TBS YAWAFUNGULIA WAJASIRIAMALI NJIA YA MASOKO KUPITIA UBORA WA BIDHAA

August 09, 2026
Wajasiriamali na wananchi wanaoshiriki Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini wamepata elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango, kuthibitisha bidhaa na kutumia Alama ya Ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua inayolenga kuongeza uaminifu wa bidhaa na kufungua fursa zaidi za masoko ndani na nje ya nchi.

Elimu hiyo imetolewa na TBS Kanda ya Kusini kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi, ambapo wananchi na wajasiriamali wamepata fursa ya kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu viwango, ubora na taratibu za uthibitishaji wa bidhaa.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TBS Kanda ya Kusini, Abel Mwakasonda, amesema ushiriki wa shirika hilo ni sehemu ya juhudi za kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu itakayowawezesha kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika masoko.

Amesema TBS imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha wazalishaji, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, wanaelewa umuhimu wa kuthibitisha bidhaa zao na kupata Alama ya Ubora, ambayo ni muhimu katika kujenga imani ya mlaji.

“Tunawakaribisha wajasiriamali na Watanzania kwa ujumla kufika katika banda la TBS ili kupata elimu mbalimbali zinazohusiana na viwango, ubora wa bidhaa na huduma tunazozitoa. Pia tunatoa huduma za usajili wa majengo na huduma nyingine zinazohusiana na majukumu ya TBS,” amesema Mwakasonda.

Amesisitiza kuwa wajasiriamali hawapaswi kuona uthibitishaji wa bidhaa kama kikwazo, bali wanapaswa kuuchukulia kama fursa ya kukuza biashara, kuongeza thamani ya bidhaa na kujenga imani ya walaji.

Kwa mujibu wa Mwakasonda, uthibitishaji wa bidhaa na upatikanaji wa Alama ya Ubora kwa wajasiriamali kupitia utaratibu wa Serikali unatolewa bure, hivyo amewataka kutumia fursa hiyo kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika soko.

Kwa upande wao, wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo wamepongeza elimu inayotolewa na TBS, wakisema imewasaidia kuelewa kwa kina hatua wanazopaswa kuchukua ili bidhaa zao zikubalike katika masoko yenye ushindani.

Khadija, mchakataji wa bidhaa za mwani, amesema elimu hiyo imempa uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na kuthibitisha bidhaa, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara yake.

“Elimu hii imenisaidia kuelewa zaidi umuhimu wa kuthibitisha bidhaa ninazozalisha. Nimepata uelewa kwamba Alama ya Ubora inaongeza imani kwa mteja na inaweza kusaidia bidhaa yangu kufikia masoko makubwa zaidi,” amesema.

Amesema awali baadhi ya wajasiriamali walikuwa wakijikita zaidi katika uzalishaji bila kuwa na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa ubora, ufungashaji, taarifa sahihi za bidhaa na uthibitishaji, lakini elimu ya TBS imewapa mwanga wa namna ya kuboresha bidhaa zao.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini umeendelea kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa elimu kwa wananchi na wazalishaji, huku banda la shirika hilo likitumika kama kituo cha kupata maarifa kuhusu viwango, ubora na taratibu mbalimbali za uthibitishaji.

Katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kusisitiza uzalishaji wenye tija, kuongeza thamani ya mazao na kukuza bidhaa zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa, elimu hiyo inatajwa kuwa muhimu katika kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao.

Kwa wajasiriamali, Alama ya Ubora si nembo tu kwenye kifungashio cha bidhaa, bali ni ishara ya ubora inayoweza kujenga imani ya mlaji, kuongeza ushindani na kufungua milango ya masoko mapya.

TBS imesisitiza kuwa jukumu lake haliishii katika ukaguzi wa bidhaa pekee, bali linaenda sambamba na kutoa elimu na kuwajengea uwezo wazalishaji ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi mahitaji ya soko.

Hivyo, wajasiriamali na wananchi wametakiwa kutumia fursa ya Maonesho ya Nane Nane kufika katika banda la TBS, kupata elimu na kufahamu hatua wanazoweza kuchukua ili bidhaa zao ziwe na ubora unaokubalika na kuwa na nafasi kubwa zaidi katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »