itakayofikiriwa zaidi, hii ni pamoja na changamoto za bei kubwa za
Viwanja tunazokumbana nazo kutoka kwa halmashauri husika.
Katika
orodha ya Miradi ambayo ipo katika Mkoa huu ni pamoja na Mradi wa Jengo
la Biashara litajengwa katika eneo la Paradise-Mpanda hapa Mkoani
Katavi na Mradi wa Nyumba za Makazi katika eneo la Jangwani-Sumbawanga
Mkoani Rukwa. Miradi hiyo yote imeshatangazwa kwa ajili ya Kupata
wakandarasi watakao jenga miradi hiyo, hivyo muda si mrefu miradi hiyo
itaanza rasmi.
Katika
hatua nyingine, ili kutatua tatizo la uhaba wa kumbi za mikutano,
Shirika la Nyumba la Taifa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji ya
Mpanda watajenga Ukumbi wa Kisasa wa Mikutano katika eneo la madini
(Madini Plot). Huu ni mradi mwingine katika Mji wa Mpanda ambao si tu
utaleta mandhari nzuri kwa Mkoa wa Katavi bali pia Utafanya Mkoa wa
Katavi kuwa Kitovu cha mikutano muhimu ya Ushirikiano kwa mikoa ya kanda
hii ya ziwa Tanganyika na Nchi jirani, hivyo pia kuchangai ukuaji wa
uchumi katika mkoa huu.
Napenda
pia kuchukua fursa hii kuzishauri Halmashauri za Miji taasisi za
serikali, mashirika ya umma yote yanao jiusisha na utoaji wa huduma za
miundo mbinu (Maji, Umeme pamoja na Barabara) kuwa sisi NHC ni wabia wao
wakubwa kwani tunachangia kwa kiasi kikubwa kuwatafutia wateja wapya
katika kila Mradi husika. Hivyo pindi tunapoanza ama hata kabla ta
kuanza mradi husika huduma zao zinahitajika.
MPANGO WA SHIRIKA LA NYUMBA WA KUSAIDIA VIJANA KWENYE HALMASHAURI ZA WILAYA NA MIJI MASHINE ZA KUFYATULIA MATOFALI
Katika
kuunga mkono jitihada za dhati zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kuongeza ajira za vijana na kupunguza umaskini
hapa nchini na hasa Mikoa ya Katavi na Rukwa, Shirika limeamua kutoa
mashine za kufyatulia matofali kwa Halmashauri zote zilizoko katika
Mikoa hii, zikiwemo Halmashauri za Mlele, Nsimbo, Mpanda Mji pamoja na
Halmashauri ya Mpanda Vijijini kwa Mkoa wa Katavi, Pia Halmashauri
Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi-Namanyere Pamoja
na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo katika Mkoa wa Rukwa.
Mashine
hizo zitatumiwa na vikundi vya vijana vitakavyoundwa na Halmashauri kwa
kushirikiana na Meneja wa Mikoa wa NHC. Kila kikundi cha vijana
kitapewa msaada wa mashine nne (4) ambazo, kila mashine itakuwa
ikihudumia vijana wapatao 10 hivyo vijana 40 katika kila Halmashauri.
Pamoja na msaada wa mashine, Shirika litatoa Shilingi laki tano
(500,000/=) kwa kila kikundi kama kianzio cha vijana hao kununua vifaa
muhimu vya kuwezesha kazi ya kufyatua matofali kuanza. Aidha, vikundi
hivyo vya vijana vitaweza baadae kuunda SACCOS zao na hivyo kupanua
shughuli zao za kiuchumi.
Ili
kufanikisha mpango huo, Shirika kwa kushirikiana na Wakala wa Utafiti
wa Vifaa Bora vya Ujenzi wa Nyumba (NHBRA) iliyo chini ya Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na Mamlaka ya Elimu na
Ufundi Stadi (VETA) litatoa mafunzo ya siku 21 kati ya mwezi Desemba
2013 na Januari 2014 kwa wakufunzi wapatao 50, ya namna ya kutumia
mashine hizo. Wataalam hawa ndio watakaotumika katika kuvifundisha
vikundi vya vijana katika Halmashauri kuanzia mwezi Januari hadi Juni
2014.
Shirika
la Nyumba la Taifa linatanguliza Shukrani kwa kutuunga mkono katika
kufanikisha jambo hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
“KATAVI BILA UMASIKINI INAWEZEKANA, KWA KUWA MAISHA NI NYUMBA”
MAISHA YANGU NYUMBA YANGU
IMETOLEWA NA
NEHEMIA L. MSIGWA
MENEJA WA MKOA
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
EmoticonEmoticon