RATIBA RCL KUPANGWA J’NNE, LIGI KUANZA MEI 12
Upangaji
ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi
(Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi
hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi
huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya
ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao
kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati
ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari
ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi
ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja
kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa
wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo
draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari
imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao
wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam
2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar
es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo
FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine
ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe
(Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1),
Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero
ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada
ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni
uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa
ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya
wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa
iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi,
Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
TAIFA STARS KUANZA COSAFA JULAI 6
Taifa
Stars imepangwa kundi A la michuano ya Kombe la COSAFA ambapo itacheza
mechi yake ya kwanza Julai 6 mwaka huu jijini Lusaka, Zambia dhidi ya
Shelisheli.
Upangaji
ratiba (draw) wa mashindano hayo ulifanyika juzi (Mei 3 mwaka huu)
jijini Lusaka ambapo timu nyingine zilizo na Taifa Stars katika kundi
hilo ni Namibia na Mauritius. Kundi la Taifa Stars litachezea mechi zake
jijini Lusaka.
Mechi
ya pili ya Taifa Stars katika hatua ya makundi itakuwa Julai 8 mwaka
huu dhidi ya Mauritius. Mechi ya mwisho katika hatua hiyo itakuwa Julai
10 mwaka huu dhidi ya Namibia.
Kundi
B lina timu za Kenya (Harambee Stars), Botswana (Zebras), Lesotho na
Swaziland. Hatua itakayofuata baada ya hapo ni ya mtoano (knockout) na
kila kundi litatoa timu moja tu.
Iwapo
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itafuzu kwa
hatua itakayofuata itacheza Julai 13 mwaka huu na Afrika Kusini (Bafana
Bafana) ambayo pamoja na timu nyingine tano zimekwenda moja kwa moja
katika hatua ya mtoano.
Nyingine
zilizokwenda moja kwa moja hatua ya mtoano ni wenyeji Zambia, Angola,
Zimbabwe, Msumbiji na Malawi ambazo kwenye viwango vya ubora vya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ziko juu ya zile
zilizoanzia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA itafanyika Julai 20 mwaka huu.
AZAM FC KUREJEA NYUMBANI KESHO
Timu
ya Azam inatarajiwa kurejea nchini kesho (Mei 6 mwaka huu) saa 7 mchana
kwa ndege ya Emirates kutoka Morocco ambapo jana (Mei 5 mwaka huu)
ilicheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat
ya huko.
Azam
ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1, hivyo kutolewa katika raundi ya
pili ya mashindano hayo. Mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es
Salaam timu hizo zilitoka suluhu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
EmoticonEmoticon