MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ASHIRIKI KIKAO CHA KIMATAIFA CHA SHERIA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI

July 22, 2025 Add Comment
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameshiriki kikao cha 58 cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za Biashara na Uwekezaji kinachofanyika kwa siku 2 kuanzia tarehe 21 hadi 22 Julai, 2025 Jijini Vienna, Austria. 

TANESCO YAANDIKA HISTORIA AJIRA MPYA

July 22, 2025 Add Comment

 📍Waajiriwa wapya 555 wapata ajira kwa mara moja

📍Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO afungua rasmi mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao 

Na: Mwandishi Wetu, Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeandika historia kwa kuajiri watumishi wapya 555 kwa mara moja, hayo yameelezwa katika uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao, huku Mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho, jijini Dodoma.

Mafunzo hayo yamefunguliwa tarehe 21 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, yakilenga kuwapa uelewa mpana kuhusu majukumu yao ndani ya Utumishi wa Umma na ndani ya Shirika, kabla ya kuanza kazi rasmi katika maeneo waliyopangiwa kote nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Dkt. Nyansaho aliwataka watumishi hao wapya kutambua uzito wa fursa waliyoipata na kuitumikia kwa bidii, uadilifu, na uaminifu mkubwa.

“Kipekee namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kibali cha kuajiri. Hii ni fursa ya kipekee, na ni wajibu wenu kuithamini kwa kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa,” alisisitiza Dkt. Nyansaho.

Akiwaasa kuhusu mwenendo wao wa kikazi, aliwakumbusha kuwa TANESCO imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo wanapaswa kuendeleza juhudi hizo kwa kuwahudumia wateja kwa kuwajibika na kuwa na maadili ya hali ya juu.

“Tumepiga hatua kwenye utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo ni muhimu muiendeleze kwa  kuwahudumia wateja kwa uaminifu na uadilifu kwa maslahi mapana ya Shirika na Taifa kwa ujumla" alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, aliwataka waajiriwa hao kuwa mabalozi wa Shirika katika maeneo yao ya kazi kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uaminifu, na kwa kutoa huduma bora kwa wateja.

“Katika majukumu yenu, mnakwenda kukutana na wateja wetu. Wahudumieni kwa heshima na kwa moyo wa kujitolea, ili kwa pamoja tuendelee kujenga taswira chanya ya TANESCO,” alieleza Bw. Twange.

Waajiriwa hao wameajiriwa na TANESCO hivi karibuni baada ya kupitia mchakato wa ajira, huku awali wakiwa wafanyakazi wa mikataba ya muda na ajira hizi mpya zinawapa fursa ya kupata ajira za kudumu.

RAIS SAMIA ATOA BILIONI NNE UJENZI KIWANDA CHA KUZALISHA NISHATI MBADALA*

July 22, 2025 Add Comment



📌Kiwanda kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi nchini


📌REA kugharamia ununuzi wa mtambo wa STAMICO


📌Stamico yapania kusambaza Nishati Safi ya Rafiki Briquettes kila kona

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) leo tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5.

Katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam, REA itatoa jumla ya shilingi bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5; kwa mchanganuo huo, REA itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia upatikanaji wa kiwanja, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa mitambo. 

Mkataba huo umesainiwa na Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.

Mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji wa mkaa mbadala vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na viwanda vingine viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji. 

Akizungumza  katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034. 

“Katika kufanikisha lengo hilo, Wakala unatekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo uwezeshaji katika kuongeza uzalishaji na usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Watu wa vijijini.”


“Utiaji wa saini wa Mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wakala ili kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa kuona namna ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi kwa Wananchi ili waondokane na matumizi ya nishati zisizo safi na salama”. Amesema Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu REA.

“Ni matumaini yetu kuwa Mkataba huu utaende kuongeza kasi ya upatikaji wa mkaa mbadala na kwa bei nafuu ikiwa ni mojawapo ya lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Tunatambua kuwa utunzaji wa mtambo huu ni muhimu sana ili huduma iliyokusudiwa iendelee kutolewa kwa wakati bila kuathili uchumi wa Wananchi, afya na pamoja na mazingira kwa ujumla”. Amekaririwa, Mhandisi, Hassan Saidy.

Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa mbadala, Wakala unaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo usambazi wa majiko banifu, usambazaji wa majiko ya umeme, usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia majumbani (LPG ya kilo 6 na 15); usambazaji wa gesi asilia katika mkoa wa Lindi na Pwani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma. 

Kwa upande wake, Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ameishukuru Serikali kupitia REA kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo  kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira. 

“Hii ajenda ya matumizi ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na nishati isiyo safi na salama. STAMICO tumejipanga kutekeleza maono haya ya Kiongozi wetu”, amesema Dkt. Mwasse. 


Ameongeza kuwa nishati ya Rafiki Briquettes kwa sasa inatumiwa na Jeshi la Magereza ambapo Magereza yote 129 nchini kote yanatumia nishati hii kama aina mojawapo ya nishati ya kupikia, vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). 

Taasisi nyingine ni pamoja na vyuo mbalimbali vya mafunzo, shule za msingi na sekondari, hoteli, migahawa, na sehemu wanazochoma nyama na chipsi. 


Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO itaendelea kutunza mitambo hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa Wananchi.



MWISHO!!!

NAIBU WAZIRI UMMY AKAGUA MAANDALIZI YA MASHUJAA

July 22, 2025 Add Comment




Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amefanya ukaguzi wa maandalizi  kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yanayotarajiwa kufanyika tarehe 25 Julai, 2025 katika Uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma.

Mhe. Nderiananga ametembelea  Uwanja huo leo tarehe 22 Julai, 2025 ili kujionea maandalizi ambapo amesema yamefikia hatua nzuri inayoridhisha.

Aidha katika maadhimisho hayo  mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.


JESHI LA POLISI TANGA LAKAMATA BOTI ILIKUWA IKISAFIRISHA MIRUNGI KUTOKA NCHINI KENYA

July 22, 2025 Add Comment








Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetekeleza operesheni ya mafanikio usiku wa tarehe 22 Julai 2025 kwa kukamata boti aina ya fibre, rangi nyeupe, iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amesema kuwa boti hiyo ilikamatwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine) katika eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale, mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga, kufuatia taarifa za kiupelelezi na ufuatiliaji wa kina wa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchunguzi, watuhumiwa wawili waliokuwa kwenye boti walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, lakini boti pamoja na shehena ya mirungi vilikamatwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeeleza kuwa litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani.
Aidha, Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika jamii, hususan vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.