WATAKA KAMATI IWATAJE WABUNGE WANAOHUSIKA NA UJANGILI:IMEWEKWA DESEMBA 31.
Wananchi mbalimbali wakiwamo wasomi na
wabunge, wamelitaka Bunge kuweka wazi majina ya wabunge waliotajwa
kuhusika na vitendo vya ujangili wa wanyamapori. (HM)
Wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati
ndogo ya Uchunguzi ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu
Operesheni Tokomeza Ujangili, Mwenyekiti wake, James Lembeli alisema
baadhi ya wabunge walitajwa kujihusisha na ujangili.
Akizungumza jana, Wakili wa siku
nyingi nchini, Peter Shayo alisema ili Serikali na Bunge waonekane wako
makini na wanachukizwa na vitendo vya ujangili ni lazima wawataje
hadharani wabunge hao.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa alisema jana kuwa hakuona mantiki ya kamati hiyo
kutowataja wabunge hao.
Mwanasayansi bingwa mtafiti, Profesa
Watoky Nkya alisema: "Kamati imetumia fedha nyingi za kodi za wananchi
wakijua hakuna aliye juu ya sheria. Tulitarajia kuwafahamu wote
waliohusika na ujangili."
Diwani wa Kata ya Shighati, Enea Mrutu
alisema haiwezekani wabunge wawang'oe mawaziri wanne lakini miongoni
mwao wapo wanaotuhumiwa kwa ujangili na kuachwa bila kutajwa.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
alisema: "Kazi yetu wabunge ni kuisimamia Serikali, kwa hiyo wale
wabunge waliotajwa watajwe ili nao wawajibike ili Bunge letu liwe na nia
thabiti ya kuisimamia Serikali," alisema Mbatia.
Akizungumzia madai hayo, Lembeli
alisema majina ya wabunge hao yapo kwenye viambatanisho vya ripoti yake
kwa Bunge. Chanzo: mwananchi
EmoticonEmoticon