HOSPITALI ZATAKIWA KUSIMAMIA, KULINDA MIUNDOMBINU ILIYOPO

June 16, 2025 Add Comment


Na WAF - Bariadi, Simiyu 


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Hospitali zote nchini kuwa na utamaduni wa kusimamia na kulinda miundombinu iliyopo kwa wivu mkubwa kwakuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na vifaa tiba. 

Waziri Mhagama amesema hayo leo Juni 15, 2025 alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simuyu kwa lengo la kukagua ubora na huduma zinazotolewa, kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya mama na mtoto, kukagua ujenzi unaoendelea katika jengo hilo pamoja na kuzungumza na watumishi katika hospitali hiyo.  

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameirahisisha sana kazi yetu ya tiba nchini, ameifanya iwe nyepesi, kuna mashine na miundombinu ya kila aina, hapo mtoaji huduma amerahisishiwa kwa kiasi kikubwa sana, na hiyo ndio faida ya Serikali sikivu," amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagma amesema Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 29 kwenye huduma za afya ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 19.8 hivyo miundombinu iliyopo inapaswa kulindwa kwa wivu mkubwa. 

"Ombi langu jingine kwenu ninyi watumishi mzingatie maadili katika utoaji wa huduma zenu, wakataeni wale  wanaokwepa kiapo chao cha maadili na kujiingiza kwenye makosa ya jinai, tuzingatie viapo vyetu na kutoa huduma kwa utu na usiri mkubwa," amesisitiza Waziri Mhagama. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama ameitaka Idara ya TEHAMA kusimamia mwenendo mzima wa usimamizi wa shughuli zote za hospitali na kuacha mara moja mapungufu yote yaliyopo katika Idara hiyo. 


Jambo jingine, Waziri Mhagama amesema kumekuwa na tatizo la lishe katika mkoa wa Simiyu, ameielekeza hospitali kushirikiana na mkoa kutengeneza mazingira mazuri ya kutoa elimu kwa kina mama badala ya kusubiri hadi watoto wakiwa wagonjwa ili kuhakikisha vifo vyao vinapungua nchini.

DKT. ADESINA AMALIZA ZIARA YA SIKU NNE NCHINI TANZANIA

June 15, 2025 Add Comment
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 4 aliyoifanya nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 hadi 15 Juni 2025.

Dkt. Adesina aliondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kusindikizwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo.

Ziara ya Dkt. Adesina nchini imetokana na mwaliko kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa madhumuni ya kutembelea miradi ambayo benki hiyo imetoa fedha ya kuigharamia.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na barabara ya mzunguko ya Dodoma ambayo kwa pamoja Rais Samia na Dkt. Adesina waliitembelea jijini Dodoma Juni 14, 2025.

Dkt. Adesina ni Rais wa 8 wa AfDB na katika uongozi wake amefanya mageuzi makubwa katika benki hiyo na kuifanya kuwa chombo imara, chenye mtaji wa kutosha na utaalamu wa kuchagiza mageuzi ya kiuchumi barani Afrika hususan katika sekta za miundombinu, kilimo, afya, nishati, mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya kifedha.

Kutokana na mchango mkubwa alioutoa barani Afrika, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kilimtunikia Shahada ya Heshima ya Falsafa katika Sayansi katika mahafali ya 55, duru ya kwanza yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Juni 13, 2025.












MNYETI AWATAKA WAFUGAJI KUFUNGA KISASA KUONGEZA TIJA

June 14, 2025 Add Comment


Na. Stanley Brayton, WMUV 

PWANI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wafugaji kuachana na Ufugaji wa kizamani na kufuga kisasa ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini itakayoendana na mahitaji ya Soko ya sasa.

Akizungumza katika Ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Ufugaji Kibiashara na Mnada wa Mifugo yanayoshirikisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Namibia, yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo iliyopo Chalinze  Mkoa wa Pwani, Mhe. Mnyeti, amesema Serikali awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa inaendelea kuhamasisha wafugaji kuachana na Ufugaji wa kizamani na kuingia kwenye Ufugaji wa kisasa wenye tija.



“Ni matumaini yangu kuwa wafugaji mtachangamkia fursa hii kwa kutafuta na kununua mbegu bora za mifugo zitakazowaletea tija zaidi kwenye ufugaji wenu kuliko kuendelea na Ufugaji wa kizamani usio na tija.” ameseama Mhe. Mnyeti 


Aidha, Mhe. Mnyeti amesema maonesho hayo ya mifugo yamelenga  kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za mifugo ili kumwezesha mfugaji kuzalisha mazao mengi ya mifugo na kupata faida zaidi ili kuifanya Sekta ya Mifugo iweze  kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa  na kuwawezesha pato la mtu mmoja mmoja.


Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema swala la Malisho ya Mifugo imekuwa changamoto na wafugaji wengi wanatembea na rundo kubwa la mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho, lakini Ufugaji wa kisasa utasaidia kuwa na Mifugo michache yenye tija ambayo italeta faida kubwa kutokana na uzito na ubora wa mifugo kuliko kuwa na Mifugo mingi yenye uzito mdogo ambayo haina faida yeyote wala tija.

Katika hatua nyingine  Mhe. Mnyeti amewataka wafugaji kutafuta mbegu Bora za Malisho na kuzipanda kwa wingi kwa ajili ya Mifugo yao ili Mifugo iweze kupata chakula Cha kutosha kitakachowafanya kuwa Bora zaidi.

Mhe. Mnyeti amehitimisha hotuba yake kwa kukishukuru Chama cha Wafugaji Ng’ombe Kibiashara, Ranchi ya Mbogo pamoja na wadau wengine kwa kuandaa na kufanikisha maonesho hayo ambayo yameambatana na mnada wa mbegu bora za mifugo zenye tija zaidi kwenye uzalishaji wa Mifugo Bora mana wameungana na Serikali katika kuhamasisha Ufugaji wa kisasa.



LATRA YATOA MWEZI MMOJA WATOA HUDUMA WA TIKETI MTANDAO KUUNGANISHA MIFUMO NA SERIKALI

June 14, 2025 Add Comment
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka watoa huduma wa tiketi mtandao kuunganisha mifumo yao na mfumo wa serikali inayosimamiwa na LATRA pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kabla ya Julai 1, 2025.

DKT.BITEKO AWAASA CCM BUKOMBE KUDUMISHA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

June 14, 2025 Add Comment


📌 Azindua maduka ya kisasa 31 Ushirombo


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,  Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Bukombe wasikubali kuvutana na kugombana bali wadumishe amani, kuendelea kuheshimiana na kulinda utu wao hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Dkt. Biteko amesema hayo Juni 14, 2025 wilayani Bukombe, mkoani Geita mara baada ya kuzindua maduka 31 ya kisasa yaliyopo katika eneo la Ofisi za CCM wilayani humo.

“Naomba niwakumbushe tena kwa sasa tunaukaribia mwezi wa Oktoba, 2025. Tunakaribia kuingia katika zoezi la Uchanguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, niwaombe tu kwamba, zoezi la uchaguzi ni zoezi la mara moja, lakini maisha yetu sisi yanadumu na yataendelea kudumu na kuna maisha baada ya kampeni na baada ya Uchanguzi. Hivyo, kwa heshima, nawaomba tuendelee kudumisha umoja, upendo na undugu uliopo baina yetu,” amesema Dkt. Biteko.


Katika hatua nyingine, amezungumzia ujenzi wa maduka hayo ya kisasa kuwa ni hatua kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa eneo hilo la Ushirombo na maeneo mengine ya jirani kwa kuwa ni chanzo cha maendeleo na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.

Amesisitiza “ Maduka haya yataongeza mvuto na hivyo kuongeza thamani ya eneo hili la ardhi pamoja na thamani ya jengo. Ukuaji wa eneo letu hili huchangiwa zaidi na shughuli za madini na shughuli nyingine za kiuchumi. Taarifa zinaonesha kuwa, Mkoa wa Geita umeonesha kasi kubwa zaidi ya ukuaji kutokana na shughuli za madini, na watu wanaochimba watapata huduma kwenye hili,”

Aidha, amewapongeza na kuwashukuru Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe na Madiwani 23 kwa ushirikiano wao na kusema kuwa wamefanya kazi kubwa ya kuchangia ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa anafurahishwa kufanya kazi nao akiongeza kuwa wajumbe wa kata wanazotoka wanaweza kuwapima kwa kazi walizofanya. 

Dkt. Biteko amesema kuwa CCM katika wilaya hiyo itaendelea kuunga mkono mawazo mapya yatakayotolewa kwa ajili ya kusaidia maendeleo ambapo ametaja baadhi ya miradi ya ujenzi wa soko, stendi na barabara inayoendelea kujengwa wilayani humo inalenga kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.

Vilevile, Dkt. Biteko awaomba wanachama wa CCM kumuunga mkono kwa kumchagua Rais Samia na mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila  amewapongeza CCM Wilaya ya Bukombe kwa ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa hilo ni darasa na siasa ni uchumi na ni wajibu wa CCM kukiimarisha chama chao. 


Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mkoa wa Geita, Evarist Gervas amepongeza Dkt. Biteko kwa kuimarisha Chama katika wilaya  hiyo na kushirikiana vizuri na viongozi wa Chama kwa kuimarisha wilaya hiyo kiuchumi.


Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa maduka hayo ya kisasa, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa amesema kuwa Wilaya hiyo  inatimiza sera ya CCM ya miradi ya uwekezaji na kwa kutambua kauli mbiu ya siasa na uchumi, ilitekeleza wazo la ujenzi wa maboresho ya vibanda hivyo 21 vilivyokuwepo awali liliasisiwa na Mbunge wa jimbo la Bukombe Dkt. Biteko.


Amesema Dkt. Biteko alitoa wito wa kuwa na vitega uchumi zaidi vya Chama cha Mapinduzi na kutunza na kuboresha mandhari ya eneo la CCM la Wilaya ya Bukombe. Ndipo Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Bukombe ikapitisha pendekezo hilo.


Ametaja faida za mradi kuwa ni pamoja na CCM wilayani humo kukusanya mapato kwa wingi.


MWISHO