TANESCO YAANZA UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA WAZIRI NDEJEMBI, TRANSFOMA KUBWA YAWASILI NGARA

May 19, 2026




 ðŸ“Œ Siku 10’baada ya Mbunge Bahemu kuibua changamoto ya kukatika umeme Ngara.


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kuanza kazi ya kufunga transfoma mpya yenye uwezo mkubwa katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera ili kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Hatua hiyo inakuja ikiwa zimepita siku tisa tangu Waziri Ndejembi alipolielekeza shirika hilo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja linapeleka transfoma kubwa kufuatia malalamiko ya kukatika kwa umeme yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mhe. Dotto Bahemu.

Leo Mei 19, 2026, transfoma hiyo kubwa imewasili katika kituo cha kupozea umeme cha Djululigwa wilayani Ngara huku wataalamu wa TANESCO wakianza kazi ya kuifunga.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Ngara, Eng. Amani Chidundo amethibitisha kuwasili kwa transfoma yenye uwezo wa 5MVA na kueleza kuwa kazi ya kuifunga inatarajiwa kuchukua takribani saa 12 kukamilika.


Eng. Chidundo amesema changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani humo ilikuwa ikitokana na transfoma ya awali yenye uwezo wa 3MVA kuzidiwa uwezo kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme.

Akishuhudia kazi ya ufungaji wa transfoma hiyo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ngara ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kusikiliza na kufanyia kazi kwa haraka changamoto ya wananchi wa Ngara.

“Leo tunapokea transfoma kubwa inayoenda kuondoa changamoto ya WanaNgara. Tuombe wananchi mpokee na tutoe shukurani kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhua Hassa, Waziri pamoja na Mbunge kwa kuletewa mtambo mkubwa wa transfoma kuhakikisha zile changamoto tulizokuwa tukizipata, zinakwenda kupungua” amesema Mkubila.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »