| WASHIRIKI WA WARSHA HIYO WAKIIFUATILIA |
| WASHIRIKI WAKIWA MAINI KUFUATILIA MIJADALA KWENYE WARSHA HIYO. |
Na Oscar Assenga,Tanga.
WATENDAJI wa Serikali wametakiwa kuwa na huruma kwa wazee hasa katika utoaji huduma mbalimbali ikiwemo za matibabu,malazi na mahitaji yao muhimu kwani wengi wao hushindwa kupewa kipaumbele wanapohitaji huduma hizo kutokana aina ya maisha waliyonayo kwenye jamii zinazowazunguka.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na washiriki kwenye warsha ya siku mbili iliyokuwa ikihusu huduma za wazee kwenye maeneo ya watendaji zinapewa kipaumbele iliyoratibiwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Old Nguvumali Women Centre (Ongwece) yenye makazi yake nguvumali jijini Tanga ambapo ilihusisha watendaji wa kata kutoka halmashauri ya jiji la Tanga na wakuu wa idara.
Akizungumza katika warsha hiyo,Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabokweni,Hamza Omari alisema serikali haina budi kuhakikisha inawasaidia wazee wa aina zote hapa nchini kwa kutenga bajeti maalumu ambayo itawahudumia kwenye mahitaji yao muhimu kutokana na wazee wengine kutopata msaada kwenye jamii zao.
Masoud alisema wazee wengi hawana utambulisho wa matibabu na kusema endapo watafanikiwa kuwekewa utaratibu wa kuwa na vitambulisho itasaidia kuondokana na adha ambazo wamekuwa wakikutana nazo mara kwa mara wanapokuwa wakihitaji huduma hiyo muhimu
Aidha aliongeza kuwa wakati umefika kwa jamii kubadilika na kuwathamini wazee ikiwemo kuacha kusema wazee wamepitwa wakati kwani hata nao watakuja kuwa miongoni mwao siku zijazo na huenda wakakutana na hali kama hizo endapo watashindwa kuwajali na kuwaheshimu wakati huu.
Naye Hanafi Masoud ambaye ni Ofisa Mtendaji kata ya Chumbageni alisema tatizo kubwa lililopo kwenye jamii nyingi hapa nchini ni kupotoka kimaadili na kushindwa kuwaheshimu na kuwapa kipaumbele wazee kama ilivyokuwa hapo zamani.
Aidha aliiomba asasi zisizo za kiserikali ziendelee kuhamasisha jamii ili kuweza kuona umuhimu wa wazee kutokana na wengi wao kuwa na mchango mkubwa sana lakini pia akiitaka serikali kuhakikisha inawahudumia wazee wasiojiweza kwa asilimia mia moja.
Kwa upande wake,Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Jiji la Tanga,Kassim Sengasu alishauri jamii kuangalia mfumo gani ambayo unaweza kutumika kuwaangalie wazee baada ya kustaafu kwa kushirikiana na taasisi za kidini kwani zikiwekwa pembeni hao wazee watakuwa kwenye hali ngumu sana.
Hata hivyo,Mwezeshaji wa Warsha hiyo,Lucas Munako alisema dhana ya uzee ipo rasmi kwenye mfumo wa serikali na imejikita katika umri kwa mujibu wa miongozo iliyopo kuanzia miaka sitini na kutaka wazee wangewekewa utaratibu mzuri wa kuwawezesha ili kuweza kujikimu katika maisha yao.
Awali akizungumza ,Mratibu wa Asasi hiyo,Devina Kibaja alisema lengo la warsha hiyo kwa watendaji hao ni kuweza kuwapa uelewa wa juu ya umuhimu wa wazee katika maeneo yao ya kiutendaji wanayoyaongoza katika sehemu zao wanazotoka.
Mwisho.
EmoticonEmoticon