Na Oscar Assenga Tanga
TUME ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), imeadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, ikijivunia mchango wake katika kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, ikiwamo kuzalisha wataalamu wanaochangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza jana wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 40.
Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni kuwawezesha wataalamu na wabunifu mbalimbali ambao kwa sasa wanatumia ujuzi na maarifa yao kutengeneza suluhisho za changamoto zinazolikabili Taifa.
“COSTECH tunajivunia mafanikio mengi sana, lakini kubwa zaidi ni kuzalisha wataalamu mbalimbali wanaolisaidia Taifa letu,” alisema Dkt. Nungu.
Alimtaja mmoja wa wataalamu hao kuwa ni Dkt. Cecilia China, msomi kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ambaye kwa sasa anamiliki kampuni na anatarajia kuanzisha kiwanda cha dawa za kusindika ngozi kwa kutumia malighafi inayotokana na maganda ya korosho.
Dkt. Nungu alisema hatua hiyo ni mfano wa namna sayansi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kutumika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuibua fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Aidha, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Tanga, hususan Jiji la Tanga, kujitokeza kwa wingi kutembelea maonyesho hayo ili kujifunza na kuona teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na wataalamu na wabunifu wa Kitanzania.
“Niwaombe wakazi wa Mkoa wa Tanga, hususan wakazi wa Jiji la Tanga, mje kwa wingi kutembelea maonyesho haya ili muone teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na wataalamu kutoka hapa nchini kwetu. Tupo hapa hadi Agosti 24, karibuni sana,” alisema.
Maonyesho hayo yanaendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga, yakihusisha taasisi na wadau mbalimbali wa elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.
EmoticonEmoticon