Meneja Mkuu wa MSALABS , Albert Kamwela na Afisa Mahusiano wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Mary Lupamba wakigawa mitungi ya gesi ya kupikia kwa watu wenye ulemavu katika kata ya Nyang’hwale
Mmoja wa wanufaika akiendesha baiskeli aliyokabidhiwa na Kampuni ya MSALABS kwa kushirikiana na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwainua wananchi wenye mahitaji maalum.

Wafanyakazi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na MSALABS wakifurahi katika picha ya pamoja na watu wenye ulemavu
Afisa wa Kampuni ya MSALABS akikabidhi Baiskeli kwa mama mlemavu katika hafla hiyo , huku mnufaika akiwa mwenye furaha na matumaini
Kampuni ya MSALABS inayotoa huduma ya maabara ya kupima madini katika mgodi wa Barrick Bulyanhulu uliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga imeshirikiana na mgodi huo kukabidhi misaada mbalimbali kwa wananchi wanaoishi kwenye mazingira magumu kwenye kata ya Mwingiro , Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Hafla ya kukabidhi msaada huo imefanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Nyamikonze kilichopo wilayani Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi, wakazi wa eneo hilo pamoja na baadhi ya wafanyakazi kutoka Barrick Bulyanhulu na MSALABS.
Meneja wa Kampuni ya MSALABS,Albert Kamwela, amesema lengo la kutoa msada huo ni kuboresha maisha ya wananchi wenye maisha ya kawaida na walemavu kwa kuwapatia nyenzo za usafiri na majiko ya kupikia ya gesi kwa ajili ya kuhamasisha watumie nishati safi ya kupikia.
Kamwela ameitaja misaada iliyotolewa kuwa ni vyerehani (2) , Baiskeli za walewavu (2), Baiskeli za kawaida (10), Mitungi ya gesi ya kupikia (32).
Afisa Mahusiano wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Mary Lupamba akiongea katika hafla hiyo amesema Barrick inatambua na kuthamini umuhimu wa ushirikiano na watu wenye ulemavu na itaendelea kuhamasisha wakandarasi wake kutekeleza sera na kanuni za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kuwakumbuka wananchi wenye changamoto za ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwingiro, Gasper Kashepa, aliishukuru kampuni ya Msalabs na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kuendelea kushirikiana na jamii zinazozunguka mgodi huo kwa kutoa misaada yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa eneo hilo.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, Lucy Mayunga akiongea kwa niaba ya wanufaika amesema msaada huo utachangia kuinua ustawi wa kaya nyingi na kusaidia makundi yenye mahitaji maalum kupata fursa bora za maendeleo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya kila siku.

EmoticonEmoticon