Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kwa kufikia malengo kwenye ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha miaka minne mfululizo ambapo amewataka kutumia mapato hayo kujenga miradi mikubwa ya kimkakati.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 24 juni, 2026 wakati akihutubia Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) 2024/25 ambapo wamepata hati safi.
Mhe. Mtanda amesema ni wakati sasa kwa halmashauri kuwekeza kwenye miradi mikubwa ambayo italeta makusanyo makubwa zaidi na kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato badala ya kujenga miradi mingi midogo pekee ambayo kimsingi haitumiki kurejesha fedha.
"Tumieni asilimia 40 ya makusanyo yenu kwa mujibu wa sheria kufanya hata mradi mmoja mkubwa ambao utakuwa alama kama wa uwanja wa mpira ambao mtajihakikishia ukusanyaji wa mapato kwa siku za mbeleni na sio kubaki na miradi midogo tu." Mhe. Mtanda.
Aidha, amewataka halmashauri hiyo kumaliza tatizo la maji kwenye hospitali ya wilaya ndani ya siku 14 kwa kuhakikisha wanaongeza wigo wa usambazaji kutoka kwenye chanzo cha kisima kirefu cha mita 24 kilichojengwa na wahisani Doris Mollel Foundation ili yafike katika majengo yote ya kutolea huduma.
Naye, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Mwanza Ndugu Richson Ringo amesema katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2024/25 halmashauri ya wilaya ya Kwimba imepata hati safi na kwamba mwenendo huo ni wa miaka mitano mfululizo.
Ameongeza kuwa pamoja na halmashauri hiyo kupata hati safi za ukaguzi kwa miaka 3 mfululizo lakini wanapaswa kuifanyia kazi hoja moja ya muda mrefu, pamoja na kujibu hoja na mapendekezo 36 yaliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ambavyo wamezijibu hoja 35 kati ya 79 zilizoibuliwa.




EmoticonEmoticon