OFISI YA WAZIRI MKUU NA TAASISI YA CHAKULA NA LISHE TANZANIA KUSHIRIKIANA KUANDAA MPANGO WA LISHE TAIFA

July 01, 2026

 Na Mwandishi wetu- Dodoma 




Na Mwandishi Wetu- Dodoma


Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na  Lishe  Tanzania  (TFNC) Bi. Debora Charwe amesema, Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa Mpango wa Muda Mrefu wa Lishe wa Taifa (NN-LTP)  ili kuongeza jitihada za sekta mtambuka  katika kuboresha utekelezaji wa  lishe kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.


Bi. Debora ameyasema hayo leo tarehe 30 Juni, 2026 wakati akifungua Warsha ya mafunzo kuhusu kuandaa mpango wa muda mrefu wa lishe wa Taifa (National Nutrition Long Term  Plan  2026-2050) ambayo  inafanyika jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia Juni 30 hadi Julai 02, 2026

Amesema, mafunzo hayo yanatolewa kwa Wataalam  kutoka ngazi ya Wizara mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu uandaaji wa  mipango ya muda mrefu  wa lishe  inayojumuisha sekta mtambuka pamoja na  kubadilishana uzoefu kusaidia katika usanifu, muundo na taratibu za utekelezaji wa Mpango wa muda mrefu wa Lishe wa Taifa.








Vilevile Bi. Debora amefafanua kuwa, mpango huo  unaandaliwa chini ya usimamaizi wa Ofisi ya Waziri  Mkuu  kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC)  na wadau wengine wa maendeleo kwa kuzingatia haja ya  kuifanya lishe kuwa moja ya kichocheo  na kipimo katika  kufikiwa kwa malengo ya Dira  ya Maendeleo ya Tanzania kufikia 2050. 

 Aidha, warsha hiyo imehusisha Afisa viungo wa lishe kutoka Wizara mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) pamoja na  Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

==MWISHO==

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »