Na Mwandishi wetu,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt.James Mataragio, ametembelea maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea jijini Dodoma.
Hayo yamefanyika katika siku ya pili tangu kuanza kwa maonesho hayo Aprili 20, 2026, ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya nishati wanashiriki kuonesha huduma, teknolojia na ubunifu wao.
Katika maonesho hayo, Dkt. Mataragio amepata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya nishati, akijionea shughuli na maendeleo yanayofanywa katika sekta hiyo nchini.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Dkt. Mataragio amesisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa, akibainisha kuwa rasilimali hizo zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa nishati na mapato ya Serikali.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia, ili kuwavutia wawekezaji zaidi na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Aidha, amehimiza taasisi na wadau wa sekta hiyo kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia mpya, na kujenga ushirikiano utakaosaidia kuendeleza uchimbaji, uchenjuaji na matumizi bora ya mafuta na gesi nchini.
Katika maonesho hayo, Dkt. Mataragio aliambatana na Bi. Ziana Mlawa, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Nishati, ambapo ameshiriki katika kutembelea mabanda na kujionea shughuli mbalimbali zinazooneshwa na wadau wa sekta hiyo.







EmoticonEmoticon