RAIS SAMIA AIMARISHA DEMOKRASIA NCHINI KWA KURUHUSU MAANDAMANO,ATAJWA KUWA MAMA WA DEMOKRASIA TANZANIA

January 24, 2024

 


#Viongozi wa CHADEMA wampongeza Rais kwa kufungua ukurasa mpya nchini kupitia falsafa yake ya R4

# Atajwa kuwa ni “Mama wa Demokrasia” wa Tanzania

Januari 24, 2024

Na Waandishi Wetu -Dar es Salaam

Kitendo cha Polisi kuruhusu maandamano ya CHADEMA leo ni ishara ya utekelezaji wa falsafa ya R4 ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeimarisha demokrasia na umoja nchini.

CHADEMA kimepanga kufanya maandamano hayo jijini Dar es Salaam kudai marekebisho ya sheria za uchaguzi na Katiba Mpya.

Kabla ya Rais Samia kuingia madarakani mwezi Machi 2021, maandamano ya upinzani na mikutano ya hadhara ilipigwa marufuku na Polisi nchini.

Lakini katika hali ambayo watu wengine hawakuitarajia, Polisi wametoa ruhusa kwa CHADEMA kufanya maandamano yao ya leo kwa amani na kuwaahidi ushirikiano.

Hata hivyo, Polisi wamewapa viongozi wa CHADEMA masharti manne ili kuhakikisha kuwa maandamano hayo yanafanyika salama.

Masharti hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa waandamanaji hawaleti uvunjifu wa amani au kusababisha mali za watu kuibiwa na kuharibiwa.

Viongozi na mashabiki wa chama hicho cha upinzani pia wameonywa na Polisi kuwa wasitumie lugha za uchochezi na kejeli ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa amani au makosa ya jinai.

Pia waandamanaji wameambiwa wafuate njia zilizokubaliwa na muda uliopangwa ili kuepusha kusababisha foleni na tafrani barabarani.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, amempongeza Rais Samia wa uongozi wake wa maridhiano kwa kuruhusu maandamano.

“Big up kwa ⁦Polisi, tunawaahidi amani mwanzo mwisho. Big up sana pia kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hili,” amesema Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Sugu ameongeza kuwa Rais Samia ameonesha kuwa hana hulka ya kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuminya demokrasia.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amewapongeza Polisi chini ya Rais Samia kwa ushirikiano wao kwa chama chake.

“Nalipongeza Jeshi la Polisi kwa busara hii. Karibuni Watanzania wote, tuandamane kwa amani,” Mbowe amesema.

Falsafa ya R4 (Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding of the Nation) ya Rais Samia imebadili upepo wa siasa nchini.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Serikali ya Rais Samia kuruhusu maandamano ya upinzani.

Mwezi Mei mwaka jana, Polisi jijini Dar es Salaam waliruhusu maandamano ya Umoja wa Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kwenda Ofisi za Bunge na kuwapatia ulinzi.

Rais Samia ameimarisha demokrasia kwa kuruhusu maandamano, kuruhusu vyama vya upinzani vifanye mikutano ya hadhara nchi nzima na ameimarisha usalama na kufanya wanasiasa wa upinzani waliokimbia nchi kurejea nchini.

Samia pia ameongeza uhuru wa wananchi wa kuongea, uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Wananchi kadhaa wakitoa maoni yao kupitia kwenye mitandao ya kijamii wamemtaja Rais Samia kama “Mama wa Demokrasia” wa Tanzania kwa uongozi wake wa maridhiano

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »