TRAMEPRO YATAKA TIBA ASILIA, UTAFITI NA UHIFADHI WA MAZINGIRA KUINGIZWA KWENYE AJENDA YA AFYA AFRIKA

Kajunason August 18, 2026

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limezitaka Serikali za Afrika kuingiza tiba asilia, utafiti wa kisayansi na uhifadhi wa mazingira katika ajenda ya afya ya bara hilo, likisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga mifumo ya afya yenye kujitegemea, salama na endelevu.

Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Nne wa Eastern Africa Regional Ministerial Steering Committee (ReSCo) unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 18 hadi 19, 2026, unaowakutanisha Mawaziri na viongozi wa afya kutoka Nchi Wanachama 14 za Umoja wa Afrika katika Kanda ya Afrika Mashariki, pamoja na wataalamu na wadau wa sekta ya afya chini ya uratibu wa Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC).

TRAMEPRO imempongeza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kwa kushiriki katika mkutano huo, ikisema Tanzania kuwa mwenyeji wa jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za afya zinazovuka mipaka. Shirika hilo limeeleza kuwa ReSCo ni jukwaa muhimu la kisiasa na kitaalamu linalolenga kuimarisha usalama wa afya, ufuatiliaji wa magonjwa, maandalizi na mwitikio wa milipuko pamoja na ustahimilivu wa mifumo ya afya katika Afrika Mashariki.

Kuhusu tiba asilia, TRAMEPRO imesema mjadala wa kujenga afya endelevu na uhuru wa kiafya wa Afrika unapaswa kuzingatia rasilimali na maarifa ya jadi ambayo yamekuwa sehemu ya maisha ya jamii kwa vizazi. Hata hivyo, imeonya kuwa tiba asilia haipaswi kutumiwa bila kuzingatia usalama, ubora na ushahidi wa kisayansi, bali inapaswa kufanyiwa utafiti, kuthibitishwa inapowezekana na kudhibitiwa kwa mujibu wa viwango na maadili ya kitaaluma.

Shirika hilo limependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa tiba asilia, madaktari, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, Serikali, mamlaka za udhibiti, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha bidhaa na maarifa yanayotokana na tiba asilia yanatumika kwa usalama na manufaa ya wananchi.

Katika eneo la afya ya mama, mtoto na vijana, TRAMEPRO imetaka kuongezwa kwa tafiti zinazoweza kubaini manufaa, hatari na mwingiliano wa tiba asilia na dawa nyingine. Imesisitiza kuwa afya ya makundi hayo inapaswa kulindwa dhidi ya matumizi yasiyo salama ya tiba au bidhaa yoyote, bila kujali chanzo chake.

Aidha, TRAMEPRO imeitaka Afrika kuongeza uwekezaji katika utafiti wa mimea dawa, maliasili na maarifa ya jadi ili kuongeza uwezo wa kuzalisha bidhaa za afya zenye usalama, ubora na ufanisi unaoweza kuthibitishwa. Kwa mujibu wa shirika hilo, hatua hiyo inaweza kupunguza utegemezi wa bidhaa na maarifa kutoka nje, kuongeza ajira na kuifanya Afrika kuwa mzalishaji wa maarifa, teknolojia na bidhaa za afya.

Kwa upande wa mazingira, TRAMEPRO imesisitiza kuwa afya ya binadamu haiwezi kutenganishwa na afya ya mazingira, kwa kuwa misitu, maji, udongo, hewa, mimea dawa na viumbe hai ni sehemu muhimu ya mfumo wa uhai. Limeonya kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kuathiri afya za jamii, kupunguza upatikanaji wa rasilimali za tiba asilia na kuhatarisha urithi wa maarifa ya jadi.

Kutokana na hali hiyo, shirika hilo limehimiza kuimarishwa kwa mtazamo wa One Health, unaotambua uhusiano wa karibu kati ya afya ya binadamu, wanyama na mazingira. Pia limezitaka Serikali, Africa CDC, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika utafiti, ubunifu na udhibiti wa bidhaa za tiba asilia.

TRAMEPRO imependekeza pia kuwepo kwa ushirikiano wa kikanda katika utafiti, ubunifu, uzalishaji na udhibiti wa bidhaa za tiba zinazotokana na maliasili za Afrika, sambamba na kulinda mazingira yanayohifadhi rasilimali hizo na kuheshimu haki za jamii zinazomiliki maarifa ya jadi.

Shirika hilo limesema Afrika yenye afya, salama na inayojitegemea inahitaji kuunganisha nguvu za sayansi ya kisasa, teknolojia, utafiti, maarifa ya jamii, tiba asilia na uhifadhi wa mazingira, likisisitiza kuwa mkutano wa ReSCo ni fursa muhimu ya kujenga mifumo ya afya inayoweka usalama wa mgonjwa, ushahidi wa kisayansi, ubora, uwajibikaji na uendelevu katika msingi wa ajenda ya afya ya bara.

“Hakuna afya endelevu bila mazingira salama; na hakuna afya ya Afrika inayojitegemea bila kuwekeza katika sayansi, utafiti, maarifa na rasilimali zake,” TRAMEPRO imesema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »