MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA HATIFUNGANI -MABAYANI

May 13, 2025 Add Comment


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA) inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira awamu ya tatu kupitia ufadhili wa Hatifungani ya Kijani (TANGA WATER GREEN BOND).


 Ambapo kwa sasa kazi ya uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba makubwa yenye kipenyo cha 600mm yanayolazwa kwa urefu wa kilomita 6 kutoka katika Mtambo wa kusukuma maji Mabayani kuelekea katika Kituo cha kuzalisha maji Mowe imekwishaanza na utekelezaji wake umefikia asilimia 20.

Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi Mzawa S.T.C Construction company Limited ambapo lengo kuu ni kuongeza uwezo wa kusukuma maji kutoka lita Milioni 42 zilizopo sasa hadi kufikia lita Milioni 60 ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na ya uhakika kwa wakazi ya Jiji la Tanga pamoja na Miji ya Muheza na Mkinga.



ULEGA AVUNJA MKATABA WA MKANDARASI MZEMBE

May 13, 2025 Add Comment

 



Na Mwandishi Wetu, Tanga

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara Mkoani Tanga baada ya Mkandarasi kutoka China kushindwa kutimiza masharti ya mkataba. 

Mkandarasi huyo, kampuni ya China Railway 15 Bureua Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja - Mkange (km 95.2) wilayani Pangani anadaiwa kushindwa kufanya kazi aliyotakiwa kuifanya kwa wakati ingawa tayari amelipwa fedha yote na serikali. 

Baada ya kuvunja mkataba wa awali, Waziri Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kuondoa kilometa 25 za barabara hiyo ambazo hajazifanyiwa kazi na badala yake itangazwe zabuni mpya ili wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo wapewe kazi na waanze haraka. 

Kufuatia agizo hilo, sasa kilometa 25 za barabara hiyo na kilometa 70 za barabara inayoanzia Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) zitaunganishwa kwenye zabuni ili apatikane Mkandarasi wa kuijenga.

Ulega ametoa maelekezo hayo leo Mei 12, 2025 kwenye ziara yake Mkoani Tanga ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ambayo Serikali imekwishamlipa Mkandarasi kiasi cha shilingi Bilioni 47 ingawa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 48 tu.

“Mkandarasi huyu ametuangusha na hapa sisi hadai hata senti kwani tushamlipa zaidi ya bilioni 40, yupo nyuma ya muda, vifaa hajavileta vyote, wafanyakazi hawajawaleta wote, hivyo nimechukua maamuzi ya kumnyang’anya sehemu ya kazi ya mradi ili mradi huu ukamilike kwani ni wa muda mrefu na ni kilio cha wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kiujumla”, amesisitiza Ulega.

Ulega ameendelea kusisitiza kuwa maamuzi hayo ya kumyang’anya mkandarasi sehemu ya kazi ni kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi kwasababu Serikali ingeamua kuvunja mkataba wote ingechukua zaidi ya miezi 6 hadi mwaka mzima mpaka Mkandarasi mpya aanze kazi na hasara yake mradi kuendelea kuchelewa.

Vilevile, Ulega amemtaka Mkandarasi huyo kuilipa fidia Serikali kwa kuchelewesha mradi huo ambapo ameielekeza timu wa wataalam kuendelea kuchambua kimkataba juu ya hatua zitakazochukuliwa. 

Ulega amemwagiza Katibu Mkuu huyo kumweka mkandarasi huyo katika orodha ya Wakandarasi wasiofanya kazi vizuri katika miradi ya ujenzi kwa siku za usoni ili iweze kusadia wakati wa kupata Makandarasi wengine katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.

Kuhusu kilometa 70 ambazo Mkandarasi atatakiwa kuzimalizia, Ulega ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuisimamia kampuni hiyo ya China Railway 15 Bureua Group kufanya kazi usiku na mchana ili azikamilishe kuzijenga kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na ikiwa Wataalamu hao watashindwa kuwasimamia kikamilifu na wao watabadilishwa.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi kutoka TANROADS, Mhandisi Julius Msofe ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 47.82 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 100 na kuongeza kuwa muda wa mkataba wa miezi 36 sawa na asilimia 100 umeisha tangu tarehe 31 Machi 2025.









NAIBU WAZIRI UMMY AZINDUA MIRADI YA KIUCHUMI YA WENYE ULEMAVU

May 13, 2025 Add Comment

Na Mwandishi wetu- Dar es salaam 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amezindua miradi ya kiuchumi ambayo iko chini ya  Shirika lisilo la Kiserikali la Strategic Alternative Learning Technique (SALT), inayohudumiwa na vijana wenye changamoto za ufahamu.

Mhe. Nderiananga alifanya uzinduzi huo Jijini Dar es Salaam kwa miradi ambayo ni pamoja na  Salt Special Supermarket, Mgahawa na Bakery itakayohudumiwa na vijana wenye ulemavu wa ufahamu huku akisema jumla ya vijana na Watoto 83 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma kwa wananchi hatua itakayowasaidia kujipatia kipato chao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Aidha, Mhe. Nderiananga aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, kujiwezesha kiuchumi na kusaidia mashirika yanayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake  ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa fedha kwa watu wenye ulemavu ili wafanye kazi zao vizuri. Nimefurahi kuona Shirika hili la SALT linafanya kazi zake kwa ubunifu kwa kuwafundisha stadi za kazi na ubunifu wa mavazi,” alisema Mhe. Nderiananga.

Vilevile, alifafanua kwamba ikiwa  kila mmoja atafanya kwa nafasi yake katika kuwawezesha watu wenye ulemavu itaongeza chachu kwao kujituma kufanya kazi kwani vipaji na uwezo wao utatambulika na kuungwa mkono hali itakayoongeza uzalishaji katika Nchi.

“Nitoe wito tuendelee kuliunga mkono Shirika hili na mengine yanayowasaidia watu wenye ulemavu wa aina zote kwani yanafanya kazi kubwa hivyo viongozi wetu wa Serikali za Mitaa tuyapokee mashirika haya na kuwapa ushirikiano kwa manufaa ya Taifa letu.

Aidha alibainisha kwamba watu wenye ulemavu wanahitaji fursa bila kunyanyapaliwa huku akiwataka wazazi na walezi kutosikiliza maneno ya kukatisha tamaa na badala yake wawaamini watoto wao kuwa wana uwezo wa kipekee.

Aliwahimiza  wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kutumia fursa za mafunzo yanayotolewa katika taasisi mbalimbali ili kuwajengea Watoto kujiamini kuwa wanaweza na wanamchango katika jamii.

“Baadhi ya mafunzo yanayotolewa na SALT ni pamoja na uokaji, mapishi, mitindo ya mavazi na wahudumu katika migahawa hatua inayowajengea ujuzi wa kujipatia kipato ili kuendesha maisha hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Strategic Alternative Learning Technique (SALT), Bi. Rebeca Lebi alieleza kuwa Shirika hilo lilianza mwaka 2019 kwa lengo la kuwasaidia watoto na vijana wenye changamoto za ufahamu ambazo ni  Usonji (Autistic Spectrum Disoder), Down syndrome, Mtindio wa ubongo (Cerebral Palsy ), Ulemavu wa akili (Intellectual Impairment) , Kifafa kikali (Severe epilepsy) na changamoto zote zinazohusiana na ulemavu wa ubongo na ufahamu.

Awali akisoma risala  Meneja wa Operesheni kutoka Shirika la SALT, Bi. Jasmine Omary Iddy alisema SALT, ilianzisha chuo cha ufundi na uzalishaji (Vocational training and production) ikiwa na malengo ya kumuandaa kijana mwenye changamoto za ulemavu wa ufahamu kuweza kuwa mzalishaji  kupitia mpango wa Viwanda  10 ambavyo vitazalisha bidhaa tofauti, kama vile sabuni za kuogea, shampoo, mafuta ya kupaka, vitambaa vya batiki,  mikate na ufugaji wa samaki, kuku pamoja na bustani za mbogamboga.

“Kituo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwawezesha vijana wenye changamoto za kiakili na ufahamu kupata stadi za kazi, stadi za maisha na mazingira salama ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Lengo letu kuu ni kuwapatia fursa ya kujitegemea, kuongeza thamani katika maisha yao na kupunguza utegemezi kwa familia au jamii,” alieleza Meneja huyo.

MWISHO

SERIKALI KUTEKELEZA MFUKO WA UBUNIFU WA SAMIA “SAMIA INNOVATION FUND” WENYE THAMANI YA BIL 2.3

May 13, 2025 Add Comment
Serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa mfuko wa Ubunifu wa Samia “SAMIA Innovation Fund” wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 utakaotoa mikopo nafuu kwa wabunifu kwa lengo la kuendeleza na kubiasharisha ubunifu pamoja na kutoa fursa za ajira kwa watanzania kupitia kazi za ubunifu.