TBS YATOA ELIMU YA UTHIBITISHAJI WA BIDHAA KWA WAJASIRIAMALI SABASABA

July 07, 2026
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu na kuwahamasisha wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kukidhi matakwa ya sheria za viwango na kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika soko la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TBS, Neema Mtemvu, amesema ushiriki wa shirika hilo unalenga kuwafikia wafanyabiashara, hususan wajasiriamali wadogo, ambao bado hawajapata uthibitisho wa ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Amesema TBS ni mdau muhimu wa maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda, hivyo ipo tayari kuwasaidia wajasiriamali kufikia viwango vinavyotakiwa kisheria ili kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa salama, zenye ubora unaokubalika na zinazoweza kushindana sokoni.

“Tupo hapa kuhamasisha wafanyabiashara hawa waweze kukidhi vigezo vya ubora wa bidhaa zao. Tunatambua kuwa wengi wao ni wajasiriamali wadogo na wanahitaji msaada wa kitaalamu ili kufikia viwango,” amesema Mtemvu.

Amefafanua kuwa mjasiriamali anayehitaji kuthibitisha ubora wa bidhaa zake anatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kisha kuwasilisha maombi TBS, ambapo mchakato wa uthibitishaji huanza mara moja.

Mtemvu amesisitiza kuwa hakuna sababu kwa wajasiriamali kushindwa kukidhi viwango, akieleza kuwa TBS imeweka mazingira rafiki ya kuwasaidia wajasiriamali kupata huduma hizo kwa urahisi.

Ameongeza kuwa uthibitishaji wa ubora wa bidhaa si tu unalinda afya na usalama wa watumiaji, bali pia unafungua fursa za masoko mapana kwa wazalishaji na kuongeza imani ya walaji kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »