Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akitoa salaam na heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Hayati Mzee Cleopa David Msuya, Makamu wa Kwanza na Waziri Mkuu Mstaafu, shughuli iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya ibada, iliyofanyika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar Es Salaam, leo Jumapili, tarehe 11 Mei 2025.
KANISA ANGLIKANA LASISITIZA UMUHIMU WA UCHAGUZI MKUU OKTOBA
habariNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akihutubia mara baada kushiriki Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Rev. Canon Jacob William Kahemele iliyofanyika leo Mei 11, 2025 katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, jijini Mbeya.
📌 Askofu Mkuu Maimbo Mmdolwa ahimiza katiba ifuatwe
📌 Dkt. Biteko asema milango ya Serikali iko wazi kwa mazungumzo
📌 Asema Serikali inathamini mchango wa kanisa kwa jamii
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Maimbo Mmdolwa amewahimiza Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na kuongeza kuwa nchi inaweza kuingia katika mgogoro mbaya wa kikatiba kama watasikiliza watu wanaotaka kuahirisha Uchaguzi Mkuu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akihutubia mara baada kushiriki Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Rev. Canon Jacob William Kahemele iliyofanyika leo Mei 11, 2025 katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, jijini Mbeya.
Askofu Mmdolwa amesema hayo Mei 11, 2025 jijini Mbeya katika ibada ya kuwekwa wakfu Canon Jacob William Kahemele kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini - Mbeya ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini - Mbeya, Rev. Canon Jacob William Kahemele mara baada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo leo Mei 11, 2025 katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme - jijini Mbeya.
“ Kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu uko hapa na tuliombe Taifa zima kutoahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa tutaingia katika mtanziko mkubwa na mgogoro wa kikatiba. Kama kuna changamoto zitafutiwe suluhu ziishe,”
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akishiriki Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Rev. Canon Jacob William Kahemele iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme- Mbeya. Kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi na kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe. George Mkuchika. Ibada hiyo imefanyika leo Mei 11, 2025 katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme - jijini Mbeya.
Askofu Mndolwa ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na Taasisi za dini nchini na kuunga mkono Uhuru wa kuabudu ikiwa na lengo la kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Akizungumza mara baada ya ibada hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema milango ya Serikali iko wazi chini ya uongozi wa wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasihi wenye hoja kujongea kwa mazungumzo.
"Ninachoweza kusema kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu unakuwa uhuru na wa haki huku nchi ikiendelea kuwa na amani.
“ Uchaguzi utafanyika kwa uhuru na haki kama katiba inavyotaka, waliposikika waliotaka marekebisho ya sheria Serikali ilipitia na kufanya marekebisho ya sheria zinazosimamia uchaguzi na leo milango ya Rais Mhe. Dkt. Samia ipo wazi kwa yeyote mwenye kutoa malalamiko yake ili nchi iende mbele,” amesema Dkt. Biteko.
Amewaasa Watanzania kuendelea kuiombea nchi ili amani iendelee kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
![]() |
Dkt. Biteko amesema Serikali inathamini mchango wa madhehebu yote ya dini, ikiwemo Kanisa la Anglikana. Katika nyanja za elimu, afya, maji, na maendeleo ya jamii, Serikali inashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi.
Akitoa mfano wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini yenye makanisa 37 yanayosimamiwa na parish katika mikoa ya Songwe na Mbeya kupitia makanisa hayo yanasaidia kufikisha huduma ya kiroho kwa jamii.
![]() |
“ Kuanzia mwaka 2016 hadi 2025 Kanisa kwa kushirikiana na wadau limetumia zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendesha miradi ya “Dreams na Archive” kwa kusaidia Elimu Maalumu ya Vitendo ya kujikomboa Kiuchumi na Afya kwa Mabinti na Watoto wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI katika maeneo ya Mbeya, Songwe na Tunduma,” amesema Dkt. Biteko.
Ambapo miradi hiyo imesaidia zaidi wananchi 160,000 waliokuwa na changamoto hizo za kijamii na kiuchumi. Aidha, imejiri zaidi ya watu 150 hivyo kuwaongezea kipato na kuwarahisishia maisha wananchi.
Pia amesema Serikali itaendelea kushirikiana Kanisa la Anglikana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Dkt. Biteko amempongeza
Askofu Kahemela katika safari yake mpya ya kiutumishi huku akitoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo kumtunza na kumsikiliza Askofu huyo pamoja na kumtia moyo kuwavumilia waumini wake endapo changamoto zitatokea.
“ Tunakupongeza kwa moyo wa kujitoa kwa Mungu, kwa utii wako kwa wito wa kiutumishi, na kwa maono yako ya kiroho.
Serikali inapenda kukupa uhakika kuwa tutaendelea kushirikiana kwa karibu na Dayosisi hii chini ya uongozi wako, kwa lengo la kukuza ustawi wa wananchi wetu, kulinda tunu zetu za taifa, na kuimarisha mshikamano wa kijamii na kitaifa,” amebainisha Dkt. Biteko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mhe. Kapteni mstaafu George Mkuchika amewaomba waumini wa kanisa la hilo kuwa na umoja na mshikano mara baada ya uchaguzi wa Askofu wa Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini na kutii viongozi wa dini ili kuendeleza kazi ya Mungu.
Aidha, amesema Serikali iliyopo ni sikivu na endapo kuna malalamiko yasikilizwe, na kuwa Uchaguzi usitenganishe Watanzania bali uwaaunganishe, pia amewataka watu wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali wafanye hivyo kwa kufuata utaratibu.
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mhashamu Askofu Sospeter Ndenza amesema kuwa Askofu ni Kuhani Mkuu na Mchungaji Mkuu kwa niaba ya Kristo na anasimamia nidhamu ya kanisa na kuona ibada zinasimamiwa na kufuata taratibu za kanisa pamoja na kusimamia utoaji wa huduma za sakrementi tofauti.
Amesema wajibu huo ni mzito unahitaji uongozi na hekima ya Mungu.
“ Jacob unahitaji kumuomba Mungu akupe hekima hasa katika dunia ya leo, leo unapokusidia kuwekwa wakfu unahitaji hekima na adili ili umwakilishe kristo,” amesema Mhashamu Askofu Ndenza.
Amesema Askofu huyo asiogope vitisho kwa kuwa kutakuwa na watu watakao mpinga hata hivyo asitetereke badala yake ajue njia za Mungu na asitumie akili zake bali ajinyenyekeze kwa Mungu naye atamsaidia.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Canon Jacob William Kahemele ameahidi kuwaombea viongozi wa Serikali ili waweze kuiongoza nchi kwa amani na utulivu.
“ Wakati wa uongozi wetu tutahimiza sana watu kusali sana ili kukua kiroho kwa kuwa shetani mjanja sana na anadanganya watu kufuata njia za udanganyifu. Pia tutasisitiza
sana uamsho wa kiroho ili watu wasiwe wachanga na kuyumbishwa huku na huko,” amesema Askofu Kahemele.
Amesema wanaamini wameitwa kufanya majukumu makubwa kwa kutoa ibada, kutenda kazi kwa uaminifu sambamba na kusaidia wenye uhitaji.
Aidha, ametaja baadhi ya changamoto zinazowakumba vijana nchini za matumizi ya pombe kali, sigara na michezo ya kamari hivyo ameiomba Serikali kuzuia uholela wa uuzaji wa pombe kali na sigara.
Licha ya hayo ameipongeza Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati mfano treni ya kisasa (SGR) na kuiomba kufikiria namna ya kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Dar es salaam kwa kutumia treni hiyo ya kisasa ili kusaidia kukuza uchumi wa mkoa huo.
Ibada hiyo ya kumuweka wakfu Canon Jacob William Kahemele kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Mhe. Dkt. Tulia Akson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi
MWISHO
MBUNGE NEEMA LUGANGIRA-AKILI MNEMBA INA TIJA NA FURSA NYINGI IKITUMIKA IPASAVYO
siasaNa Mwandishi Wetu,DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalumu Kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira amesema kwamba akili mnemba (artificial intelligence - AI) ina tija na fursa nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Kilimo na Elimu na nyenginezo hapa nchini.
Aliyasema hayo wakati akizungumza katika Semina ya Akili Mnemba kwa Wabunge Wanawake iliyoandaliwa kwa Ushirikiano na Shirika ambalo alilianzisha la Omuka Hub pamoja na Bunge la Tanzania kupitia Mradi wa Female Al Leaders chini ya Women Political Leaders (WPL) na GIZ unaolenga kuimarisha Utawala Bora wa Akili Mnemba “Artificial Intelligence #Al” kwa kuimarisha Wanawake Wanasiasa barani Afrika ili waweze kuibeba ajenda hiyo na kuwa Vinara.
Alisema katika Semina hiyo wamejadiliana mambo mengi na imeonyesha akili mnemba inafursa nyingi lakini alitoa angalizo pia isipotumika kwa usahihi ina changamoto ikiwemo ukatili wa kijinsia, kurubuni watoto na inaweza kupelekea kufifisha uwezo wa kufikiria kutokana na kutufanya sisi kuwa tegemezi sana.
“Katika semina hii, akili mnemba imetushangaza sisi kama Wabunge sababu niliamua kufanya jaribio la kuiuliza hii AI swali kuwa mimi ni Mbunge na naelekea kwenye uchaguzi, naomba inisaidie kuniandalia mkakati wa kampeni na baada ya dakika chache AI ikanipa mkakati kabambe kwa usahihi hadi mwenyewe unashangaa na inakuwa na uwezo wa muda mfupi wa kupima kila kilicho kwenye mitaandao yote yenye uwezo nayo inakupa picha pana”, Alisema Mbunge Neema Lugangira.
Alisema kwamba Akili Mnemba ni kitu ambacho kina tija lakini tija hiyo ili iweze kupatikana lazima itumike kwa ufasaha na wao kama Wabunge ni kitu ambacho wanakwenda kukiangazia; ni lazima kama Tanzania iwepo sera ya akili mnemba pamoja na sheria ili kama taifa linufaike na faida zake na pia kujikinga na kudhibiti na madhara yanayoweza kupatikana kwenye eneo hilo la akila memba.
Awali akizungumza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (CCM) Jesca Msambatavangu alisema niwaondolee hofu akili mnemba haijaja kupora ajira za watu bali imekuja kuboresha ajira na kukuanzisha ajira na haijaja kumbagua mtu yoyote lakini lazima tutambue dunia ina mambo mazuri na mabaya hayo mambo wanatakiwa kujifunza mambo muhimu hivyo tunashukuru kuletewe semina hii ambavyo tunaamini itakuwa na tija”.
Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Toufiq alisema Bunge linatambua fursa na changamoto za akili mnemba hivyo Bunge wanajipanga kuandaa Sheria za Usimamizi.
Mbunge Fatma ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson kwenye Semina hiyo ya Wabunge Wanawake kuhusu Akili Mnemba “Artificial Intelligence” ambapo alisema kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefurahi kuwa sehemu ya kunufaika na mafunzo ya teknolojia ya akili mnemba.
Mhe Neema Lugangira (MB) ni mwakilishi Afrika wa Women Political Leaders (WPL)amefanikiwa kufanikisha mradi wa Female Al Leaders kuja hapa Tanzania ambapo sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuandaa Semina ya Wabunge Wanawake kwa kushirikiana na Shirika ambalo alilianzisha la Omuka Hub pamoja na Bunge la Tanzania.
MWISHO.