Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usalama wa Kidijitali na Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni kwa Waandishi wa Habari Wanawake yaliyofanyika mjini Morogoro.

Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usalama wa Kidijitali na Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni kwa Waandishi wa Habari Wanawake yaliyofanyika mjini Morogoro.
Washiriki wa mafunzo ya usalama wa kidijitali kwa waandishi wa habari wa kike wakipiga picha ya pamoja
Na Elizabeth Cosmas, Morogoro
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umeendesha mafunzo maalumu ya Usalama wa Kidijitali na Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni kwa Waandishi wa Habari Wanawake, yakilenga kuimarisha uwezo wao wa kutumia mazingira ya kidijitali kwa usalama, kujiamini na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma.
Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoanza kufanyika Julai 6, 2026 mjini Morogoro, yamewaleta pamoja waandishi wa habari wanawake kutoka Klabu za Waandishi wa Habari mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya majukwaa ya mtandaoni katika kazi za uandishi wa habari.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini ili waweze kuhimili na kujilinda wanapokutana na changamoto mbalimbali katika mazingira ya kidijitali.
“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini, kuwasaidia namna ya kuhimili na kujilinda wanapokutana na changamoto hizo. Kwa kulitambua hilo, UTPC tumeanzisha mfumo wa ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari ili kuwajengea weledi zaidi katika kazi zao,” amesema Simbaya.
Amesema ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano umeleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya habari kwa kurahisisha upatikanaji na usambazaji wa taarifa, lakini pia umeongeza changamoto mpya zinazowakabili waandishi wa habari, hususan wanawake.
Amesema kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari wataweza kuongeza uelewa wa namna ya kujilinda dhidi ya vitisho vya kidijitali na kutumia teknolojia kwa usalama zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Washiriki wamejengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidijitali ikiwemo unyanyasaji wa mtandaoni, udukuzi wa akaunti, ufuatiliaji usio salama, vitisho vya mtandaoni, ukatili wa kijinsia unaofanyika kwenye majukwaa ya kidijitali pamoja na uvunjifu wa faragha.
Aidha, washiriki wamepata maarifa na mbinu za kuimarisha usalama wao wa kidijitali, ikiwemo kulinda akaunti za mitandao ya kijamii na barua pepe, kutumia nywila salama, uthibitishaji wa hatua mbili (Two-Factor Authentication), kutambua ulaghai wa mtandaoni (phishing), pamoja na kulinda taarifa binafsi na usiri wa vyanzo vya habari.
Washiriki pia wamejengewa uelewa kuhusu namna ya kutambua vitisho vinavyohusiana na ukatili wa kijinsia mtandaoni, hatua za kuchukua wanapokumbana na changamoto hizo, pamoja na kufahamu huduma za msaada wa kisheria na kisaikolojia zinazopatikana.
Akielezea manufaa ya mafunzo hayo, mshiriki Ednah Kahema amesema yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wake kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi na matumizi salama ya teknolojia.
“Mafunzo yamenisaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika ulinzi wa taarifa zangu binafsi. Pia nitajitahidi kuhakikisha kuwa nawaambia wasikilizaji namna bora ya kuhakikisha wanajilinda dhidi ya wahalifu mtandaoni au kujilinda dhidi ya link za uongo,” amesema Kahema.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “Kuwapa Nguvu Waandishi wa Habari kwa Ajili ya Jamii Zenye Taarifa” (Empowering Journalists for Informed Communities) unaotekelezwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kusaidia Tasnia ya Habari (International Media Support - IMS), kwa lengo la kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari na kukuza upatikanaji wa taarifa sahihi katika jamii.














EmoticonEmoticon