Showing posts with label siasa. Show all posts
Showing posts with label siasa. Show all posts

NLD YAZOA WANACHAMA KUTOKA VYAMA VYA UPINZANI

October 01, 2024 Add Comment

Na Oscar Assenga, TANGA


ZAIDI ya Wanachama 150 kutoka vyama vya ADC na ACT wazalendo wamejiunga na Chama cha NLD  Mariam Sijaona aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ACT Wazalendo na Scola Kahana aliyekuwa mgombea wa nafasi ya makamo mwenyekiti bara kupitia ADC na mgombea ubunge Jimbo la kibaha katika uchaguzi wa 2020.

Idadi hiyo kubwa kujiunga na chama hicho inaonyesha namna wanavyokubalika kutokana na sera zao na hivyo kuendelea kuwaimarisha kuelekea kwenye chaguzi mbalimbali ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule mkuu wa mwaka 2025

Akizungumza wakati akiwapokea wanachama hao wapya Katibu Mkuu wa Chama hicho Doyo Hassan Doyo alisema kwamba kupokelewa kwa idadi hiyo ya wanachama kunaashiria mwelekeo mzuri wa chama hicho ambacho kwa sasa wanatarajia kuanza ziara za kujitambulisha kwa wanachama na kutangaza sera zao nchi nzima .

Aidha alisema ziara hiyo itaanza  Oktoba 30 mwaka huu  ikianzia mkoani Tanga, Pemba,Kanda ya Ziwa na Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambapo watakuwa na mikutano katika maeneo mbalimbali

Doyo, alisema katika zoezi hilo la kupokea wanachama hao wapya wakiwemo  viongozi wengine wa NLD, akiwemo Makamo Mwenyekiti Bara,Khamis Said Hamad ambapo waliwakaribisha wanachama hao wapya na kuwahakikishia kuwa wana haki sawa na wanachama wa chama hicho kwa mujibu wa katiba ya NLD.

Alisema kwamba wanachama hao wameamua kujiunga na Chama cha NLD kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Doyo katika kukuza Demokrasia nchini.

"Tunajua chama chetu kipya hakina ruzuku, lakini tupo tayari kukaa na njaa ili kupigania demokrasia ya kweli na hatimaye chama chetu kufanya vizuri kwenye chaguzi zijazo," walisisitiza wana chama hao.

Doyo aliwasihi wanachama hao wapya kusoma Itikadi ya NLD, akisisitiza kuwa Itikadi ya chama hicho imebeba uzalendo, haki, na maendeleo.


Katika hatua nyengine Chama cha National League for Democracy (NLD) kimewasilisha ombi kwa serikali kuhusu kalenda ya uchaguzi iliyotolewa na Tamisemi ambapo wameiomba  Serikali kuketi na wadau wa Uchaguzi hususani vyama vya Siasa kuona namna wanavyoweza kuongeza muda wa kampeni.

 Doyo alisema  muda uliotolewa kwa maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji ni mfupi sana na kwamba hautoshi.

Alisema kutokana na hilo ni vyema uchaguzi huo  ukasogezwa mbele ili kuongeza muda wa kampeni  ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na ufanisi bila vikwazo,

"Kupewa siku saba hadi siku kumi na nne, siku hizo haziwezi kutosha,wagombea wanahitaji muda mrefu wa kampeni Lakini pia Wananchi wanahitaji muda mrefu wa kuwachuja wagombea wao,hivyo Tunaiomba serikali kupitia Tamisemi isogeze mbele muda wa Uchaguzi, sio kuahirisha uchaguzi, bali kuongeza muda wa maandalizi,"Alisisitiza Doyo



MWISHO


MONGELLA ATOA MAAGIZO MAALUM KWA VIONGOZI CCM

September 10, 2024 Add Comment


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, ametoa maagizo maalum kwa viongozi wa chama hicho, akiwahimiza kuhakikisha kuwa wanachama wanandikishwa kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.


Mongella alitoa maagizo hayo alipomtembelea Balozi wa Shina namba 3, Safina Masanja Kitundu, katika tawi la Buduhe, Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye heshima na nafasi muhimu katika kulinda mustakabali wa nchi. Kwa hivyo, alihimiza kuhakikisha kuwa uandikishaji wa wanachama unafanywa kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kuandikisha wanachama wengi katika jumuiya za UWT, Wazazi, na Vijana, ili kukifanya chama kiwe imara.

Mongella pia alibainisha kuwa siri ya mafanikio ya chama ni kujikita kwenye mashina na kufanya kazi kwa karibu na mabalozi. Ziara yake ya siku saba mkoani Shinyanga inatarajiwa kuhitimishwa baada ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2024 na kuimarisha uhai wa chama.





MONGELA AZUNGUMZA NA VIONGOZI WA CHAMA NA WAZEE KATA YA BULUNGWA, HALMASHAURI YA USHETU

September 08, 2024 Add Comment

 Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella, akizungumza na Viongozi wa chama na Jumuiya ngazi ya Kata na Matawi,mabalozi,Wazee maarufu na viongozi wa Kimila katika kata ya Bulungwa,Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga,leo Septemba 8,2024.


Mongella anaendelea na ziara yake ya siku saba mkoani Shinyanga yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2024, kuimarisha uhai wa chama sambamba na kujitambulisha.










CHAMA HAKITAMBEBA MTU AMBAE YEYE MWENYEWE HAKUJIBEBA -HAPI

September 08, 2024 Add Comment

 


AKIWA katika mkutano na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo uliofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) Mkoani Pwani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya CCM, Ndugu. Ally Salum Hapi *(MNEC) ametuma salamu kwa viongozi wasio wajibika katika nafasi zao walizoaminiwa na wananchi huku akisema Chama cha Mapinduzi hakitambeba mtu katika uchaguzi unaokuja.

"Chama chetu kina utaratibu mzuri sana katika chaguzi muda unapofika na kila muda wa uchaguzi ndiyo maana tunasisitiza suala la kupata wagombea bora tutakao wauza kwa urahisi ambae anakubalika na wananchi na siyo anayekubalika kwenye mifuko ya watu wachache, kiongozi ambaye anazijua shida za wananchi na uchaguzi wa serikali za mitaa ndiyo msingi wa uchaguzi mkuu" alisema Hapi

Kuhusu viongozi wasiowajibika kwenye nafasi zao Hapi alitumia mkutano huo kukumbusha kuwa katika kipindi kilichosalia kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao ni muhimu kwa kila kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kujitathimini iwapo anafaa kurejea katika nafasi yake kwenye uchaguzi ujao, iwapo wananchi watamuunga mkono kutokana na kazi zake.


"Waheshimiwa madiwani naomba mchape kazi muda ndiyo huu chama hakitambeba mtu ambaye hakujibeba yeye mwenyewe kwa utendaji kazi wake, wala hakitambeba mtu anayejisemea mwenyewe ambae hakisemei chama, hamsemei Mbunge wala hamsemei Rais wa CCM ninachoomba mtambue ni kuwa unafika kwenye uchaguzi huchaguliwi wewe kwa sababu ni bingwa wa fitna au wewe ni bingwa wa kumsema vibaya mwenzio au wewe ni bingwa wa kujisemea wewe mwenyewe tu bali matendo yako na namna ulivyoshughulika na matatizo ya wananchi pamoja na kazi unazozifanya kwa hiyo tupeleke wagombea wanaokubalika wenye sifa na wanaojua uongozi na wanajua kuishi na watu, kila mwenye sifa nendeni mkawahamasishe wagombee"alisema


Katika Hatua nyingine Hapi aliwanyooshea kidole na kuwaonya watu wanaojihusisha na udalali kwenye uchaguzi kwa kujifanya wao ndiyo kila kitu juu ya ushindi wa wagombea kwa kuwa wanajua namna ya kuzungumza na wananchi hali hiyo imekuwa mzigo mkubwa kwa viongozi walioko madarakani na kusababisha washindwe kufanya kazi kwa ufasaha.


"Lakini wapo watu hapa ni madalali wa uchaguzi ambao wametengeneza upepo kwa mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi hiyo lazima amuone yeye na akiamini ushindi wa mgombea upo kwenye mikono yake, katika kipindi hiki jiepusheni na madalali wa siasa katika uchaguzi" alisema Hapi




Imetolewa na Idara ya Oganaizesheni ya Jumuiya ya Wazazi Taifa