WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI MAGEREZA NA VYUO VYA MAFUNZO WANOLEWA

June 22, 2025 Add Comment

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya waratibu, waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma. 
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya waratibu, waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma. 

Meza kuu ikiwa katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Ramadhani Kailima akizungumza jambo wakati wa mafunzo ya siku tatu ya Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha vifaa vya Bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha vifaa vya Bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma. 


Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha vifaa vya Bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma.
Hakimu Denis John Mpelembwa akiwaapisha washiriki 

Washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha vifaa vya Bayometriki wa Magereza kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 mkoani Dodoma wakila kiapo cha kutunza siri kabla ya kuanza mafunzo hayo.
Mratibu wa Uandikishaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mafunzo , akizungumza jambo.
Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Caroline Ruben akiwasilisha mada kuhusu uraia kwa washiriki wa mafunzo hayo. 
****************
Na. Waandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaasa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Magereza kwa Tanzania Bara na Vyuo vya Mafunzo kwa Tanzania Zanzibar kufanya kazi kwa weledi.
 
Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa watendaji hao ambayo yameanza leo tarehe 22 Juni, 2025 Mkoani Dodoma kwa Magereza sambamba na Unguja kwa Vyuo vya Mafunzo. 

Akifungua mafunzo kwa watendaji hao yaliyofanyika Mkoani Dodoma kwa watendaji wa Magereza, Tanzania Bara, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele amesema Tume imewateua watendaji hao kutokana na weledi wao.
 
“Sina shaka kuwa kuteuliwa kwenu kunatokana na ujuzi, uwezo na weledi mlionao katika kutekeleza majukumu ya kitaifa likiwepo zoezi la uboreshaji wa Daftari ambalo ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” amesema Mhe. Mwambegele.
 
Amewahakikishia watendaji hao kuwa kwenye mafunzo hayo ya siku tatu Tume itawapa ujuzi wa kutosha kwa nadharia na vitendo kuwawezesha kutekeleza jukumu lao kwa weledi.
 
Akifungua mafunzo kama hayo Kisiwani Unguja, Zanzibar kwa watendaji wa Vyuo vya Mafunzo, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani Mstaafu, Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk ametoa wito kwa watendaji hao kuvitunza vifaa vya uboreshaji wa daftari.
 
“Ninatoa wito kwenu kuhakikisha mnavitunza vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari na kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi kwa usahihi wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo,” amesema.
 
Jaji Mbarouk pia amewahakikishia watedaji hao kuwa maafisa kutoka Tume watakuwepo muda wote wa zoezi na kwamba endapo watapata changamoto ya aina yoyote wasisite kuwasiliana nao.
 
Kwa mujibu wa ratiba zoezi hilo la uboreshaji wa Dafatri kwenye Magereza na Vyuo vya Mafunzo linafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 04 Julai, 2025 ambapo watakaohusika ni mahabusu na wafungwa walihukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe, Jaji wa Rufani (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk 
akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya waratibu, waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wa Vyuo vya Mafunzo kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yaliyoanza leo Juni 22 -24, 2025 Mjini Unguja Zanibar. 
Mkurugenzi wa Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Adam Mkina akizungumza wakati wa Mafunzo hayo.
Meza Kuu ikiwa katika mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea 

KAMISHNA KUJI AZINDUA JENGO LA UTAWALA, NYUMBA ZA WATUMISHI HIFADHI YA TAIFA MTO UGALLA

June 21, 2025 Add Comment


Na. Edmund Salaho, Kaliua -Tabora


Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji leo tarehe 21, Juni 2025 amefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla iliyopo Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora na kuzindua Jengo la Utawala pamoja na nyumba za watumishi kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA.


Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa majengo hayo Kamishna Kuji alisisitiza kutunzwa kwa miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

“Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendeleza juhudi za kuboresha miundombinu katika hifadhi hizi mpya kwa kuboresha miundombinu ya barabara majengo ya Utawala hifadhi, Nyumba za Askari pamoja  na Vitendea kazi vingine, hivyo, nisisitize kuitunza miundombinu hii ili iweze kutumika kwa muda mrefu”.

“TANAPA tuna kila sababu ya kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anaendelea kuiboresha sekta hii ya Utalii na Uhifadhi hapa nchini. Uwekezaji wa miundombinu hii ni mwendelezo wa adhma kubwa ya Serikali katika Hifadhi za Taifa Nchini. Tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wake kwani matokeo ya juhudi zake yanaonekana” alisema Kamishna Kuji.


Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla alibainisha kuwa, Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ilipatiwa fedha za kutekeleza mradi wa Jengo la Utawala, Nyumba za watumishi tatu (3), pamoja na nyumba ya Mkuu wa Hifadhi vyote vikigharimu kiasi cha ShsT. milioni 701.9 ambapo kwa sasa miradi hii yote imekamilika na iko tayari kwa matumizi.

Pia, Kamishna Kuji alifanikiwa kufanya kikao na Menejimenti ya hifadhi pamoja na Maafisa na Askari Uhifadhi wa hifadhi hiyo na kujadili mikakati ya namna bora ya kukuza uhifadhi na kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii ili kupata mapato mengi na kutoa mchango mkubwa wa mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ni moja ya Hifadhi mpya tano zilizopandishwa hadhi mwaka 2019 na kuwa Hifadhi ya Taifa. Hifadhi hii yenye sifa kedekede kwa mandhari yake nzuri na ya kuvutia ya Mto Ugalla, Misitu ya miombo yenye makundi makubwa ya wanyama ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 3,865 na ni ya sita kwa ukubwa kati ya Hifadhi 21 za Taifa Ilizopo hapa nchini.

Uboreshwaji wa miundombinu katika katika hifadhi za Taifa hasa zile zilizopandishwa hadhi mwaka 2019 ni suala muhimu ili kuweka mazingira mazuri ya kukuza utalii na kufanikisha shughuli za utawala na uhifadhi.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MUHEZA YATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA WA VIUNGO,MACHUNGWA NA MKONGE

June 21, 2025 Add Comment


Na Oscar Assenga, MUHEZA


Halmashauri ya Wilaya ya Muheza,imewatangazia Neema kubwa ,Wakulima wa Machungwa na Matunda aina ya Machungwa,

Neema hiyo kubwa inakuja wakati ambao Kilimo cha mazao hayo kikizidi kukua wilayani humo.


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt.Jumaa Mhina aliwaambia Waandishi wa Habari, wakati wa hafla ya kuwaaga Madiwani wa Halmashauri hiyo iliyofanyika leo wilayani humo,

Dkt Mhina amesema ,wawekezaji wameshaanza kujitokeza kwaajili ya kujenga viwanda na baadhi ya viwanda vitatangazwa hivi karibuni,

"Tayari tumepokea wawekezaji ambao wameshajenga viwanda vya usindikaji wa mazao ya viungo vya chai na sasa mazao hayo yamepanda thamani ambapo karafuu,imepanda kutoka 6,000 hadi 20,000 kwa kg moja ,hivyo hivyo kwa mazao mengine ni hivyo kama pilipili manga,midarasini na Iriki,mazao yote haya yamepanda juu sana kwenye soko" Aliongeza Dkt.Mhina


Kuhusu Zao la Machungwa na Mkonge,Dkt.Mhina alisema,mazao hayo kwasasa kuna Uwekezaji mkubwa unakuja na utatangazwa hivi karibuni, alisema kwasasa kuna kiwanda kinachojihusisha na usindikaji wa maganda ya Machungwa kimeanza kufanya kazi, nakwamba wawekezaji wengine wameshaanza kujitokeza kwaajili ya kufanya Uwekezaji,

"kuhusu za Machungwa, tayari viwanda vya usindikaji vimeshaanza kazi hasa kiwanda Cha kusindika maganda ya Machungwa, lakini pia wawekezaji wengine wameshaanza kujitokeza,

kwa upande wa Mkonge,kilio cha mitambo ya kisasa aina ya korona kuchakata Mkonge wa daraja la 1,2,3,4 ,hadi mwishoni mwaka huu kila kitu kitakuwa tayari na tutawangazia hivi karibuni" Alisisitiza Dkt.Mhina


Kwaupande wake, Mwenyekiti anayemaliza muda wake katika Halmashauri hiyo,Erasto Mhina, amesema,kwakipindi cha miaka mitano wamejitahidi kutekereza miradi mbalimbali katika Wilaya hiyo ikiwemo kuwainua Wakulima wa Mazao ya Kimkakatati kwakuwatafutia masoko makubwa ambayo yamesaidia kuinua uchumi wa Wakulima,

" Uchumi wa wakazi wengi wa Muheza unategemea zaidi Kilimo hasa cha Machungwa na Viungo vya chai,tumejitahidi sana kutekereza miradi hii ya Kilimo na sasa Tunapereka nje ya nchini" Aliongeza Mhina

MWISHO

TANZANIA NA URUSI KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI

June 21, 2025 Add Comment


📌 *Dkt. Biteko awakaribisha Warusi kuwekeza katika nishati safi ya kupikia*


📌 *Urusi kuisaidia Tanzania katika afya, usalama mtandao na ulinzi wa miundombinu*


📌 *Kampuni kubwa ya nishati duniani INTER RAO Export yaonesha nia ya kuwekeza Tanzania*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev kuhusu kuimarisha ushirikiano  katika sekta ya nishati na maeneo mengine muhimu ikiwemo teknolojia na uwekezaji.


Mazungumzo hayo kati ya Dkt. Biteko na Mhe. Tsivilev yamefanyika kando ya Jukwaa  la Kimataifa la Uchumi St. Petersburg nchini Urusi.

Kupitia mkutano huo Dkt. Biteko amesema kiwango cha uwekezaji  nchini kutoka Urusi kinafikia  dola za Kimarekani milioni 424 kupitia miradi 44 inayoajiri watu zaidi ya 3,000 huku akielezea fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati. 


"Tanzania ina asilimia 61.7 ya nishati kutoka vyanzo vinavyoweza kurejeshwa na fursa za uwekezaji zenye thamani ya dola bilioni 4 katika sekta ya nishati," amesema Dkt. Biteko.

Ametaja jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya nishati sambamba na kushirikisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitolea mfano Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Dar es Salaam mwezi Januari 2025 uliolenga kutoa umeme kwa waafrika milioni 600 ambao hawana umeme.


Pia, Dkt. Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Urusi kuongeza uwekezaji nchini hususan katika nishati safi ya kupikia ambapo ameelezea uwepo wa fursa za uwekezaji wa sekta binafsi  za uzalishaji umeme wa kujitegemea na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amefurahishwa na uhusiano wa kidiplomasia wa takribani miaka 64 kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uhusiano huo unalenga kunufaisha wananchi wa nchi hizo.


Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amezungumzia umuhimu wa nishati katika maendeleo ya kiuchumi hususan katika masuala ya usalama wa nishati, upatikanaji, bei nafuu, na ufanisi. 


Mhe. Tsivilev amesema kuwa Urusi ipo tayari kusaidia teknolojia na kujengea uwezo wataalamu wa Afrika ikiwemo Tanzania ili kuhakikisha uhuru wa teknolojia unakuwepo.

"Urusi ina mkakati wa haki katika ushirikiano na malengo ya kuendeleza mifumo ya nchi kwa washirika wa muda mrefu," amesema  Mhe. Tsivilev.


Amezungumzia maeneo mengine ambayo Urusi imeahidi kuisaidia Tanzania ni pamoja na afya, usalama wa mtandao na ulinzi wa miundombinu muhimu.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INTER RAO Export, ambayo ni moja ya Kampuni kubwa zaidi ya nishati duniani, Bw. Maxim Sergeev licha ya  kuonesha  nia ya kuwekeza nchini amesema kuwa Kampuni hiyo ina uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo mashine umba na jenereta pia ina mikataba ya kila mwaka inayofikia dola bilioni 8.

Aidha, mazungumzo hayo kati ya Dkt. Biteko na Tsivilev yamehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania Moscow, Mhe.  Frederick Kibuta, Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi John Ulanga na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Marwa Petro.


Kando ya mazungumzo  hayo naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange amefanya mazungumzo na Kampuni ya Rosatom na Unigreen kuhusu ushirikiano wa uzalishaji wa umeme unaotokana na urani pamoja na jua ambapo Unigreen inaendelea na taratibu za uwekezaji nchini.


*Mwisho*

Benki ya CRDB yatoa zawadi kwa watoto Muhimbili, yamuaga Profesa Janabi

June 21, 2025 Add Comment

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohammed Janabi kumtakia utumishi mwema wa majukumu anayoenda kuyaanza hivi punde. Hafla hiyo fupi ilifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili sambamba na kuwafungulia Akaunti ya Junior Jumbo Watoto 76 waliozaliwa hospitalini hapo.

Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohammed Janabi (kushoto) akimsikiliza kwa umakini Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kumuaga na kumtakia kazi njema katik amajukumu yake mapya anayotaraji akuyaanza hivikaribuni.



Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) na Balozi wa Akaunti ya Junior Jumbo ya Benki ya CRDB, Paula Masanja (kushoto) wakimkabidhi mmoja wa wanawake (katikati) waliojifungua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zawadi kwa ajili ya mtoto wake kuadhimisha Wiki ya Mtoto wa Afrika.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam. Tarehe 19 Juni 2025: Katika kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa Juni 16 kila mwaka, Benki ya CRDB imetembelea wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapongeza wazazi kwa kujifungua salama.

Licha ya ziara hiyo iliyofanyika katika wodi ya watoto njiti hospitali hapo, Benki ya CRDB pia imetumia nafasi hiyo kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi kwa kushinda kiti cha Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema siku zote wamekuwa wakitoa elimu ya fedha na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma za benki tangu wakiwa wadogo ili kujenga msingi imara wa uchumi binafsi siku zijazo.

“Katika wiki hii ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tumeona ni vyema kuja kuzungumza na wazazi hapa Muhimbili. Tunasisitiza elimu ya fedha ianze kutolewa tangu kwa watoto wadogo na ili kuliweka suala hili kwa vitendo, watoto wote waliopo hapa tutawafungulia Akaunti ya Junior Jumbo yenye shilingi 10,000 ya kuanzia ili mzazi akitoka hapa akaendeleze utaratibu wa kumtunzia mwanaye fedha zitakazomsaidia siku zijazo,” amesema Nsekela.

Kwa akiba yoyote iliyomo kwenye Akaunti ya Junior Jumbo, Benki ya CRDB hutoa riba ya mpaka asilimia 5 kwa mwaka hivyo kumpa uhakika mzazi au mlezi uhakika wa fedha za uhakika pindi mwanaye atakapoanza shule au atakapokuwa na mahitaji mengine yanayohitaji fedha.

“Akiba inawekwa kidogokidogo ingawa matumizi yake huwa makubwa pale yanapojitokeza. Ni vizuri kujenga utamaduni wa kuhifadhi fedha kidogo ambazo kadri muda unavyoenda zitazidi kuongezeka hivyo kutosha kwa ada na matumizi mengine ya shule au kwa jambo jingine ambalo mzazi atahitaji kulifanya kwa ajili ya mtoto wake,” amesema Nsekela.

Akimuaga Profesa Janabi anayetarajia kuondoa wiki ijayo kwenda kuanza majukumu yake mapya na Shirika la WHO hivi karibuni, Nsekela amemsifu kwa mikakati makini aliyonayo na kumuahidi kwamba Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana naye huko na anakokwenda na itaendeleza uhusiano mwema uliopo na Hospitali ya Taifa Muhimbili hata baada ya yeye kuondoka.

“Nilikusikiliza wakati wa kampeni za kuomba uchaguliwe kuiongoa WHO. Ulikuwa na mikakati 10 lakini mimi nimevutiwa na tatu ambazo ni utafiti na ubunifu, ubia pamoja na ufadhili wa huduma za afya kwa vyanzo vya ndani. Naamini vipaumbele hivi sio tu vitazifaa nchi zote 47 utakazokuwa unazihudumia bali vinato anafasi kwetu sekta binafsi kushiriki zaidi kuimarisha huduma za afya katika mataifa yetu. Benki ya CRDB itashirikiana nawe katika maeneo haya yote,” amesema Nsekela.

Kwa upande wake, Profesa Janabi ambaye ameimarisha ufanisi huduma hospitalini hapo tangu alipoteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji mwaka 2022, ameishukuru Benki ya CRDB kwa kwenda kumuaga akisema ni kampuni ya kwanza kufanya hivyo jambo linaloonyesha heshima kubwa ambayo taasisi hiyo kubwa ya fedha imempa.

“Uhusiano wangu na Benki ya CRDB ni wa muda mrefu. Tangu nilipokuwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tulikuwa pamoja mkitusaidia kugharimia matibabu ya watoto. Nafurahi mmenikumbuka leo na kuja kuniaga,” amesema Profesa Janabi.

Akitarajiwa kuondoka wiki ijayo, Profesa Janabi anaiacha Tanzania akikumbukwa kwa utoaji wake wa elimu kupitia mitandao ya kijamii jambo lililoongeza hamasa ya kuepuka ulaji usiozingatia mahitaji ya kiafya unaoweza kumsababishia mtu magonjwa yasiyoambukiza.

Katika kuendeleza elimu hiyo, Profesa Janabi aliwaeleza wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwamba wangepata chakula cha mchana pamoja na akasisitiza: “Mlo wetu leo utakuwa tunda moja la apple (tufaa).”

Akiwa mkurugenzi mtendaji mwanzilishi wa JKCI, Profesa Janabi alifanikiwa kuifanya kuwa taasisi mahiri inayohudumia wagonjwa wa ndani na watokao nje ya nchi hivyo kuacha mchango ambao hautosahaulika.

Balozi wa Akaunti ya Junior Jumbo, Paula Masanja aliwatia moyo wazazi waliojifungua watoto njiti na kuwahamasisha kuitumia akauniti hiyo kwa ajili ya watoto yao akisema ni muhimu kuwa na akiba kwa ajili ya matumizi yatakayojitokeza wakati wowote.

“Nami ni mzazi mwenye mtoto mdogo kama ninyi. Akaunti ya Junior Jumbo ni nzuri, itumieni kwa ajili ya watoto wenu,” alihamasisha Paula.