MORO SISTERS KUANZA KUJIFUA JANUARI 20.

January 16, 2014
Na Daudi Julian,Morogoro.
TIMU mpya ya soka ya wanawake ya Moro Sisters inatarajia kuanza mazoezi Januari 20, mwaka huu, katika uwanja wa Shujaa uliopo mjini Morogoro.

Akizungumza na Mtandao huu, kocha wa timu hiyo, Charles Sendwa ‘kocha mtaalamu’ alisema maandalizi kwa ajili ya kuanza mazoezi hayo yanakwenda vizuri na kwamba yatakuwa yakianza saa 9.00 alasiri ili saa 10 jioni kuipisha timu ya Burkina Faso inayotumia pia uwanja huo kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza.

Sendwa alisema timu hiyo ina zaidi ya wachezaji 15 wenye umri chini ya miaka 20 na lengo lake ni kuipa mafanikio zaidi katika soka la wanawake.

Kocha huyo alisema mara baada ya kufanya mazoezi kwa siku kadhaa, Moro Sisters itaanza kucheza michezo mbalimbali ya kirafiki ndani na nje ya mkoa huu.

Alisema anaamini timu hiyo itafanya vizuri na kupata mafanikio makubwa katika mchezo huo kwa kuwa inaundwa na wachezaji chipukizi.

“Nimejipanga vizuri kuifikisha timu katika kilele cha mafanikio kikubwa naomba wadau wa soka watuunge mkono”, alisema.
 
Katika hatua nyingine, kocha huyo ametoa wito kwa wadau wa michezo nchini kuisaidia timu hiyo vifaa vya mchezo wa soka kama vile jezi, mipira, soksi, viatu, koni na bips ili iweze kufanya vizuri.
 
“Tunaanza mazoezi lakini vifaa bado tatizo hivyo tunawaomba wadau wa michezo likiwemo Shirikisho la Soka Nchini (TFF) watusaidie vifaa hivyo”, alisema.
 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »