Na Ashrack Miraji
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mheshimiwa Upendo Wella, amewaasa wazazi na walezi wa Kata ya Tambukareli kuchangia fedha za chakula kwa ajili ya watoto wao mashuleni. Amesisitiza kuwa upatikanaji wa chakula shuleni ni jambo la msingi linalochangia kuboresha afya, maendeleo ya akili na ufaulu wa wanafunzi.
Mheshimiwa Wella alitoa wito huo wakati wa ziara yake katika Kata ya Tambukareli, akiwa kwenye ziara maalum ya kutembelea kata kwa kata kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Tabora. Alibainisha kuwa lishe bora ni msingi wa elimu bora na ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha watoto wanapata huduma hiyo muhimu.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, wananchi walionyesha kufurahishwa na ujio wa kiongozi huyo na walimpongeza kwa juhudi zake za dhati za kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati. Walisema kuwa utendaji wake umekuwa wa kipekee na unaleta matumaini mapya kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Mmoja wa wananchi, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alieleza kuwa Mkuu huyo wa Wilaya amekuwa mkombozi wa kweli kwa watu wa Tabora. Alisema kuwa tangu Mheshimiwa Wella alipoanza kuhudumu katika wilaya hiyo, matatizo mengi ambayo yalikuwa sugu sasa yameanza kupata suluhisho.
"Tunaona tofauti kubwa. Masuala ambayo hapo awali yalikuwa hayaangaliwi kwa uzito sasa yanapewa kipaumbele. Tunamshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea kiongozi kama huyu ambaye ni mchapakazi na mwenye kusikiliza wananchi," alisema mwananchi huyo kwa furaha.
Mheshimiwa Wella aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika kutatua changamoto zote zinazowakabili. Alisema dhamira yake kuu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na kwamba maendeleo ya wilaya hiyo yanakuwa ya haraka na jumuishi.
Ziara ya Mkuu wa Wilaya inaendelea katika kata mbalimbali za Tabora, ambapo anafanya mikutano ya hadhara, kusikiliza malalamiko ya wananchi, na kutoa majibu au miongozo ya moja kwa moja ili kuhakikisha matatizo yanatatuliwa kwa wakati na kwa tija
EmoticonEmoticon