TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAENDESHA MAFUNZO YA HAKI ZA BINADAMU NA WAJIBU WA ASKARI WAKATI WA UCHAGUZI MKUU

September 19, 2025 Add Comment



Tume ya Haki za Binadamu imeendesha mafunzo ya haki ya binadamu na wajibu wa Askari Polisi wakati wa uchaguzi kwa askari Polisi ngazi ya kata wilaya ya Tanga. 

Mafunzo hayo  yamefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa jiji la Tanga leo Septemba19, 2025 ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha  askari hao  kuhusu umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na misingi ya haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan kuelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Utafiti na Nyaraka wa Tume ya Haki za Binadamu, Bi Monica Mnanka, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu,.

Amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha  Askari Polisi umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki za binadamu ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

Nao baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga waliopata nafasi ya kuhudhuria mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo  yatakuwa msaada mkubwa kwao katika kutoa elimu kwa wananchi kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi.




Tume ya Haki za Binadamu inaendelea na zoezi la kutoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali, yakiwemo Jeshi la Polisi,pamoja na waandishi wa habari, Tanzania Bara na  Zanzibar.



DKT.BITEKO ASEMA KUPIGA KURA NI UWEKEZAJI WA MAISHA

September 19, 2025 Add Comment
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewaasa wananchi kushiriki katika zoezi la upigaji kura Oktoba 29 ili kuchagua viongozi watakaoweza kutimiza matarajio yao ya kuwaletea maendeleo.


Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 19, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Lyambamgongo wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

“ Uchaguzi ni uwekezaji wa maisha, kupiga kura na kuchagua viongozi  inakupa uhalali wa kudai maendeleo kutoka kwa wale uliowachagua. Mimi huwa nashangaa mtu hapigi kura wala haudhurii vikao vya maendeleo lakini anakuwa wa kwanza kulalamika,” amesema Dkt. Biteko.


Amesema wapiga kura wa Kata hiyo 4,600 waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura na kuichagua CCM ili katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwaletee maendeleo.

Ametaja baadhi ya mikakati ya CCM katika Kata hiyo kuwa ni kuwaletea gari ya wagonjwa pamoja na kufikisha umeme katika vitongoji saba ambavyo havijafikiwa na umeme.


Fauka ya hayo, amewaeleza wananchi hao kuwa katika uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaruhusu wananchi wa Bukombe kuchimba madini katika Pori la Kigosi ili wapate fursa ya kujipatia kipato. 

Pia, amesema Wilaya ya Bukombe haikuwa na stendi, soko la kisasa wala jengo la halmashauri hata hivyo Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili wa utekelezaji wa miradi hiyo hivyo wamchague kwa kumpa kura nyingi Oktoba 29.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa wananchi kutogawanyika kwa sababu yoyote ile hususan wakati wa Uchaguzi Mkuu.


Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Lyambamgongo, Boniface Shitobero amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara, zahanati mbili, madarasa na vifaa vya maabara katika shule za sekondari.


“ Kuna shule shikizi ambayo ametuletea fedha kwa ajili ya kujenga madarasa, kila kijiji kina umeme,” amesema Shitobero.


Aidha, amesema CCM ikipewa ridhaa ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo itatekeleza miradi mipya kama shule na hospitali.


Mwisho.

RC DODOMA ATANGAZA KIAMA KWA WEZI WA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA

September 19, 2025 Add Comment

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amekemea vikali vitendo vya wizi wa Miundombinu ya Majitaka, hasa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka katika Jiji la Dodoma,vitendo vilivyoibuka na kushamiri kwa kasi siku za hivi karibuni.

Mhe. Mkuu wa Mkoa huo, amekemea vitendo hivyo wakati wa ziara yake akiambatana na Kamati ya Usalama Mkoa aliyoifanya Septemba 19, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Mjini Kati Dodoma.

Mhe. Senyamule ameonyesha kukerwa na tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya watu wasio na woga wa mali za serikali, na kwamba serikali itachukua hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani kwa kuwa vitendo wanavyofanya ni uhujumu uchumi.

Mhe. Senyamule ameahidi kupambana na kadhia hiyo ndani ya Mkoa kwa kuviagiza vyombo vya dola kuanza kazi kwa kuwabaini wahalifu hao pamoja na wanunuzi kwani makundi yote hayo yanachofanya ni uhalifu, uhujumu uchumi na kuhatarisha usalama wa raia wengine.

Awali akitoa taarifa kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma juu ya changamoto hiyo ya wizi wa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amesema hadi kufikia mwezi Agosti, 2025 mifuniko takribani 61 imeibiwa ikiwa ni hasara kwa serikali ya shilingi Milioni 91.


ORYX GAS NA TCRF WAENDELEA KUUNGA MKONO MATUMIZI YA NISHATI SAFI KWA KUZINDUA JIKO LA NISHATI SAFI SHULE YA SEKONDARI YUSUF MAKAMBA

September 19, 2025 Add Comment

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania kwa kushirikiana na tumeshirikiana na Tanzania Communities Rise Foundation(TCRF) wamezindua jiko linatumia mfumo wa nishati safi katika Shule ya Sekondari Yusuf Makamba iliyopo Dar es Salaam lengo likiwa kuondoa matumizi ya mkaa katika shule hiyo yenye wanafunzi 1391.

WATUMISHI WIZARA YA NISHATI WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZU SAHIHI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

September 19, 2025 Add Comment


📌 *Ni baada ya Dkt.Biteko kuwakabidhi  majiko yanayotumia umeme kidogo (Induction Cookers).*


📌 *Yaelezwa kuwa majiko hayo yanatumia umeme kidogo kwa gharama ndogo*

Watumishi wa Wizara ya Nishati leo wamepata  elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko yanayotumia umeme kidogo  ( Induction cookers) baada ya kukabidhiwa majiko hayo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko hivi karibuni.


Dkt. Biteko aliwakabidhi majiko hayo Watumishi wa Wizara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwa kutambua kuwa Watumishi hao ni mabalozi katika utoaji wa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati- Mtumba,  Dodoma yameandaliwa na Kitengo cha Nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na wataalam kutoka Kampuni ya Positive Cooker.



Akitoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya majiko hayo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni  ya Positive Cooker, Ndg. Atukuzwe Willson ameeleza kuwa lengo la utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya uhamasishaji  wananchi kutumia umeme kwa matumizi ya kupikia  kupitia majiko janja yanayotumia umeme kidogo.


“Lengo la kutoa elimu hii ni kuhakikisha  kila Mtanzania anaachana na matumizi ya nishati isiyosafi ili kulinda mazingira pamoja na   afya zetu lakini pia ni  sehemu ya jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia ambapo hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya  watanzania wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia." Amesema Willson

Akizungumza kuhusu  majiko hayo janja ya umeme amesema  yanatumia wastani  wa nusu uniti hadi uniti moja na nusu kwa wastani wa dakika 15 mpaka dakika 90 sawa na shilingi 65 mpaka shilingi 534 tu hali inayothibitisha ufanisi wa majiko hayo kuwa na  gharama nafuu, kuokoa muda, kulinda afya pamoja na mazingira.