REA YAPAMBA MAONESHO YA KITAIFA YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

September 21, 2025 Add Comment


*📌Yaendelea kusambaza majiko ya gesi na  majiko banifu kwa bei ya ruzuku*


*📌Wananchi waaswa kutembelea banda la REA kupewa elimu ya miradi ya umeme kwenye vitongoji na nishati safi*


*📌Geita waipongeza REA kwa utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia*


📍Geita


Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imekuwa kivutio pekee kwa taasisi za Serikali zinazoshiriki katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita. 

Ushiriki wa REA katika maonesho hayo umevutia wananchi wengi kutembelea banda la Wakala ambapo wataalam kutoka REA wanaendelea kutoa elimu ya miradi mbalimbali ya REA inayotekelezwa hapa nchini kwa mafanikio pamoja kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kusambaza na kuuza majiko banifu kwa bei ya ruzuku na majiko ya gesi.



Masaki Health Expo yaelimisha wananchi kuhusu mitindo bora ya maisha

September 21, 2025 Add Comment

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Wananchi wamejitokeza kwa wingi katika Maonesho ya pili ya Afya ya Masaki (Masaki Health Expo) yaliyofanyika leo Septemba 21, 2025 katika mtaa wa Twiga 06, Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya taasisi na watoa huduma 20 wameshiriki kwa kutoa elimu na huduma mbalimbali za afya bure.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Masaki Wellspring Hub (MWH) yamehusisha huduma za lishe, tiba ya viungo (physiotherapy), afya ya akili, afya ya uzazi pamoja na afya ya kinywa na macho.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MWH, Dkt. Yonazi Charles, amesema lengo la maonesho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu mitindo bora ya maisha na kutoa huduma muhimu kwa kushirikiana na wadau wa afya.

“Muitikio umekuwa mkubwa. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali, na tunahimiza kila mmoja kutumia fursa ya maonesho haya ambayo ni bure kushiriki,” amesema Dkt. Charles.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Kliniki za Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) katika Halmashauri ya Kinondoni, Dkt. Omary Mwangaza, amewataka wananchi kutumia maarifa waliyopata kubadili mitindo ya maisha ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

“Magonjwa mengi yanachangiwa na mitindo ya maisha. Kila mmoja anatakiwa kuchukua hatua mapema kujali afya yake,” amesema na kuipongeza MWH kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza afya za wananchi kupitia elimu na huduma za bure.

Miongoni mwa watoa huduma walioshiriki, ONA Eye Care ilitoa huduma za uchunguzi wa macho, ambapo mwakilishi wake, Bi. Neema Elly, amewaonya wazazi kuhusu madhara ya watoto kutumia muda mwingi kwenye simu, televisheni na tablet.

“Matumizi ya vifaa hivyo muda mrefu husababisha changamoto kubwa za macho, hivyo ni vyema wazazi wakawa makini,” amesema.

Aidha, Maple Bloom School kupitia Mkurugenzi wake, Bi. Matilda Sizya, imeshiriki kwa kutoa elimu ya lishe bora kwa watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 18, huku akibainisha changamoto kubwa ipo kwenye uelewa wa malezi na makuzi.

Wananchi waliohudhuria wameipongeza Shirika la MWH na wadau wake kwa kuandaa maonesho hayo waliyoyataja kuwa msaada mkubwa kwa jamii, kutokana na kupata huduma bora na ushauri kutoka kwa wataalamu bila malipo.

KATIBU MKUU MRAMBA AKUTANA NA KAMPUNI YA NYUKLIA YA CHINA

September 21, 2025 Add Comment


📌 *Wajadili ushirikiano katika kuzalisha umeme wa nyuklia nchini*


📌 *Watanzania kujengewa uwezo  katika masuala ya nyuklia*


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba ameongoza ujumbe wa Serikali ya  Tanzania katika kikao na Shirika la Taifa la Nyuklia la China (China National Nuclear Corporation – CNNC), kujadili fursa za ushirikiano  katika kuanzisha na kuendeleza mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia ya nyuklia.


Katika kikao kilichofanyika jijini Vienna, Austria pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 69 Wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomi (IAEA), Wawakilishi wa CNNC waliieleza Tanzania kuwa kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika kujenga na kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa nyuklia, na wako tayari kushirikiana na Tanzania katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya aina hiyo.

“Tanzania imeanza maandalizi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nyuklia ikiwa ni utekelezaji wa dhamira na nia njema ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuona nchi inakuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati, hivyo tupo tayari kushirikiana na CNNC katika safari hii ya kuzalisha umeme wa nyuklia." Amesema Mramba


Ametoa shukrani kwa CNNC kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania, akibainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme wa nyuklia kama sehemu ya mkakati wa kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu na ya uhakika.

 Katika kikao hicho, CNNC  imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania kupitia mafunzo ya kiufundi, ziara za mafunzo, pamoja na kutoa ufadhili kwa masomo ya uzamili katika fani ya nyuklia. Hatua inayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa kutosha kusimamia na kuendeleza miradi ya nishati ya nyuklia nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Bw. Jing Zhang, Mkuu wa Idara ya Ufundi wa IAEA, Mha. Joseph Kirangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Maji na Madini kutoka Zanzibar, Prof. Najat Mohamed,  Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Nguvu za Atomi Tanzania (TAEC), Mha Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu na Wataalam wa masuala ya Nyuklia.



RAIS DKT.SAMIA ANATAMBUA MCHANGO WA MADHEHEBU YA DINI KATIKA KUENDELEZA MAARIFA-MAJALIWA

September 21, 2025 Add Comment


*_Asema elimu haiwezi kukamilika kama hakuna maadili._*

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwa dhati mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo BAKWATA na wadau wote wa elimu katika kuimarisha maadili, kuendeleza maarifa na kuleta mshikamano wa kitaifa kupitia elimu. 

 

Amesema kuwa elimu haiwezi kukamilika kama hakuna maadili kwani ndiyo yanayojenga utu, heshima na mshikamano wa kijamii. "Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu inakuza maarifa na ujuzi, sambamba na malezi yanayoimarisha tabia bora na maadili ya kizalendo kwa vijana wa Kitanzania".

 


Amesema hayo Jumamosi Septemba 20, 2025 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia katika hafla ya usiku ya utoaji tuzo za elimu za mufti iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Serena hotel jijini Dar es Salaam.

 

"Rais Dkt. Samia anawapongeza sana BAKWATA kwa juhudi kubwa mnazozifanya katika masuala yote ya maendeleo ya jamii hususan mchango wenu katika kuendeleza elimu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia malezi ya maadili na maarifa, Serikali inathamini sana mchango wa taasisi za dini kama BAKWATA katika kuunga mkono malezi ya watoto na vijana". Amesema Mheshimiwa Majaliwa.

 


Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya elimu nchini kwani limeanzisha na kuendesha shule, madrasa na vyuo vinavyotoa elimu bora ya dini na ya kawaida, sambamba na kujenga maadili mema kwa vijana.

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tuzo za Elimu za Mufti ni jukwaa la kitaifa la kutambua na kuthamini michango ya kipekee katika elimu, ubunifu, malezi na maadili ya vijana wa Kitanzania. "Tukio hili linaakisi muonekano wa taifa lenye watu wanaojituma, wanaothamini elimu, na wanaochangia ustawi wa taifa letu bila kujali itikadi za dini au misimamo ya kisiasa."

 


Amesema kuwa tuzo hizo zinatambua ubunifu, uongozi, mshikamano wa jamii na mchango wa wadau katika kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi, bora na endelevu. Hili ni tukio linaloonesha kwa vitendo methali ya Mtume (S.A.W) isemayo: “tafuteni elimu hata kama ni mpaka China”; ikiashiria kuwa elimu ni chombo cha ukombozi na maendeleo ya jamii yoyote na hakuna mipaka katika kuitafuta."

 

Amesema Serikali kwa upande wake kupitia Dira ya Maendeleo ya 2050 imeweka malengo ya muda mrefu kuhakikisha kwamba itaendeleza ushirikiano kati ya taasisi za dini, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha elimu inaendelea kuwa injini ya maendeleo ya taifa.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa sekta binafsi, mashirika ya kidini, mashirika ya maendeleo na jamii kwa ujumla kuwekeza zaidi katika elimu. "lengo ni kuhakikisha kuwa tunawajenga vijana wetu wawe wabunifu, waadilifu na wazalishaji wa fursa za ajira badala ya watafuta ajira pekee, ongezeni uwekezaji katika elimu".

 

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, amesema kuwa tuzo hizo zimetolewa kutokana na bakwata kuthamini elimu kwa kuwa uislam ni elimu sio ujinga "Elimu ndio uhai wa uislam na ni nguzo kuu ya uslam, uislam unamchango mkubwa sana duniani katika elimu"


Kadhalika, Sheikh Dkt. Abubakar amempongeza Rais Dkt. Samia kwa usimamizi wake mzuri kwa namna anavyosimamia elimu nchini. Pamoja na hii pia tunathamini sana wadau mbalimbali wanaojitoa katika kusimamia sekta ya elimu na kutilia mkazo masuala ya elimu"

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa elimu wa Bakwata Ally Abdalah Ally amesema kuwa mpango wa tuzo hizo zilizobuniwa na Mheshimiwa Mufti zinalengo la kuinua na kuwatia moyo wadau wa elimu wanaojitoa na kujitolea ipasavyo katika mabadiliko chanya ya elimu kwa maendeleo endelevu. Katika hafla hiyo, tuzo ishirini na tatu zilitolewa.

DKT.BITEKO KUFANYA MAKUBWA KATA YA BUGELENGA

September 20, 2025 Add Comment


📌 Asema  watakaounganishiwa umeme kupewa majiko


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu. Doto Mashaka Biteko amewapongeza wananchi wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe kwa kushirikiana na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata yao ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na miradi ya maji.

Ametaja moja ya mradi kuwa ni ujenzi barabara ya Bufanka - Ikalanga hadi Bukombe ambapo ameahidi kuwa CCM ikipewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, itatekeleza miradi zaidi ili kuwaletea maendeleo wananchi kwa kukabiliana na kero zinazowakabili.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 20, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Bugelenga wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.


Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji sita vya Kata ya Bugelenga na kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika vitongoji tisa vya Kata hiyo.

Amewaeleza wananchi kuwa CCM itaendelea kusogeza huduma bora za jamii ambapo ameahidi kuwa kuanzia sasa wananchi wakiunganisha umeme watapewa majiko ya umeme bure ikiwa ni njia ya kupunguza gharama ya kupikia ikilinganishwa na matumizi ya kuni.


Dkt. Biteko pia amesema watajenga kituo kikubwa cha kupooza umeme ili kuweza kusambaza umeme huo hadi Mbogwe, watajenga madarasa, maabara na jengo la utawala.


“ Mgombea udiwani ameeleza kuhusu shule zinazohitaji ukarabati hivyo ni lazima zikarabatiwe katika kipindi kinachokuja. Pia, 

Nataka niwaambie tutajenga wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa katika Kata hii,” amesema Dkt. Biteko.


Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM imedhamiria kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuongeza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji. 

Kuhusu umuhimu wa elimu, amewaasa wananchi hao kuwasomesha watoto wao kwa kuwa Serikali imeendelea kulipa ada kwa wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita.


Vilevile, amehimiza wananchi wa Bugelenga kumchagua mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa katika kipindi cha uongozi wake amekuwa na mapenzi na wananchi hao kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Bugelenga, Donald Rubigisa amewashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa kushirikiana naye katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga shule.


Amemshukuru Dkt. Biteko kwa kusaidia kujenga daraja kubwa lililoondoa adha ya usafiri kwa wananchi hususan wakati wa masika.


“ Nawashukuru kwa imani yenu kwangu nataka niwaambia mimi nitafanya kazi, mkinichagua mimi, Dkt. Biteko na Dkt. Samia Suluhu Hassan tutatekeleza miradi mipya ya maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.


Aidha, amesema Kata yake ina shule zinazohitaji ukarabati ikiwemo Shule za Msingi Bufanka, Bugelenga na Msasani hivyo amemuomba Dkt. Biteko mara atakapo chaguliwa tena kuwa mbunge asaidie kuboresha shule hizo.


Pia, amesema Kata hiyo inahitaji chumba cha kuhifadhia maiti na kukosa mawasiliano ya simu ya uhakika.


Mgombea huyo amewahimiza wananchi wake Oktoba 29 kujitokeza kwa wingi na kuwachagua wagombea wa CCM.


Mwisho.