Na Oscar Assenga, TANGA
Programu ya Tanga Yetu imeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana na watoto wa Jiji la Tanga, kupitia miradi inayolenga kuimarisha elimu, ujuzi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Afisa Mawasiliano wa Programu ya Tanga Yetu, Cliford Sangai, alisema programu hiyo inayofadhiliwa na Foundation Botnar na kutekelezwa na Kampuni ya Innovate kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga, imeshiriki maonyesho hayo kuonyesha matokeo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa jijini humo.
Alisema Tanga Yetu inatekeleza zaidi ya miradi 15 katika maeneo ya elimu, teknolojia na ubunifu, ikiwa na lengo la kuhakikisha watoto na vijana wanapata fursa za kukuza uwezo wao na kutumia maarifa kutatua changamoto zinazowakabili.
“Tumekuja kwenye wiki hii kuonyesha namna ambavyo Tanga Yetu imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali katika elimu, ujuzi na ubunifu, pamoja na kuonyesha bidhaa na suluhisho zinazotokana na mawazo ya vijana wa Tanga,” alisema Sangai.
Kwa mujibu wa Sangai, baadhi ya miradi inayotekelezwa inalenga kukabiliana na changamoto ya watoto katika kujifunza kusoma na kuandika, huku matokeo ya mradi huo yakitumika katika kutengeneza mpango wa Kitaifa wa KKK.
Alisema programu hiyo pia imejikita katika kuwawezesha vijana kutumia vipaji na ujuzi wao katika teknolojia na ubunifu, akisisitiza kuwa vijana wa Tanga wana uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa zinazoweza kutatua changamoto za jamii na hata kufikia soko la kitaifa.
“Vitu ambavyo tunaona vinafanyika katika miji mingine vinafanyika pia Tanga. Vijana wetu wamekuja na bidhaa walizobuni na kuzitengeneza wenyewe, jambo linaloonyesha uwezo mkubwa walionao,” alisema.
Vijana wapelekwa kwenye uchumi wa kidijitali
Sangai alisema katika eneo la ujuzi, Tanga Yetu imekuwa ikiwawezesha vijana kupata mafunzo mbalimbali yanayowaongezea uwezo wa kujiajiri na kuzalisha kipato kupitia teknolojia.
Alitaja baadhi ya mafunzo hayo kuwa ni Graphic Design, uchapishaji wa mabango na T-shirt, utengenezaji wa maudhui ya kidijitali (Content Creation), usimamizi wa mitandao ya kijamii (Social Media Management) pamoja na ujuzi mwingine wa kidijitali.
Alisema vijana wanaotembelea banda la Tanga Yetu katika maonyesho hayo wanaweza kuona miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo ya elimu, ujuzi na ubunifu, pamoja na namna inavyowasaidia vijana wa Tanga kujenga uwezo na kutengeneza fursa.
Ubunifu watatua changamoto za jamii
Sangai alisema Tanga Yetu pia imeanzisha Mfuko wa Ubunifu wa Tanga Yetu, ambao umewezesha vijana wanane kupata ufadhili wa kujaribu mawazo yao ya kibunifu yenye lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii ya Jiji la Tanga.
Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni mfumo unaolenga kuwasaidia wavuvi kufahamu maeneo yenye samaki pamoja na kufuatilia usalama wa vyombo vyao wanapokuwa baharini.
“Tumeshazoea wavuvi kuamka usiku na kwenda kuvua bila kujua samaki wapo wapi. Vijana wamekuja na mfumo unaoweza kumsaidia mvuvi kufahamu eneo ambalo samaki wapo na kwenda kuvua kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa mfumo huo pia unafuatilia mwenendo wa chombo cha uvuvi, hivyo iwapo kitatokea ajali baharini, watu waliopo nchi kavu wanaweza kufahamu eneo ambalo chombo hicho kimepata tatizo na kuchukua hatua kwa haraka.
Sangai alisema hatua hiyo inaonyesha namna ubunifu unavyoweza kutumika kama nyenzo ya kutatua changamoto zinazolikabili Jiji la Tanga na Taifa kwa ujumla.
Vijana 300 wanufaika na mafunzo ya kidijitali
Kwa upande wake, Zainabu Msuya, mnufaika wa Mradi wa Kidijitali unaosimamiwa na Swahili Digital chini ya Programu ya Tanga Yetu, alisema amepata fursa ya kujifunza ujuzi mbalimbali wa teknolojia na sasa anaweza kutumia maarifa hayo kujiajiri na kuwawezesha vijana wengine.
Alisema mradi huo unatoa mafunzo katika maeneo ya Graphic Design, Artificial Intelligence (AI), Content Creation, Social Media Management na ujuzi wa kidijitali kwa ujumla.
Msuya alisema yeye ni mmoja wa wanufaika wa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo na baadaye alipata nafasi ya kuwa mmoja wa wasimamizi katika awamu zilizofuata.
“Mradi huu umeweza kuwawezesha vijana wengi. Kwa awamu zilizofuata tulihusisha vijana 100 kwa kila awamu, na kwa ujumla vijana 300 wamepata mafunzo kupitia programu hii,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yamewasaidia vijana kuongeza uelewa wa teknolojia na kupata uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kujenga fursa za kiuchumi.
Mitandao ya kijamii kuwa chanzo cha kipato
Naye Swahibu Bilal, msimamizi wa mradi wa kidijitali, alisema programu hiyo imekuwa ikiwafundisha vijana namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi na kuitumia kama nyenzo ya kutengeneza kipato.
Alisema awali vijana wengi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kibiashara, lakini kupitia mafunzo hayo wameweza kujifunza namna ya kusimamia akaunti, kutengeneza maudhui na kutumia majukwaa hayo kukuza shughuli zao.
“Vijana wengi awali walikuwa hawaelewi namna ya kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza kipato, lakini kupitia mafunzo haya sasa wanaweza kufanya mambo mbalimbali na kutumia ujuzi huo kujenga fursa zao,” alisema Bilal.
Programu ya Tanga Yetu inaendelea kushirikisha vijana katika elimu, ujuzi, teknolojia na ubunifu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwaandaa kutumia maarifa na vipaji vyao katika kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya Jiji la Tanga na Taifa kwa ujumla.
EmoticonEmoticon