Halmashauri tisa Tanga zakabidhiziwa Pikipiki na Shirika la Misaada la (JICA)toka nchini Japani

April 22, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.

JUMLA ya Pikipiki tisa aina ya Honda 250CC zenye thamani ya sh.milioni 90 zimekabidhiwa kwa halmashauri tisa zilizopo mkoani hapa kwa matumizi ya maafisa wanaoshughulika na ukaguzi,ufuatiliaji wa tathimini ya shughuli za kilimo zinazofanywa na maafisa ugani wa vijiji katika kutekeleza miradi ya ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa kwa wakati(DADP).

Pikipiki hizo zilikabidhiwa zikiwa na kofia ngumu pamoja na visanduku vilivyo na  vifaa vya matengenezo ya dhahura na tayari kwa ajili ya matumizi ya shughuli zilizokusudiwa.

Akikabidhi pikipiki hizo kwa mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego kwa niaba ya wakuu wa wilaya nyengine zilizopo mkoani hapa,Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa aliwataka kuhakikisha pikipiki hizi zinatumika kwenye matumizi yaliyokusudiwa na sio vyenginevyo ili kuweza kuleta tija zaidi katika kilimo.

Gallawa alisema maafisa hao wapaswa kusimamiwa kikamilifu ili kuweza kufanya kazi zao ipasavyo kwa utaratibu uliowekwa na kwa ajili ya kuwahudumia wananchi waliopo katika vijiji vyao

Mkuu huyo wa mkoa alisema lazima wahakikishe pikipiki hizo zinatumika kwenye matumizi yalikusudiwa na sio vyinginevyo ili ziweza kuleta matunda wakati wakifanya shughuli zao pamoja na kupata takwimu nzuri wakati wakiwa kwenye utafiti wao.

Awali akisoma taarifa ya makabidhiano ya pikipiki hizo, Msaidizi wa katibu tawala wa Mkoa wa Tanga, Hassani Kalombo alisema pikipiki hizo zilitolewa na nchini ya Japani kupitia shirika lao la Misaada liitwalo Japan International Cooperation Agency (JICA) ambapo halmashauri tisa zilizopo mkoani hapa ambazo ni Tanga Jiji, Korogwe Mji, Korogwe Halmashauri, Pangani, Mkinga, Muheza, Lushoto, Kilindi na Handeni zilipatiwa pikipiki hizo.

Alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya kilimo,chakula na ushirika imekuwa ikiendelea na jitihada za kuboresha mipango na utekelezaji wa programu ya uendelezaji wa sekta ya kilimo(ASDP) ikiwa ni pamoja na kuhuisha mfumo wa ufuatiliaji na tathimini.

Akipokea pikipiki hizo, Mkuu wa wilaya ya Tanga, Halima Dendego alihaidi kuwa pikipiki hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa na kueleza lengo kubwa kushirikiana kila idara kwenye wilaya zao ili kuweza kufanikisha malengo yao na kuhaidi kuyafanyia kazi maelekezo hayo.
Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »