DC UPENDO WELLA AWAASA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA MASHULENI

August 22, 2025 Add Comment


Na Ashrack Miraji 


Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mheshimiwa Upendo Wella, amewaasa wazazi na walezi wa Kata ya Tambukareli kuchangia fedha za chakula kwa ajili ya watoto wao mashuleni. Amesisitiza kuwa upatikanaji wa chakula shuleni ni jambo la msingi linalochangia kuboresha afya, maendeleo ya akili na ufaulu wa wanafunzi.


Mheshimiwa Wella alitoa wito huo wakati wa ziara yake katika Kata ya Tambukareli, akiwa kwenye ziara maalum ya kutembelea kata kwa kata kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Tabora. Alibainisha kuwa lishe bora ni msingi wa elimu bora na ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha watoto wanapata huduma hiyo muhimu.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, wananchi walionyesha kufurahishwa na ujio wa kiongozi huyo na walimpongeza kwa juhudi zake za dhati za kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati. Walisema kuwa utendaji wake umekuwa wa kipekee na unaleta matumaini mapya kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Mmoja wa wananchi, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alieleza kuwa Mkuu huyo wa Wilaya amekuwa mkombozi wa kweli kwa watu wa Tabora. Alisema kuwa tangu Mheshimiwa Wella alipoanza kuhudumu katika wilaya hiyo, matatizo mengi ambayo yalikuwa sugu sasa yameanza kupata suluhisho.



"Tunaona tofauti kubwa. Masuala ambayo hapo awali yalikuwa hayaangaliwi kwa uzito sasa yanapewa kipaumbele. Tunamshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea kiongozi kama huyu ambaye ni mchapakazi na mwenye kusikiliza wananchi," alisema mwananchi huyo kwa furaha.



Mheshimiwa Wella aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika kutatua changamoto zote zinazowakabili. Alisema dhamira yake kuu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na kwamba maendeleo ya wilaya hiyo yanakuwa ya haraka na jumuishi.


Ziara ya Mkuu wa Wilaya inaendelea katika kata mbalimbali za Tabora, ambapo anafanya mikutano ya hadhara, kusikiliza malalamiko ya wananchi, na kutoa majibu au miongozo ya moja kwa moja ili kuhakikisha matatizo yanatatuliwa kwa wakati na kwa tija

NCAA YALIPIA MASHABIKI 500 MECHI TAIFA STARS NA MOROCCO

August 22, 2025 Add Comment



Na Hamis Dambaya, DSM.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imenunua tiketi 500 kwa ajili ya kulipia mashabiki 500 kuingia uwanja wa Benjamini Mkapa leo tarehe 22 agosti, 2025 kwa ajili ya kushuhudia mechi ya  robo fainali ambapo timu ya Tanzania -Taifa stars itacheza na Morocco majira ya saa mbili usiku katika uwanja wa Benjamini mkapa Dar es Salaam.

Akikabidhiwa tiketi hızo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Meneja wa idara ya huduma za utalii na Masoko Mariam Kobelo amesema kuwa uamuzi wa kuingiza mashabiki hao 500 una lengo la kuunga mkono juhudi za serikali za kuendeleza michezo na utalii pamoja na kuhamasisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini hususani hifadhi ya Ngorongoro.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT)  Neema Msita ameipongeza NCAA kwa uamuzi huo na kusema kuwa michuano ya fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) imevuta mashabiki wengi  katika nchi za Afrika na dunia kwa ujumla hivyo ni sehemu muhimu ya kutangaza vivutio vya utalii.

Taifa stars na Morocco zitachuana ijumaa hii katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.


MWIKALO WA NLD ACHUKUA FOMU JIMBO LA TANGA

August 22, 2025 Add Comment






Na Oscar Assenga, Tanga.


MGOMBEA wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Tanga kwa tiketi ya Chama cha National League For Democracy (NLD) Ramadhani Mwikalo amesema dhamira yake ni kutaka kufufua viwanda vya mkoa pamoja na zao la Mkonge kwa kuliongezea thamani ikiwemo kulitafutia masoko zaidi nje ya nchi akieleza ndio  njia pekee ya kumaliza tatizo la ajira kwa wananchi.


Aliyasema hayo Agosti 21 mwaka huu mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo hilo na msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Tanga Mwanaidi Nondo , 

Alisema kwamba kwa sasa uhitaji wa Mkonge katika masoko ya nje ni mkubwa licha ya uzalishaji wake kuwa mdogo hivyo kuahidi kutafuta masoko pamoja na kushawishi wawekezaji kuja kwa wingi kuwekeza mkoani Tanga.


"Lengo letu kama chama ni moja tu kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Tanga katika nyanja nzima ya maendeleo na endapo nitapata ridhaa kwa nafasi ya ubunge kipaumbe cha kwanza zaidi ni kuhakikisha tunakwenda kuimarisha na kuzidisha kilimo cha zao la Mkonge lakini ukiangalia Kasi yake bado ni mdogo kulingana na uhitaji wa soko uliopo kwa sasa" amesema Mwikalo


"Lakini pia kufufua viwanda vilivyokufa na vilivyopo kuviimarisha vile vilivyopo kuongeza kasi ya uzalishaji lakini kuongeza ushirikiano na wawekezaji waliopo ili tuweze kupata viwanda vingi zaidi" ameongeza Mwikalo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Tanga Abdulkarim Nassoro amesema kuwa chama kinajivunia kumsimamisha Mgombea huyo kwa nafasi ya ubunge ambaye ana utaalumu katika sekta ya uzalishaji ikiwemo viwanda , masuala ya uvuvi pamoja na Madini wakiwa na imani kuwa kupitia nafasi yake itakuwa ni suluhisho la ajira kwa wananchi hususani vijana.


"Tanga tuna matatizo mengi ikiwemo matatizo kwa vijana katika ajira na Mwikalo ni mtaalamu wa masuala ya viwanda, anajua masuala mengi ya uvuvi na Tanga tumezungukwa na Bahari changamoto yake itakuwa imefiki utatuzi, tuna matatizo ya Barabara yetu yaTanga Pangani , Ramadhani ataisimamia lengo ni kuwa Barabara ya mfano katika kiwango cha lami tunayo maeneo mengi ya Madini pia Mgombea wetu atahakikisha hayo yote anakwenda kuyasimamia kwa manufaa ya wananchi" amesema Abdulkarim


Amesema kuwa pamoja na kumpata Mgombea ubunge Jimbo hilo pia limejipanga kwa kuhakikisha linasimamisha wagombea wa udiwani katika kata zote 27 za uchaguzi ambao watakwenda kuishawishi Halmashauri kuongez Kasi ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ili iende ikawe suluhisho la mikopo ya Kausha damu ambayo imekuwa ikiwadhalilisha wananchi hususani wanawake.


"Tutasimamisha wagombea katika kata zote 27 za Jimbo letu la Tanga tena watu wenye mvuto ambao wanaweza kujenga hoja ili waweze kumsaidia Mbunge wetu katika baraza la Halmashauri tunajua udhaifu uliopo kwa madiwani waliopita sasa lazima NLD tuonyeshe chachu kuleta mifumo mwingine wa uongozi" ameongeza mwenyekiti huyo.



WAZIRI KABUDI ATAJA MAMBO MATANO SEKTA YA HABARI INAPASWA KUTEKELEZA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

August 22, 2025 Add Comment

 


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, ametaja mambo matano ya msingi ambayo sekta ya habari inapaswa kutekeleza kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akifafanua, Profesa  Kabudi amesema jukumu la kwanza ni kuwajulisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao, la pili kutoa elimu juu ya sera za wagombea, na la tatu kuibua pamoja na kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.

Aidha, ametaja jukumu la nne kuwa ni kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum, ikiwemo vijana na wanawake, huku la tano likiwa kupambana na taarifa potofu na kuepuka kuzisambaza.

Profesa Kabudi ameyasema hayo katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unapaswa kuzingatia taaluma, weledi na maadili ya uandishi wa habari.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Wakili Patrick Kipangula, amesema ni kosa la jinai kwa waandishi wa habari kufanya kazi hiyo bila kuwa na ithibati.

Kipangula alisema hayo wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kanda ta mashariki, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

"Ukisoma kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari inaeleza kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi za uandishi wa habari ni lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, kwa hiyo hakuna mtu yoyote anaruhusiwa kufanya kazi yoyote ya kihabari isipokuwa tu awe amepewa ithibati na bodi, kwa hiyo waandishi ambao wanataka kufanya kazi ya kuripoti taarifa za uchaguzi wahakikishe wamepewa ithibati" alisema Kipangula.


Mwisho