Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania kimeanzisha mashindano ya uchoraji yanayolenga kuhamasisha jamii, hususan watoto na vijana, kueleza hisia zao kupitia sanaa kufuatia tukio la mlipuko lililotokea nchini Iran mwezi Februari mwaka huu, ambapo Shule ya Msingi ya Minaab ililipuliwa na kusababisha vifo vya wanafunzi 168.
Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Hafisa wa Uhusiano kwa Umma wa kituo hicho, Amani Salum, amesema jumla ya shule 50 zimeshiriki katika mashindano hayo huku wanafunzi zaidi ya 200 wakishiriki kuonyesha vipaji vyao kupitia michoro mbalimbali yenye ujumbe wa amani, mshikamano na upendo.
Amesema kati ya washiriki hao, washindi 40 wamepatikana na wanatarajiwa kupatiwa zawadi maalum ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kutumia sanaa kuelimisha jamii na kuwasilisha ujumbe wenye manufaa.
Kwa upande wake, Jaji wa mashindano hayo ambaye pia ni mtaalamu wa masomo ya sanaa za ufundi, Dkt. Eric Mgema, amesema michoro ina nafasi kubwa katika jamii kwani husaidia kueleza hisia na fikra za watu kwa njia rahisi na yenye kugusa jamii kwa urahisi zaidi.
Dkt. Mgema amesema sanaa ya uchoraji ni moja ya njia muhimu za mawasiliano zinazoweza kubeba ujumbe mzito wa kijamii na kuhamasisha watu kutafakari kuhusu matukio mbalimbali yanayotokea duniani.




EmoticonEmoticon