Kocha mpya wa Azam FC. Joseph Marius Omog (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.
KLABU ya Azam inapenda kuufahamisha umma hususan
wapenzi wa mpira wa miguu kuwa imeingia mkataba na kocha Joseph Marius Omog
raia wa Cameroon kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia leo.
Kocha Omog ni bingwa kwani anakuja kuifundisha Azam
akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville)
kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013).
Timu hii ilikuwa haijatwaa ubingwa wa ligi kwa zaidi
ya miaka 30. Kwa mwaka huu wametwaa ubingwa wakiwaacha wapinzani wao, Diables
Noirs kwa pengo la pointi kumi (10) wakikusanya pointi 87 katika ligi yenye
timu 18.
Pia ni mwaka jana tu (2012) aliiwezesha A.C Leopards
kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu
na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria
na Sfaxien ya Tunisia.
Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika
yalifikiwa baada ya miaka 38 tangu klabu ya Jamhuri yas Kongo ifanye hivyo, na
kumfanya kocha Omog kuwa moja ya makocha wa kupigiwa mfano barani Afrika.
Kadhalika mwaka huu 2013, A.C Leopards chini ya
ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na
kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri
(bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Yote hayo ameyafanya akitumia asilimia kubwa ya
wachezaji wa ndani ya Kongo huku akiwainua kutoka katika hali ya kuonekana
wachezaji wa wastani hadi kuwa tishio na kuhofiwa kote barani Afrika.
Azam Football Club inamuona kocha Omog kuwa anakidhi
vigezo vya kuendana na dira ya klabu ambayo ni kukuza na kuwaendeleza wachezaji
na kushindana kwa kiwango cha juu kwa lengo la kuwa mabingwa katika mashindano
mabalimbali ambayo timu inashiriki.
Uongozi wa Azam FC utampatia ushirikiano wa kutosha
ili kufanikisha malengo na mipango thabiti ya klabu.
Maelezo Binafsi
Kocha Omog ni mchezaji wa zamani wa timu ya Dragon
Yaounde Cameroon. Alipata mafunzo ya ualimu wa michezo na elimu ya viungo
(Sports and physical education) kutoka chuo cha vijana na michezo (Higher
Institute of Youth and Sports, INJS Yaounde).
Baadaye alipata fursa ya kujiendeleza nchini
Ujerumani ambako mwaka 1987 alitunukiwa stashahada ya ukufunzi wa mpira wa
miguu na leseni B ya ukocha kwa viwango vya Shirikisho la mpira wa miguu barani
Ulaya, UEFA.
Aliporejea nyumbani kwao Cameroon Joseph Marius
Omog, alifundisha kabumbu katika klabu mbalimbali, zikiwemo; Fovu of Baham na
Aigle of Menoua na kufanikiwa kufuzu kwa fainali za kombe la Cameroon. Mwaka
2001 aliteuliwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions
chini ya kocha raia wa Ujerumani Winfried Schafer.
Omog amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya
Cameroon iliyoundwa na wachezaji wa ndani ijulikanayo kama Intermediate Lions
hadi mwaka 2010 na baada ya hapo akelekea Kongo kuionoa A.C Leopards kwa
mafanikio makubwa na hasa kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho wakiifunga
Djoliba ya Mali kwa ushindi wa jumla wa magoli 4-3 katika michezo miwili ya
fainali.
EmoticonEmoticon