JIJI LA TANGA LAWATAKA WENYE MABASI HADI FEBRUARI 28 WAWE WAMEHAMIA STENDI YA KANGE

February 04, 2026

 


Na Paskal  Mbunga, Tanga.

Halmashauri ya Jiji la Tanga (TCC) imetoa muda hadi Februaru 28, ofisi za makampuni ya mabasi yaliyoko jijini Tanga yawe yamehamia katika stendi kuu ya Kange,  nje kidogo ya jiji hili.

Marufuku hiyo inaanza rasmi tarehe 28 Februari, mwaka huu.


Akizungumza katika kikao cha  madiwani kilichofanyika leo jijini Tanga, Mstahiki Meya wa Jiji, Mustafa Seleboss alisema kwamba  tangazo la kutotumiwa stendi kuu ya Ngamiani lilitolewa miaka mingi iliyopita, lakini lilipuuzwa na wahusika bila kuchukuliwa hatua.

"Sasa ni marufuku baada ya tarehe 28 mwezi huu kwa gari lolote la kubeba abiria kwa maana mabasi kuweka ofisi zao hapa jijini kwani wanatakiwa kuweka katika stendi kuu ya Kange na siyo Ngamiani.  

Alisema uongozi wa jiji umefanya ukarabati mkubwa katika stendi ya Kange na kukaribisha uwekezaji wa ndani na nje ya mkoa wa Tanga.

Mstahiki Meya alimwomba Mkuu wa wilaya ya Tanga,  Dadi Kolimba kulipa umuhimu wa kipekee suala la watakao kwenda kinyume cha agizo la uzuiaji wa magari ya abiria (mabasi) kuendelea kutumia stendi ya Ngamiani.

Katika hatua nyingine, Diwani wa kata ya Maweni alikieleza kikao hicho kwamba maisha ya wananchi wa kata ya Maweni yako hatarini kiafya baada ya kiwanda jirani kutoa hewa chafu na kuchafua hali ya mazingira.

Kwenye kikao hicho ambacho ni cha robo ya mwisho wa mwaka,  Diwani Joseph Colvas aliwaeleza wajumbe kwamba kata ya Maweni iko hatarini kupata magonjwa ya milipuko kutokana na kuvuta hewa chafu inayozalishwa katika kiwanda kimojawapo jijini hapa.

(Mwisho).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »