Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

RAIS STUBB AZINDUA MRADI WA EURO MILIONI 20 WA UHIFADHI WA MISITU – FORLAND

May 16, 2025 Add Comment




Rais wa Jamhuri ya Finland, Mhe. Alexander Stubb, leo amezindua rasmi Mradi wa Kusimamia Uhifadhi wa Misitu, Matumizi Bora ya Ardhi na Kuongeza Thamani ya Mazao ya Misitu (Forestry, Land Use, and Value Chains Development in Tanzania – FORLAND), wenye thamani ya Euro milioni 20.

Mradi huo unalenga kukuza kanuni endelevu za uhifadhi wa misitu, kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania, pamoja na kuendeleza usimamizi wa misitu katika jamii, upandaji miti, na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Mei 16, 2025 katika Bustani ya Botanical Garden jijini Dar es Salaam, Rais Stubb ameshiriki katika zoezi la upandaji miti na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Finland katika sekta ya misitu.







“Nina imani mti nilioupanda utakua kama yalivyo mashirikiano kati ya nchi zetu katika sekta ya misitu, hususan kupitia mradi huu wa FORLAND,” amesema Rais Stubb.

Aidha, Rais Stubb ameeleza kuwa Finland ina misitu inayochukua asilimia 70 ya eneo la nchi hiyo, na kwamba bidhaa zake za misitu zinatambulika kwa ubora na uimara wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), amesema kuwa mradi wa FORLAND unatekelezwa katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii zinazozunguka misitu hiyo.


“Nchi yako (Finland) imekuwa mshirika muhimu kwa Tanzania katika sekta ya misitu, ikiwa imesaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile Mpango wa Usimamizi wa Eneo la Hifadhi ya Usambara Mashariki (1988–2002), vyuo vya misitu nchini Malawi, Tanzania na Zambia (1999–2005), Programu ya Kitaifa ya Misitu (2005–2010), pamoja na Biashara ya Kibinafsi ya Misitu na Kaboni (2010–2011),” amesema Mhe. Chana.

Ameongeza kuwa Finland pia imeisaidia Tanzania kupitia Programu za Kitaifa za Misitu na Nyuki (2013–2016), pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali za Misitu (NAFORMA) tangu mwaka 2009.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na wanadiplomasia na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania na Finland.



WAZIRI AWESO ACHAGULIWA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAWAZIRI WA ZAMCOM 2025/2026

May 16, 2025 Add Comment


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia Mhe  Caesar Chacha Waitara, amemwakilisha Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb), Waziri wa Maji katika Mkutano wa 12 wa Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zambezi Watercourse Commission-ZAMCOM) uliofanyika tarehe 15 Mei 2025 jijini Windhoek, Namibia.

Katika mkutano huo wa ZAMCOM unaojumuisha nchi nane za Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa ZAMCOM katika kipindi cha mwaka 2025/2026.





Serikali Kuanza Kutambua Wanafunzi Kila Hatua Kupitia Mfumo Mpya

May 15, 2025 Add Comment

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatarajia kuanzisha mfumo shirikishi wa tafiti za elimu ili kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na usimamizi wa takwimu ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wadau wa elimu.

Mke wa Rais Finland Afanya “Royal Tour” Makumbusho ya Taifa Dar

May 15, 2025 Add Comment

Na Mwandishi Wetu

Mke wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb, leo Jumanne Mei 14, 2025, amefanya “Royal Tour” kwenye Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine alifurahia sana historia ya zamadam na utamaduni wa Tanzania.

CCM TANGA KUSHIRIKIANA NA TFF KUBADILISHA MUONEKANO WA UWANJA WA CCM MKWAKWANI

May 15, 2025 Add Comment

 






Na Oscar Assenga,TANGA

KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga wamefanya ziara maalumu ya ukaguzi wa uwanja wa CCM Mkwakwani ambao umefanyiwa maboresho makubwa na hivyo unaweza kutumika kwenye mchezo wa nusu fainali wa CRDB Federation Cup kati ya timu ya Yanga na JKT.

Akizungumza mara baada ya kuutembelea uwanja huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman alisema kwamba uwanja huo kutokana na maboresho makubwa upo tayari kwa ajili ya mchezo huo utacheza Mei 18 mwaka huu.

Alisema kwamba walifanya maboresho makubwa ya uwanja huo sehemu ya kuchezea ambayo ilikuwa na changamoto awali kwa jitihada walizifanya viongozi kwa kushirikiana na TFF kupitia Rais Karia waliwaunga mkono CCM kwa jitihada za kufanya ukarabati wa uwanja wao na TFF kugharamia majani sasa mambo yapo vizuri.

Aidha alisema lakini matarajio yao kwa kushirikiana na TFF wameshaandaa michoro namna ya kuubadilisha muonekano wa uwanja huo uwanja wa Mkwakwani kwa kuweka viti na kutengeneza jukwaa la kisasa.

“Lakini pamoja na hilo pia tutabadilisha muonekano wa vyumba vya kubadilisha nguo,vyoo nk na sasa hivi tumeshakamilisha michoro na tupo kwenye mchakato wa kutafuta wadau ili waweze kutuunga mkono

Hata hivyo alisema kwamba mchezo wa Nusu Fainali hiyo kuchezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani Jijini Tanga ni heshima kubwa kwao na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo.

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wapenzi wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuweza kuipa sapoti nusu fainali hiyo .

Mwisho.