KAPINGA ATAJA VIGEZO VYA ZIADA UPELEKAJI UMEME VITONGOJINI
habari*📌 Lengo ni kuhakikisha kila Jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na umeme*
*📌 Vinahusisha mahitaji ya kiuchumi na Kijamii, ukubwa wa Jimbo na Kitongoji*
*📌 Mkurugenzi Mkuu REA atakiwa kumsimamia kwa karibu Mkandarasi wa miradi ya Vitongoji Ziwa Tanganyika*
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya umeme katika Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada ikiwemo ukubwa wa vitongoji, ukubwa wa Jimbo pamoja na mahitaji ya kiuchumi na kijamii.
Lengo la kuweka vigezo hivyo ni kuhakikisha kuwa kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na nishati ya umeme.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Olesendeka aliyeuliza kwamba Serikali imejipangaje kutekeleza miradi ya Vitongoji kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro ambapo umbali kutoka Kitongoji kimoja hadi kingine ni zaidi ya kilometa kumi.
"Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza miradi hii ya Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada, tumeangalia ukubwa wa jimbo husika, ukubwa wa Vitongoji na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika. Niwahakikishie Wabunge mtaona utofauti katika miradi hii tunayoitekeleza hivi sasa." Amesema Kapinga
Akijibu swali la Mbunge wa Nyasa Mhe. Stella Manyanya aliyeuliza kuhusu kitongoji cha Songea Pori kilichopo katika Kijiji cha Lunyele na Kitongoji cha Nindi kilichopo Kijiji cha Konganywita kufikishiwa nishati ya umeme, Mhe. Kapinga amesema Vitongoji hivyo vimefanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika vinahitaji njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kati kwa umbali wa kilometa tatu.
Amesema Serikali inatarajia kuvipelekea umeme vitongoji hivyo kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB) ambao utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2025/2026.
Kuhusiana na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme katika Jimbo la Nyasa Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imeshakutana na Mkandarasa na kumuagiza kuweka Wakandarasi wadogo (sub contractors) katika miradi yake anayotekeleza.
Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kauli ya Serikali kuhusu kusuasua kwa Mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika, Mhe. Kapinga amesema katika utekelezaji wa miradi ya Vitongoji Serikali imehakikisha inawapata wakandarasi wenye weledi.
Kuhusu Wakandarasi ambao wanasuasua, Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika.
Aidha, amemuagiza kuchukua hatua za ziada kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa weledi.
REA YAHAMASISHA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA MIRADI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
habariWADAU WAJADILI MPANGO MAHSUSI WA NISHATI KATIKA WIKI YA NISHATI JADIDIFU
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ameongoza wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa Nishati wa Misheni 300.
Mjadala huo umefanyika katika Wiki ya Nishati Jadidifu 2025 inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Masuala mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo namna ya kuvutia na kushirikisha wawekezaji kutoka sekta binafsi na taasisi za kifedha, ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Mpango Mahsusi wa Nishati ikiwemo kuhakikisha asilimia 75 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
WAZIRI MKUU MAJALIWA AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA JAPAN
_▪️Asema Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania_
_▪️Aagiza tathmini ya barabara za Kibiti-Lindi na Morogoro-Dodoma_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.
Amekutana na kiongozi huyo leo (Alhamisi, Mei 29, 2025) katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan, ambapo Mheshimiwa Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Amesema Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.