DKT.BITEKO AWAASA CCM BUKOMBE KUDUMISHA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU
habari siasa📌 Azindua maduka ya kisasa 31 Ushirombo
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Bukombe wasikubali kuvutana na kugombana bali wadumishe amani, kuendelea kuheshimiana na kulinda utu wao hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Dkt. Biteko amesema hayo Juni 14, 2025 wilayani Bukombe, mkoani Geita mara baada ya kuzindua maduka 31 ya kisasa yaliyopo katika eneo la Ofisi za CCM wilayani humo.
“Naomba niwakumbushe tena kwa sasa tunaukaribia mwezi wa Oktoba, 2025. Tunakaribia kuingia katika zoezi la Uchanguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, niwaombe tu kwamba, zoezi la uchaguzi ni zoezi la mara moja, lakini maisha yetu sisi yanadumu na yataendelea kudumu na kuna maisha baada ya kampeni na baada ya Uchanguzi. Hivyo, kwa heshima, nawaomba tuendelee kudumisha umoja, upendo na undugu uliopo baina yetu,” amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, amezungumzia ujenzi wa maduka hayo ya kisasa kuwa ni hatua kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa eneo hilo la Ushirombo na maeneo mengine ya jirani kwa kuwa ni chanzo cha maendeleo na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.
Amesisitiza “ Maduka haya yataongeza mvuto na hivyo kuongeza thamani ya eneo hili la ardhi pamoja na thamani ya jengo. Ukuaji wa eneo letu hili huchangiwa zaidi na shughuli za madini na shughuli nyingine za kiuchumi. Taarifa zinaonesha kuwa, Mkoa wa Geita umeonesha kasi kubwa zaidi ya ukuaji kutokana na shughuli za madini, na watu wanaochimba watapata huduma kwenye hili,”
Aidha, amewapongeza na kuwashukuru Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe na Madiwani 23 kwa ushirikiano wao na kusema kuwa wamefanya kazi kubwa ya kuchangia ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa anafurahishwa kufanya kazi nao akiongeza kuwa wajumbe wa kata wanazotoka wanaweza kuwapima kwa kazi walizofanya.
![]() |
Dkt. Biteko amesema kuwa CCM katika wilaya hiyo itaendelea kuunga mkono mawazo mapya yatakayotolewa kwa ajili ya kusaidia maendeleo ambapo ametaja baadhi ya miradi ya ujenzi wa soko, stendi na barabara inayoendelea kujengwa wilayani humo inalenga kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
![]() |
Vilevile, Dkt. Biteko awaomba wanachama wa CCM kumuunga mkono kwa kumchagua Rais Samia na mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila amewapongeza CCM Wilaya ya Bukombe kwa ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa hilo ni darasa na siasa ni uchumi na ni wajibu wa CCM kukiimarisha chama chao.
Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mkoa wa Geita, Evarist Gervas amepongeza Dkt. Biteko kwa kuimarisha Chama katika wilaya hiyo na kushirikiana vizuri na viongozi wa Chama kwa kuimarisha wilaya hiyo kiuchumi.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa maduka hayo ya kisasa, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa amesema kuwa Wilaya hiyo inatimiza sera ya CCM ya miradi ya uwekezaji na kwa kutambua kauli mbiu ya siasa na uchumi, ilitekeleza wazo la ujenzi wa maboresho ya vibanda hivyo 21 vilivyokuwepo awali liliasisiwa na Mbunge wa jimbo la Bukombe Dkt. Biteko.
Amesema Dkt. Biteko alitoa wito wa kuwa na vitega uchumi zaidi vya Chama cha Mapinduzi na kutunza na kuboresha mandhari ya eneo la CCM la Wilaya ya Bukombe. Ndipo Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Bukombe ikapitisha pendekezo hilo.
Ametaja faida za mradi kuwa ni pamoja na CCM wilayani humo kukusanya mapato kwa wingi.
MWISHO
TFS YABORESHA MIUNDOMBINU YA UTALII MSITU WA PUGU KAZIMZUMBWI KUPITIA MRADI WA BIONUWAI
habariKisarawe, Pwani – Juni 2025
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi, unaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha miundombinu rafiki kwa utalii katika maeneo ya hifadhi ya misitu nchini.
Katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, moja ya misitu ya asili ya pekee inayopatikana karibu kabisa na Jiji la Dar es Salaam, mradi huu unajenga jengo la kisasa la mbao kwa ajili ya mapumziko ya watalii. Jengo hilo, lenye ukubwa wa mita za mraba 72, litakuwa na sehemu tatu za kupumzikia wageni na lina uwezo wa kuhudumia hadi watu 50 kwa wakati mmoja.
Kazi ya ujenzi imefikia asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 26 Juni 2025 kwa gharama ya shilingi milioni 120. Kukamilika kwa jengo hili kutakuwa hatua muhimu ya kuboresha huduma kwa wageni na kuongeza mvuto wa utalii wa misitu katika Ukanda wa Pwani.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya kazi, Msimamizi wa Ujenzi, Bw. Fredrick Chakyi alisema kuwa mradi sasa unasonga mbele kwa kasi baada ya changamoto za mvua zilizokuwepo awali kupungua.
“Awali mvua zilikuwa changamoto kubwa, lakini hali sasa ni shwari. Tunatarajia kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa,” alisema Chakyi.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baraka Mtewa, alieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuimarisha utalii wa misitu na kuhifadhi bioanuwai kwa njia endelevu.
“Mradi huu utasaidia kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, kuongeza mapato ya hifadhi, na kuchochea maendeleo ya kijamii kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka Msitu wa Pugu Kazimzumbwi,” alisema Mtewa.
Kwa msaada wa UNDP na ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), mradi huu unalenga kulinda mazingira ya asili, kuimarisha uthibiti wa mabadiliko ya tabianchi, na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, jamii, na wadau wa maendeleo.
TFS inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali ili kuhakikisha kuwa rasilimali za misitu si tu zinahifadhiwa, bali pia zinatumika kwa njia endelevu katika kuleta tija kwa taifa – kijamii, kiuchumi, na kimazingira.
KAMISHNA WA UMEME NA NISHATI JADIDIFU AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM
habari▪️Aridhishwa na hatua ya utekelezaji wa miradi
▪️Awataka wakandarasi kuzingatia viwango na TANESCO kuongeza usimamizi ili kuepuka ongezeko la gharama
▪️Aisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika
Na. Agnes Njaala, Dar es Salaam
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, tarehe 12 Juni 2025, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ya Gridi Imara inayoendelea katika Jiji la Dar es Salaam, na kutoa maelekezo muhimu kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.
Miradi hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma bora na ya uhakika kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Kamishna amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, licha ya changamoto mbalimbali za kimazingira, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na jitihada za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
“Nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa, lakini nimeagiza wakandarasi waharakishe kazi, vifaa vipatikane kwa wakati, na viwango vya kazi vizingatiwe ili miradi hii itoe matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi,” amesisitiza Mhandisi Luoga.
Akifafanua amebainisha kuwa miradi hiyo ya kimkakati, inayotekelezwa na TANESCO kwa ufadhili wa Serikali, inalenga kuboresha huduma ya umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Aidha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo muhimu.
Katika maagizo yake, ameitaka TANESCO kuongeza usimamizi kwa wakandarasi katika kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa wakati, na kusimamia ubora wa kazi ili kuepuka ongezeko la gharama zitokanazo na ucheleweshaji.
Kwa upande wake, Mhandisi Abdallah Chikoyo, Meneja wa Miradi ya Kuzalisha Umeme TANESCO aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji , ameahidi kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi na kuweka mipango kazi inayotekelezeka kwa wakati.
“Tumejipanga kuongeza nguvu katika usimamizi wa miradi hii, na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi, tukitimiza wajibu wetu katika kuboresha huduma ya umeme nchini,” amesema Mhandisi Chikoyo.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Kamishna Luoga alitembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Mabibo, Kinyerezi na Gongo la Mboto. Katika vituo hivyo, kazi ya ufungaji wa mashine umba zenye uwezo mkubwa (transformers) inaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ikiwa ni hatua ya kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam.