Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts
WAGANGA WAFAWIDHI NCHINI NA WATUMISHI NDANI YA SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WAWEKEZAJI

WAGANGA WAFAWIDHI NCHINI NA WATUMISHI NDANI YA SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WAWEKEZAJI

March 28, 2024 Add Comment




NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.



NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,akisisitiza jambo wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.


BAADHI ya Washiriki wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel,wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.


NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela,akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika kwa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi Jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imewataka waganga wafawidhi nchini na Watumishi ndani ya Sekta ya Afya kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ikiwemo uanzishaji wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ulioshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki na kuchangia mada zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo.

“Sekta binafsi imesaidia kwa kiwango kikubwa kuipunguzia Serikali mzigo hasa upande wa ajira kwani vijana wengi wameajiriwa kupitia sekta binafsi, hali ambayo sio rahisi kuiachia mzigo serikali pekee.”amesema Dkt.Mollel

Aidha Dkt. Mollel amewaasa Wakurugenzi wa OR- TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuhakikisha vinapata vituo hivyo mapema iwezekanavyo.

“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mambo mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja, nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati”, amesema Mollel

“Tunataka tutakapokutana tena katika mkutano wa mwaka 2026 tutazungumza masula mengine kama kuajiri watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuongezwa” amesisitiza Mollel.

Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.

“Sekta ya Afya ni moja na kazi nyingi za afya zinaanzia katika ngazi ya msingi na dada yangu Dkt. Grace amesisitiza hapa hakuna huduma za afya bila msingi kwani huduma zote zinaanzia huko kwa wananchi walio wengi ndipo wanaanzia kabla ya kuja huku juu kupatiwa huduma,” amesema.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela amesema kuwa kupitia mkutano huo mapendekezo mbalimbali yameweza kutolewa kupitia majadiliano yaliyofanyika ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa huduma za afya ya msingi.

“Mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti za afya za mifumo ya bima na jambo hili limesisitizwa kwa ukubwa na wakashauri vyanzo mbalimbali viweze kutumika ikiwemo kuwashirikisha wadau kama Wizara ya Fedha,”amesema.

Amesema pendekezo lingine lililotolewa ni kwa wadau pamoja na Serikali ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ya msingi kwenye rasilimali watu na vifaa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora.

SHILINGI TRILIONI 1.4 KUTUMIKA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MALARIA, UKIMWI NA KIFUA KIKUU

March 21, 2024 Add Comment

 Na WAF- Dodoma

Serikali ya Tanzania imepokea jumla ya dola za kimarekani milioni 602 sawa na trilioni 1.4 za kitanzania kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2026.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa mkakati wa utekelezaji wa fedha hizo kupitia mradi mpya wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa saba.

Dkt. Jingu amesema fedha zilizopokelewa zimetokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya ili ziweze kuwafikia wananchi katika maeneo yao bila kikwazo.

“Mkutano huu umeandaliwa kwa wakati muafaka ili uwe chachu ya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakua na ufanisi uliokusudiwa huku lengo letu ni kuangalia na kufanyia kazi mambo muhimu tuliyojiwekea kwenye mikakati itakayoongoza utekelezaji wa mradi huu katika kipindi chote cha utekelezaji”. Amesema Dkt. Jingu

Aidha, Dkt. Jingu amefafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kutenga rasilimali zinazotumika kugharamia utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya hivyo ameushukuru mfuko wa dunia kuweza kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua zilizopangwa. 

“Tunatakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji na kuongeza uwajibikaji kwa lengo la kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya nchini. Ili kufikia malengo haya, wote tunao wajibu wa kusimamia na kutekeleza ipasavyo mipango tuliyojiwekea na kuwezesha shughuli zote za mradi ambazo zimepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2024-2026 zinakamilika kwa asilimia mia moja”. Amesisitiza Dkt. Jingu.

Akitoa salamu za Serikali ya Marekani, Mwakilishi wa Serikali ya Marekani Dkt. Etruda Temba, ameishukuru Serikali kwa kuandaa mkutano huo na kusema wadau wa Maendeleo wanatambua mchango wa Serikali  huku akitoa angalizo wakati wa utekelezaji kuepuka ubadhirifu wa fedha ili kupata matokeo yaliyokusudiwa.

Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Subisya Kabuje, amesema Wizara yao imekuwa mnufaika mkubwa wa fedha za Mfuko wa Dunia ambapo katika kipindi cha awamu ya sita TAMISEMI ilipokea shilingi Bilioni 39.9 zilizofanikisha ukamilishaji wa mfumo wa taarifa za afya wa GoTHOMIS ambao umekuwa kichocheo kikubwa katika kusimamia huduma za afya kwenye ngazi za Mikoa na Vituo vya afya.

Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua Mkutano huo, Maganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, amesema ni lazima nchi kujipanga kufikia malengo ya dunia namba tatu lakini pia kukamilisha lengo kwenye sekta ya Afya mkakati wa tano, ili ifikapo 2026 nchi iweze kujipima kikamilifu mafanikio iliyopata.






MADEREVA WA MABUS YAENDAYO MIKOANI WAPATIWA HUDUMA YA UPIMAJI MACHO

March 15, 2024 Add Comment


Na Mwamvua Mwinyi,MBEZI Machi 15

Hii ni wiki ya maadhimisho ya Ugonjwa wa Shinikizo la macho au Presha ya Macho duniani ambapo hospitali ya CCBRT,kwa kushirikiana na hospitali ya Barrack PolisI Kilwa Road na halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, wameadhimisha kwa kutoa huduma ya upimaji macho kwa madereva wa mabasi yaendayo mikoani kwa lengo la kunusuru uoni wa macho yao kutokana na kazi muhimu wanayoifanya.

Pia huduma hii inatolewa kwa mtu yoyote anayefika kituoni hapo ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo la wiki moja tarehe 12.3.2024 zaidi ya watu 400 walikuwa wamepatiwa huduma.

Ugonjwa wa presha ya macho unatajwa na wataalamu wa afya ya macho duniani kuwa wa kwanza kusababisha upofu usiotibika duniani.





WANAUME ZAIDI YA 1000 WAPASULIWA UGONJWA WA MABUSHA DAR

March 12, 2024 Add Comment

 

Na Andrew Chale,DAR.

WANAUME zaidi ya 1000 Mkoa wa Dar es Salaam, wamefanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa mabusha (Ngilimaji) kwenye kambi maalum iliyoendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Wadau, mwishoni mwa mwaka 2023.


Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Dkt. Mohammed Mang’una wakati wa taarifa kwa Umma iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu  juu ya matokeo ya tathimini ya hali ya kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha nchini hususani mkoani Dar es Salaam.

Dkt. Mohamed Mang’una amesema mkoa wa Dar es Salaam, watu wamekuwa wakipata ugonjwa huo wa matende na mabusha kutokana na hali ya kimaisha ikiwemo kuhamahama, kutokakuwa na elimu sahihi na hali ya kimazingira.


"Takwimu za waliofanyiwa upasuaji wa ugonjwa mabusha ama ngilimaji mwishoni mwa mwaka jana katika kambi tulivuka lengo kwa kuwafanyia upasuaji wanaume zaidi ya 1000.


Upasuaji huu ni mkubwa kwani ulivuka lego lile tulilojiwekea, Lakini pia tunaendelea na zoezi la kutoa elimu ilikuweza kuwafikia watu wote  Dar es Salaam." Amesema Dkt . Mohamed Mang'una.


Awali,  Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa kwa umma na kueleza kuwa, watu zaidi Milioni 3.7 wameweza kuwaepusha na hatari ya kupata maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huo wa matende na mabusha.


"Katika tathimini hizo, ni faraja kwetu kuona kuwa tumefanikiwa kuwanusuru wananchi zaidi ya Milioni 3.7 kuepuka na ugonjwa huu matende na mabusha mkoa wa Dar es Salaam.

Nipende kumshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, ambapo mwaka jana aliahidi kutoa kiasi cha Dola za kimarekani milioni tatu, katika kipindi cha 2024 ilikufanikisha juhudi za kutokomeza magonjwa hayo.’’ Amesema Waziri Ummy Mwalimu.


Aidha, imeelezwa na wataalamu kuwa, chanzo kikubwa  cha matende na mabusha ni vimelea vya minyoo midogomidogo jamii ya Filaria, mtu akipata minyoo hiyo inaenda kwenye damu na inaweza kusababisha madhara sehemu za haja ndogo na baadae inaweza kusababisha maji kujikusanya kwenye sehemu za korodani.


Ambapo, maji yakizidi ndio unakuta sehemu hizo za siri zinavimba na baadaye hadi ngozi inaweza kuaathiri na kuweka ugumu wakati inapitakiwa kupatiwa matibabu.


Pia sababu nyingine ya magonjwa hayo ni mbu ambao ndio wanaeneza hiyo minyoo, ni sehemu zote Nchini lakini zaidi wanapatikana sehemu za Pwani kutokana na hali ya kimazingira, Wakati tafiti zinaanza waligundua mbu aina ya Culex, hiyo ilibainishwa na wataalam wanaoangalia tabia za mbu na wadudu lakini baadaye ikabainika kuwa ni mbu wa aina zote wanaweza kusambaza vimelea vya minyoo midogomidogo vinavyosababisha matende na mabusha. Hata mbu anayeeneza Malaria anaweza kusambaza vimelea hivyo vya matende na Mabusha.


"Jamii ifanye bidii ya kuzuia mbu kama vile kusafisha mazingira yanayomzunguka, kufukia madimbwi ya maji, kutumia vyandarua, inamaanisha unapojikinga na mbu hujikingi na Malaria peke yake, bali unajikinga dhidi ya Homa ya Denge, Matende na Mabusha na vingine vingi."  Imebainisa taarifa hiyo ya kitaalamu.

NHIF YABORESHA KITITA CHA MAFAO,YAONGEZA HUDUMA 247

February 29, 2024 Add Comment



Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bernard Konga akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Maboresho ya Kitita cha Mafao jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bernard Konga akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Maboresho ya Kitita cha Mafao jijini Dar es Salaam.



*Kitita cha Mafao chenye maboresho kuanza Machi Mosi


Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
MFUKO wa Taifa wa bima ya Afya NHIF umesema imefanya maboresho ya kitita cha mafao kwa wanachama wake pamoja kuangalia madai yaliyokuwapo kwa madaktari ikiwa ni kutaka wanachama wanapata huduma bora na Mfuko kuwa na uendelevu.


Katika maboresho hayo wanachama watapata huduma za kibingwa bobezi kuanzia ngazi ya Hospitali za kanda.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga amesema kitita cha mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zimetolewa kwa wanufaika na bei zake nchini huku kitita hicho kikabaki vilevile bila kuongeza fedha nyingine .


Amesema maboresho ya mwisho ya kitita cha mafao hayo kimezingatia maoni ya wadau na kuweka milango kuendelea kuboresha lengo ni wanachama wasipate usumbufu.


Hata hivyo amesema kuwa katika maboresho wameongeza ulinzi wa mfuko katika kudhibiti mianya ya udanganyifu juu ya kupata huduma wasio wanachama.


“Ni miaka Nane sasa tangu maboresho ya hiki kitita cha mafao kinachotumika kufanyika hivyo ni muhimu wa kufanya marejeo kutokana na mahitaji ya sasa.


"Umuhimu wa kufanya marejeo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo kwenye kitita cha mafao”,amesema Konga.


Amesema wanachama wanaotumia dawa za shinikizo la damu na sukari sasa wanaweza kupata huduma kuanzia ngazi ya chini huku wanachama wanaopata huduma ya uchujaji damu gharama zikiwa zimepunguzwa.


“Huduma za kibigwa na bingwa bobezi kama matibabu ya Moyo,Saratani na Figo sasa zinaweza kutolewa kuanzia ngazi ya kanda na sio lazima mwanachama kwenda ngazi ya Taifa”,Amesema.


Aidha ameongeza kuwa changamoto ya ukosefu wa dawa sasa imeisha kwani dawa mpya zaidi ya 247 zimeongezwa kwenye kitita kwenye maboresho yaliyofanyika.


Konga amesema maeneo yaliyofanyiwa maboresho ili kuleta unafuu ni gharama za usajili na ushauri wa daktari huduma za dawa na tiba za upasuaji na vipimo huku akisisitiza kuwa gharama za maboresho hayo hazimgusi mwanachama bali kati ya NHIF na mtoa huduma.


Amesema maboresho ya kitita hicho yanatarajia kuanza rasmi Marchi Mosi,2024 huku mfuko huo unaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu maboresho zaidi ya kitita hicho.